Posted Date::2/25/2008
CCM, Chadema wavutana
Na Mussa Juma, Kiteto
MATOKEO ya mwanzo ya uchaguzi mdogo wa ubunge uliofanyika jana katika Jimbo la Kiteto, yanaonyesha mgombea kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Victor Kimesera, anaongoza dhidi ya mpinzani wake mkuu, Benedict Nangoro wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika uchaguzi huo.
Hata hivyo, CCM wanadai kuwa mgombea wao anaendelea kuzoa kura katika kata kadhaa, hivyo kuwa na uhakika kwamba ataibuka mshindi na kukirudisha kiti hicho mikononi mwao.
Hadi kufikia jana wakati tunaenda mtamboni, majira ya saa 3:00 usiku, Kimesera ambaye ni Mkurugenzi wa Baraza la Wazee wa Chadema, alikuwa akiongoza katika baadhi ya vituo vilivyopo katika kata saba kati ya kata 15 za jimbo hilo kwa kupata kura 6,149 na kumwacha kwa mbali mgombea wa CCM, Nangoro aliyepata kura 3,672.
Kata hizo, ni Kibaya, Bwagamoyo, Lengatei, Matui, Njoro, Olboroti na Partimbo.
Matokeo ya vituo vyote vilivyoko katika Kata ya Kibaya iliyoko mjini Kiteto, hadi kufikia jana jioni, ndiyo pekee yalikuwa yamepatikana.
Katika kata hiyo iliyokuwa na wapigakura 1,605, Kimesera alishinda uchaguzi huo kwa kupata kura 1,153 na kuwaacha kwa mbali Nangoro wa CCM aliyeambulia kura 450. Jumla ya waliojiandikisha katika kata hiyo, ni watu 3,092.
Kutokana na matokeo hayo, mamia ya wafuasi wa Chadema na wa vyama vingine vya upinzani, walimiminika mitaani na kuanza kusherehekea kwa amani ushindi huo.
Hali hiyo iliwafanya askari wa Kutuliza Ghasia (FFU) kuingilia kati na kuanza kuwatawanya wafuasi hao.
Hata hivyo, katika Kata ya Partimbo ambako ni ngome ya CCM, mgombea wao, Nangoro alikuwa akiongoza kwa kura 1,033 dhidi ya kura 787 alizopata Kimesera wa Chadema.
Taarifa hizo zinaeleza kwamba katika Kata za Dosidosi na Engusero ambayo ni maeneo ya wafugaji CCM inaongoza ingawa hazikusema kwa kiasi gani cha kura.
Hata hivyo, kwa mujibu wa Msimamizi wa Uchaguzi jimboni hapa, Festo Kang'ombe, matokeo kamili ya uchaguzi huo, yatatolewa leo saa 5:00 asubuhi.
Katika matokeo hayo ya awali ya baadhi ya vituo katika Kata ya Bwagamoyo, mgombea wa Chadema, alikuwa akiongoza kwa kupata kura 1,055 dhidi ya kura 706 alizopata mgombea wa CCM.
Katika Kata ya Lengatei, Chadema ilikuwa imepata kura 234 wakati wa CCM alipata kura 113. Kata ya Matui, Chadema (kura 1,602), CCM (kura 685), Kata ya Njoro, Chadema (kura 496), CCM (kura 307), Kata ya Olboroti Chadema (kura 822), CCM (kura 378) na Kata ya Partimbo, CCM (kura 1,033), Chadema (kura 787).
Hata hivyo, uchaguzi huo ambao ulifanyika kwa amani, ulitawaliwa na mapungufu kadhaa katika baadhi ya vituo vya kupigia kura.
Baadhi ya mapungufu hayo ni katika Kituo cha Kaloleni, zaidi ya wapigakura 50 walishindwa kupiga kura kutokana na majina yao kutoonekana kwenye orodha ya wapigakura licha ya kuwa na shahada.
Kata ya Matui ambayo ni moja ya kata yenye wapigakura wengi, kulikuwa na upungufu wa tatizo la upungufu wa fomu namba 21 'B' ya matokeo ya jumla hasa katika kituo cha Azimio.
Hata hivyo, akizungumza na mwandishi wa habari hii, Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kiteto, Kang'ombe alikiri kuwapo na mapungufu katika baadhi ya vituo, lakini akasema mengi yalipatiwa ufumbuzi.
"Ni kweli kulikuwapo na upungufu katika baadhi ya vituo kwa wapigakura kutokana majina yao, lakini kulitokana na wao kutokuwa makini katika kutafuta majina yao na matatizo ya kibinadamu wakati wa uchapaji wa orodha ya wapigakura," alisema Kang'ombe.
Katika vituo vyote vya kupigia kura jana, kulikuwapo na askari wa FFU hali iliyosababisha uchaguzi kuwa shwari wakati wote.
Tuma maoni kwa Mhariri