Kiteto: Chadema ni kilio
2008-02-25 17:10:50
Na Simon Mhina, Kiteto
Simanzi imewakumba wanachama na mashabiki wa chama cha upinzani cha CHADEMA wilayani hapa, baada ya kibao kugeuka ghafla na matokeo ya uchaguzi kuonyesha mgombea wa ubunge wa chama hicho, Bwana Victor Kimeseara, amepigwa bao na yule wa CCM, Bwana Benedict Nangoro.
Kwa mujibu wa matokeo hayo yaliyopatikana kutoka katika maeneo tofauti jimboni humo, hadi kufikia asubuhi ya leo, mgombea wa CCM alikuwa akipeta kwa kuzoa kura zinazotajwa kufikia 14,000, dhidi ya kura 13,000 za mgombea wa CHADEMA.
Taarifa hizo zilizothibitishwa na baadhi ya viongozi wa CHADEMA zimedai kuwa, matokeo hayo ni ya kata zote isipokuwa moja ya Krash, ambayo iko mpakani mwa wilaya hiyo na Handeni.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii, kiongozi mmoja wa CHADEMA amesema hata kama watazoa kura nyingi katika kata hiyo ya Krash, bado hawataweza tena kumpiku mgombea wa CCM, kutokana na ukweli kuwa kura zilizopo hazifiki 1,000.
``Tumeanguka... hicho ndicho ninachoweza kusema,`` amesema kiongozi mmoja wa CHADEMA wakati akizungumza na Alasiri leo asubuhi.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa CHADEMA Bw. Zitto Kabwe, amekiri kushindwa kwa chama chake, lakini akatilia mashaka juu ya daftari la kudumu la wapiga kura.
Zitto ametilia mashaka daftari hilo kutokana na madai kuwa watu wengi hawakupata haki yao ya kupiga kura na hivyo kuhisi kuwa kuna hujuma imefanyika.
Hadi wakati tukienda mitamboni, matokeo rasmi ya uchaguizi huo yalikuwa bado hayajatangazwa.
Maeneo ya mengi ya mjini Kiteto yalikuwa kimya leo hii baada ya habari za kushindwa kwa mgombea wa CHADEMA kujulikana.
Matokeo ya vituo mbalimbali mjini Kiteto yameonyesha kuwa mgombea wa CHADEMA ndiye aliyeibuka kidedea baada ya kujizolea kura nyingi dhidi ya mpinzani wake.
Aidha, utulivu huo umeelezwa kuwa umechangiwa vilevile na taarifa zilizokuwa zikienezwa na baadhi ya makada wa CCM, waliokuwa wakizunguka kwenye majumba ya watu wao na kuwapa taarifa njema za ushindi, huku wakiwasihi kutulizana badala ya kushangilia mitaani, lengo ikiwa ni kuepuka kuzuka kwa fujo.
Katika hatua nyingine, imeelezwa kuwa kuharibika kwa helikopta ya CHADEMA katika siku ya mwisho ya kampeni, kumechangia kwa kiasi fulani, kushindwa kwa mgombea wao.
Jumamosi, helikopta iliyokuwa ikitumiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA.
Bw. Freeman Mbowe na mgombea wao, Victor Kimesera iliharibika mjini Dodoma na kuwafanya washindwe kuitumia katika kuwakusanya watu wao maeneo ya vijijini kama ilivyotazamiwa.
``Sio siri, lile dege lilikuwa likisaidia sana katika kuwakusanya watu mikutanoni na kuwaelezea sera za mgombea wa CHADEMA... nadhani waliwakosa baadhi ya watu pale lilipoharibika na matokeo yake CCM wakapata mwanya wa kutumia helikopta yao katika kuwawezesha kushinda,`` akasema mwananchi mmoja wa mjini Kiteto, aliyejitaja kwa jina la Alphonce Ernest.
SOURCE: Alasiri