Ritz,
Ahsanta nyingi zimwendee Sheikh Mohammed,ama hakika hii shughuli ni ndefu mno na ni nzito yataka kutuama kwa yakini ili kufahamu na kuzingatia. Nami sitaki kuwa kati ya wale wanaotaka kujipunja!ahaha!!
Gombesugu,
Marehemu Malima alikuwa na msemo akisema, ''Mtu akikutukana ulevini na wewe mtukane hapo hapo
la ukimsubiri akiwa mzima atasema alikuwa kalewa.''
Nimerushiwa kijembe ati nikiandika tena nisisahau kisa cha yule bibi wa baibui.
Sikutaka kuchelewesha nami nikajibu kuwa endapo nitaandika tena nitaandika
mkasa wa Abdu Sykes na ''intelligence surveillance'' alowekewa baada ya uhuru.
Akanivamia mtu na kusema kuwa yeye Abdu nani asiwekewe watu wa kumchunguza.
Hii ndiyo hatari ya kutojua historia ya nchi yetu.
Sasa katika majibu ya kijuba kama haya ndipo wanapopunjika watu hawa.
Laiti angeniuliza kwa utaratibu vipi ilikuwa mzalendo kama huyu si yeye tu bali baba yake
na wadogo zake wote walikuwa katika harakati akaja kuwa ''target'' akaja kuwa ''suspect''
angelipata mengi.
Lakini kuna uoga nadhani unawakumba ninapofunguka (kutumia lugha ya JF) hofu inawajia
wanaogopa kusikia mengi ambayo huenda yakawatia simanzi.
Hawa ndugu zetu hawajui lakini katika wanarakati wa TANU hakuna ambae hakula fadhila
za Abdu kuanzia Chief Marealle, Fundikira, Dunstan Omari nk. na si kwa kuwa Abdu alikuwa
na fedha nyingi sana.
La hasha alikuwa mtu karimu na muungwana kweli.
Hapa panatosha.
Unajua Abdu hadi anaingia kaburini hakupata kusema kuwa yeye ndiye aliyeasisi TANU au kusema
kuwa African Association aliasisi baba yake nk. nk.
Mwaka 1988 niliandika ''memoriam'' ya Abdu Sykes katika Africa Events miaka 20 baada ya kifo chake.
Daily News na Uhuru walipata shida sana kutoa kumbukumbu fupi waliyopelekewa kwa kusema ati iweje
historia ya nchi hii inafunganishwa na Abdulwahid Sykes?
Yeye ni nani?
Ni kweli alikuwa rafiki wa Nyerere?
Inabidi tuulize kwanza ukweli huu kabla hatujachapisha.
Na nafasi gazetini ilikuwa ya kununua.
Ahmed Rashad Ali siku alipokutana na mimi baada ya kuisoma na ilikuwa katika sala ya Eid Msikiti wa
Kitumbini, Mzee Rashad ambae alikuwa rafiki yake kipenzi alinikumbatia na machozi yakimtoka.
Mzee Rashad alinambia, ''Mohamed usitukumbushe habari za Abdu wewe hujapatapo kuona mtu kama
Abdu...''
Hatuwatukuzi hawa wazee kwa kuwakweza.
Hawa watu walikuwapo na wamefanya makubwa.
Abdu hakuingia katika harakati achume fedha.
Sana sana yeye ndiye aliyekuwa akitoa fedha kuipa TANU.
Insha Allah iko siku nitaeleza maziko ya Abdu yalikuwaje.
Yalivunja rekodi katika maziko ya Dar es Salaam.
Ule umma haukuja mazikoni kwa umaarufu wake au fedha zake.
Walikuja pale kwa ubinadamu wake na utu alokuwanao.
Ndiyo maana rafiki zake wakampa jina ''The Sweet Abdu.''
Gombesugu,
Dua yangu kwa Allah siku zote imekuwa asinihitimishe hadi nimeeleza yote niyajuayo kuhusu historia
ya uhuru wa Tanganyika na yale yalojiri baada.