20th October 2011- Jaribio la mwanzo la Nyerere kutaka kuivunja EAMWS lilikuwa mwaka 1963. Lakini jaribio hilo halikufanikiwa kwa sababu ya mpango uliopangwa na Mufti Sheikh Hassan bin Amir na kutekelezwa na Bilali Rehani Waikela, katibu wa EAMWS Tabora. Mwaka huu wa 1963 EAMWS ilifanya mkutano wake katika ukumbi wa Shule ya wasichana ya Aga Khan. Wajumbe wa mkutano huo walipowasili mjini Dar es Salaam walikuta uvumi kuwa wajumbe wa mkutano wa EAMWS watakamatwa na kuwekwa kizuizini. Chanzo cha uvumi huu hakikufahamika lakini haikuwa vigumu kuhisi.
Baada ya kuvunjwa kwa Baraza la Wazee wa TANU mwaka ule ilikuwa wazi kuwa Nyerere alikuwa amewatupa mkono washirika wake wa zamani na sasa alikuwa akitafuta wapya ili kujenga upya msingi wake wa siasa. Kutokana na mambo yalivyokuwa yakienda ilikuwa ni dhahiri washirika wake wapya hawatakuwa Waislam.Katibu wa EAMWS Tabora, Waikela alipowasili Dar es Salaam kuhudhuria mkutano aliitwa na Sheikh Hassan bin Amir. Mufti Sheikh Hassan bin Amir mbele ya Mzee Ali Comorian, alimfahamisha Waikela kuwa kulikuwa na njama zilizokuwa zikipikwa na Nyerere kumuungamiza yeye na Tewa Said Tewa ili kuvunja EAMWS ipatikane nafasi ya kuanzishwa jumuiya ya Kiislam ya Watanganyika itakayokuwa chini ya wanafiki.
Sheikh Hassan bin Amir alimwambia Waikela kuwa harakati za uhuru zilikuwa zinatekwa nyara na Wakristo kwa manufaa ya makanisa yao. Sheikh Hassan alimfahamisha Waikela kuwa ni lazima yeye afanye kila linalowezekana ili njama za Nyerere zishindwe. Waikela alimuuliza Sheikh Hassan bin Amir kwa nini amechaguliwa yeye kufanya kazi ile. Sheikh Hassan bin Amir alimuambia kuwa yeye ana imani na uwezo wake. Baada ya maneno hayo Sheikh Hassan bin Amir alinyanyua mikono yake juu na kumuombea dua Waikela. Nyerere alikuwa anamfahamu Waikela kwa kuwa alikuwa muasisi wa TANU na alikuwa ametoa mchango mkubwa katika kupigania uhuru.Nchi nzima hasa sehemu za Waislam kulikuwa mpango wa serikali wa kuwavunja Waislam nguvu na kuwakatisha tamaa.
Waikela, kama ilivyokuwa kwa viongozi wengine wa EAMWS alikuwa anasuguana na Mkuu wa Mkoa wa Jimbo la Magharibi, Richard Wambura. Kulikuwa na ujeuri kwa upande wa serikali walipokuwa wanashugulikia matatizo ya Waislam, mbali na mategemeo ya Waislam waliyokuwanayo kabla ya uhuru. Subira ya Waikela ilifikia kikomo pale Wambura alipowatukana Waislam katika mkutano wa hadhara. Baada ya kuhutubia Wambura, Waikela alipanda jukwaani na akaikumbusha serikali isiwe mwizi wa fadhila kwa kusahau jinsi Waislam walivyojitolea muhanga katika kudai uhuru. Serikali ikachukulia hotuba ya Waikela kama usaliti na yenye kuwashawishi Waislam wasiitii serikali. Ilikuwa katika hali hii Waikela mwanachama shupavu wa TANU alijitoa kwenye chama na akaamua kutumia nguvu zake kuwatumikia Waislam kupitia EAMWS.
Ilikuwa wazi kuwa Nyerere alikuwa na habari za msuguano kati ya serikali na Waislam kule Tabora na mtu ambae alikuwa akihusika na msuguano huo. Siku kabla ya mkutano wa EAMWS, Nyerere aliwaalika wajumbe wa mkutano Government House kwa chakula cha usiku. Hao waalikwa walikuwa wajumbe waliochaguliwa mahsusi. Waikela hakuwa mmoja wa hao waalikwa. Nyerere alichukua nafasi ile kuwashauri wajumbe wale waanzishe jumuiya ya Waislam wa Tanganyika ichukue nafasi ya EAMWS. Wajumbe hawa walipoleta katika mkutano hoja ya kuanzisha jumuiya ya Waislam wa Tanganyika, Waikela alisimama na kuipinga hoja ile. Alizungumza vilevile kuhusu uadui wa serikali kwa Waislam na Uislam.
Waikela alimaliza hotuba yake kwa kutoa changamoto kwa wajumbe wamuite Nyerere kwenye ufunguzi wa mkutano ili aje awaeleze wajumbe msimamo wake kuhusu kadhia hii ya chinichini baina ya serikali na Waislam. Baada ya kushindwa kwa hoja ya kuivunja EAMWS wajumbe wa mkutano ikaonekana kuwa ingekuwa vyema Nyerere aitwe kufunga mkutano ule na asomewe makubaliano yaliyofikiwa. Nyerere alifika kufunga ule mkutano na akakutana uso kwa uso na Waikela, ambae alimsomea maazimio ya mkutano. Waikela alimfahamisha Nyerere kuwa umoja kwa Waislam ni fardh ñ wajibu wa lazima. Ni kwenda kinyume na maamrisho ya Allah kuwagawa watu. Baada ya utangulizi huu Waikela huku akimnyooshea Nyerere kidole alieleza uadui unaoonyeshwa na serikali dhidi ya Waislam. Waikela alimaliza hotuba yake kwa kitisho. Alimwambia Nyerere ikiwa Waislam watamgeuka kupambanana yeye hatakuwa na uwezo wa kuwashinda.
Nyerere alitulia tuli pembeni mwa Rais wa Baraza la Tanganyika la EAMWS Tewa Said Tewa akimsikiliza Waikela. Aliposimama kujibu hotuba ya Waikela Nyerere kwa upole alisisitiza msimamo wa serikali wa kutoa haki na usawa kwa raia wake wote. Kwa kiasi fulani Nyerere alikuwa amefanikiwa kupunguza joto kati ya Waislam na serikali. Hotuba ya Waikela na ya Nyerere zikapewa umuhimu mkubwa katika radio. Waislam wengi wakajitokeza stesheni ya gari moshi Tabora kuja kumpokea shujaa Waikela. Alipewa heshima ile kwa kuwa na ujasiri wa kuweza kusimama kidete dhidi ya wale waliodhani kuwa wanaweza kuwakalia Waislam vichwani. Nyerere alihisi ameumbuka na hili lilimchoma moyo sana. Kuanzia hapa Nyerere hakumtazama Sheikh Hassan bin Amir kwa jicho jema. Alingoja nafasi yake ili alipize kisasi. Mwaka ukiofuata, tarehe 20 Januari, 1964 jeshi liliasi.
Nyerere alichukua fursa ile kuwatia kizuizini masheikh walioonekana wanapinga serikali na viongozi wa vyama vya wafanyakazi. Waikela alikuwa mmoja wa wale waliokamatwa na kuwekwa kizuizini. Nyerere kwa wakati ule hakuwa na nguvu ya kumgusa Mufti Sheikh Hassan bin Amir.Wakati ule mwaka wa 1963 shughuli za kueneza dini za EAMWS zilikuwa zikienda vizuri sana. Tabligh ilikuwa chini ya Sheikh Amir bin Juma kutoka Tanga na Wakristo wengi walikuwa wakirudi katika Uislam. Tabligh ilikuwa ikiongozwa kutoka kwa masheikh wa mikoa na wilaya. Fedha za kufanyia shughuli hizi zilikuwa zikichangwa na Waislam wenyewe. Mufti Sheikh Hassan Bin Amir yeye alikuwa akisomesha fikh, mantik, tauhid, na tafsir ya Qurían katika misikiti mbalimbali ya Dar es Salaam Wakati ule Katibu Mkuu wa EAMWS kwa Afrika ya Mashariki alikuwa V.M. Nazarali.
Mwezi Aprili 1964 ujumbe wa hali ya juu wa EAMWS ndani yake wakiwemo Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Said Omari Abdallah, Tewa Said Tewa, Katibu wa EAMWS Abdul-Aziz Khaki na mzee wa TANU Mzee Mwinjuma Mwinyikambi; Makisi Mbwana, Issa Mtambo, Omari Muhaji na Saleh Masasi waliondoka kwenda ziara ya nchi za Kiislam kutafuta msaada wa kujenga Chuo Kikuu cha Kiislam na kuanzisha uhusiano na nchi za Kiislam. Gamal Abdel Nasser alifurahishwa sana na ujumbe wa Tanganyika kiasi kwamba ingawa alikuwa katika matayarisho ya mapokezi ya Waziri Mkuu wa Urusi Kruschev, na ingawa ujumbe wa EAMWS ulikuwa wa kidini zaidi kuliko wa kiserikali, alikutana na ujumbe ule akaupatia ofisi, huduma za simu, na makatibu muhtasi ili waweze kutayarisha mipango yao kwa serikali ya Misri bila shida. Halikadhalika alimuagiza makamu wake Sharbasy afanye makubaliano na EAMWS kwa niaba yake. Serikali ya Misri ilikubali kugharamia ujenzi wa chuo hicho. Mkataba wa makubaliano ukatiwa sahihi mjini Cairo kati ya Tewa Said Tewa kwa niaba ya EAMWS na Makamu wa Rais wa Misri, Sharbasy kwa niaba ya serikali yake.
Serikali ya Misri iliahidi kujenga Chuo Kikuu cha Kiislam ambacho kitamilikiwa na kuendeshwa na EAMWS. Gharama ya mradi mzima uliuwa pauni milioni hamsini na tano za Ki-Misri. Baada ya kukamilisha kazi ile ujumbe ule uliondoka Cairo kuelekea Makka kufanya ibada ya hija. Baada ya kumaliza hija wajumbe wanne walirudi nyumbani na Tewa, Aziz Khaki, Sayyid Omar Abdallah wakaendelea na safari kwenda Aman, Jordan ambako walifanya mazungumzo na Mufti na Waziri wa Aukaf. Kutokea hapo ujumbe ulikwenda Kuwait ambako walikutana na Sheikh wa Kuwait kisha wakaenda Bhaghdad, Iraq na kukutana na rais wake, Abdisalama Arifek. Kutoka hapo ujumbe ulielekea Beirut, Lebabon ambako ulifanya mazungumzo na viongozi wa harakati za Kiislam. Baada ya kutoka Beirut ujumbe ule ulirudi tena Cairo kwa ajili ya kukamilisha makubaliano ya kujenga Chuo Kikuu.
Tarehe 20 Mei, 1964 ujumbe ulirejea Dar es Salaam na kupokelewa na viongozi wa EAMWS na Waislam kwa ujumla. Mkutano wa Halmashauri Kuu ya EAMWS ukaitishwa na Tewa Said Tewa akatoa taarifa yake kuhusu ujenzi wa Chuo Kikuu Cha Kiislam. Siku ya pili Tewa akaitisha mkutano wa waandishi wa habari na kutoa habari za kufurahisha za kujengwa kwa Chuo Kikuu Cha Kiislam kwa vyombo vya habari na kwa Waislam kwa ujumla. Kwa mafanikio haya Tewa akawa amejichimbia kaburi. Matokea haya yalijaza hofu kwa viongozi wa Kanisa. Kampeni za chinichini dhidi ya Tewa binafsi na uongozi mzima wa EAMWS zilianza.
Mara baada ya ujumbe wa EAMWS kurudi kutoka ziara yake, Nyerere alifanya mabadiliko katika baraza la mawaziri na Tewa Said Tewa, Mwenyekiti wa EAMWS upande wa Tanzania akajikuta nje ya serikali. Nyerere akamteua Tewa balozi wa Tanzania katika Jamuhuri ya Watu wa China. Mwezi Januari, 1965 Tewa alikwenda China kuanza kazi yake mpya. Inasemekana uteuzi wa wa Tewa kwenda China ulisababishwa na juhudi zake za kutaka kuwaunganisha Waislam kuwa kitu kimoja chini ya jumuiya moja yenye nguvu. Wakati ule ile mipango iliyopitishwa na mkutano wa Waislam mwaka 1962 ilikuwa ikitekelezwa vyema, shule zilikuwa zimejengwa Ilala, Kigogo na Kurasini, Dar es Salaam; shule zilikuwa zimejengwa Ruvu na Maneromango.
Shule hii ya Maneromango ilikuwa na umuhimu wa pekee kwa sababu hii ndiyo ilikuwa shule ya kwanza ya Waislam kujengwa Uzaramo. Shule za upili zilikuwa zikijengwa Dar es Salaam, Kinondoni na Moshi, Kibohehe. EAMWS ilikuwa vilevile imetiliana mkataba wa makubaliano na serikali ya Misri kuipa scholarship thelathini na tano kila mwaka kwa wanafunzi wa Kiislam kusoma Misri. EAMWS ilikuwa imejenga shule, misikiti, shule za ufundi na hosteli kwa ajili ya wanafunzi katika sehemu nyingi za Afrika ya Mashariki. Kwa hakika EAMWS ilikuwa ikifanya mambo ya maendeleo kwa Waislam.