Wanajamvi,
kuna habari za kufuja mali za EAMWS, mnajua zilisababisha nini na zilifanywa na nani?
Abdul Wahid na Sheikh Amir kuna mahali wanakutana katika chama nje ya TAA na TANU.
Mnajua ni wapi na ni nani kiongozi wa taasisi hiyo?
CC Zumbemkuu, Mag3, JokaKuu, Shariff Ritz, al maarufu Gombesugu, Jasusi, Wickama
Juhudi za Kuanzisha Chuo Kikuu cha Kiislamu chini ya EAMWS, 1964
APRILI 1964 ujumbe wa hali ya juu wa EAMWS ndani yake wakiwemo Sheikh Hassan bin Amir, Sheikh Said Omari Abdallah, Tewa Said Tewa, Katibu wa EAMWS Abdul-Aziz Khaki na mzee wa TANU Mzee Mwinjuma Mwinyikambi; Makisi Mbwana, Issa Mtambo, Omari Muhaji na Saleh Masasi waliondoka kwenda ziara ya nchi za Waislamu kutafuta msaada wa kujenga Chuo Kikuu cha Kiislamu na kuanzisha uhusiano na nchi za Kiislam.
Gamal Abdel Nasser alifurahishwa sana na ujumbe wa Tanganyika kiasi kwamba ingawa alikuwa katika matayarisho ya mapokezi ya Waziri Mkuu wa Urusi Kruschev, na ingawa ujumbe wa EAMWS ulikuwa wa kidini zaidi kuliko wa kiserikali, alikutana na ujumbe ule akaupatia ofisi, huduma za simu, na makatibu muhtasi ili waweze kutayarisha mipango yao kwa serikali ya Misri bila shida. Halikadhalika alimuagiza makamu wake Sharbasy afanye makubaliano na EAMWS kwa niaba yake.
Serikali ya Misri ilikubali kugharamia ujenzi wa chuo hicho. Mkataba wa makubaliano ukatiwa sahihi mjini Cairo kati ya Tewa Said Tewa kwa niaba ya EAMWS na Makamu wa Rais wa Misri, Sharbasy kwa niaba ya serikali yake.
Serikali ya Misri iliahidi kujenga Chuo Kikuu cha Kiislam ambacho kitamilikiwa na kuendeshwa na EAMWS. Gharama ya mradi mzima uliuwa pauni milioni hamsini na tano za Ki-Misri.
Baada ya kukamilisha kazi ile ujumbe ule uliondoka Cairo kuelekea Makka kufanya ibada ya hija. Baada ya kumaliza hija wajumbe wanne walirudi nyumbani na Tewa, Aziz Khaki, Sayyid Omar Abdallah wakaendelea na safari kwenda Aman, Jordan ambako walifanya mazungumzo na Mufti na Waziri wa Aukaf.
Kutokea hapo ujumbe ulikwenda Kuwait ambako ulikutana na Sheikh wa Kuwait kisha ukaenda Bhaghdad, Iraq na kukutana na rais wake, Abdisalama Arifek.
Kutoka hapo ujumbe ulielekea Beirut, Lebabon ambako ulifanya mazungumzo na viongozi wa harakati za Kiislam. Baada ya kutoka Beirut ujumbe ule ulirudi tena Cairo kwa ajili ya kukamilisha makubaliano ya kujenga Chuo Kikuu.
Tarehe 20 Mei, 1964 ujumbe ulirejea Dar es Salaam na kupokelewa na viongozi wa EAMWS na Waislamu kwa ujumla. Mkutano wa Halmashauri Kuu ya EAMWS ukaitishwa na Tewa Said Tewa akatoa taarifa yake kuhusu ujenzi wa Chuo Kikuu Cha Kiislamu. Siku ya pili Tewa akaitisha mkutano na waandishi wa habari na kutoa habari za kufurahisha za kujengwa kwa Chuo Kikuu Cha Kiislamu kwa vyombo vya habari na kwa Waislamu kwa ujumla.
Kwa mafanikio haya Tewa akawa amejichimbia kaburi. Matokea haya yalijaza hofu kwa viongozi wa Kanisa. Kampeni za chinichini dhidi ya Tewa binafsi na uongozi mzima wa EAMWS zilianza.
Mara baada ya ujumbe wa EAMWS kurudi kutoka ziara yake, Nyerere alifanya mabadiliko katika baraza la mawaziri na Tewa Said Tewa, Mwenyekiti wa EAMWS upande wa Tanzania akajikuta nje ya serikali.
Nyerere akamteua Tewa balozi wa Tanzania katika Jamuhuri ya Watu wa China. Mwezi Januari, 1965 Tewa alikwenda China kuanza kazi yake mpya. Inasemekana uteuzi wa wa Tewa kwenda China ulisababishwa na juhudi zake za kutaka kuwaunganisha Waislam kuwa kitu kimoja chini ya jumuiya moja yenye nguvu. Wakati ule ile mipango iliyopitishwa na mkutano wa Waislamu mwaka 1962 ilikuwa ikitekelezwa vyema, shule zilikuwa zimejengwa Ilala, Kigogo na Kurasini, Dar es Salaam; shule zilikuwa zimejengwa Ruvu na Maneromango. Shule hii ya Maneromango ilikuwa na umuhimu wa pekee kwa sababu hii ndiyo ilikuwa shule ya kwanza ya Waislamu kujengwa Uzaramo. Shule za upili zilikuwa zikijengwa Dar es Salaam, Kinondoni na Moshi, Kibohehe. EAMWS ilikuwa vilevile imetiliana mkataba wa makubaliano na serikali ya Misri kuipa scholarship thelathini na tano kila mwaka kwa wanafunzi wa Kiislamu kusoma Misri. EAMWS ilikuwa imejenga shule, misikiti, shule za ufundi na hosteli kwa ajili ya wanafunzi katika sehemu nyingi za Afrika ya Mashariki. Kwa hakika EAMWS ilikuwa ikifanya mambo ya maendeleo kwa Waislamu.
Uganda Tanzania Kenya
Shule 77 70 28
Misikiti 67 53 29
Shule za Ufundi 3 - -
Hosteli 1 - -
Chanzo: Utafiti
Baada ya Tewa kuondoka Bibi Titi Mohamed akachaguliwa kuwa makamu mwenyekiti wa tawi la EAMWS la Tanzania ili kuongeza nguvu makao makuu kwa kuwa mwenyekiti hakuwepo. Kutokuwepo kwa Tewa nchini kulileta ombwe ambalo ilibidi lijazwe. Ghafla palizuka uvumi kuwa Sheikh Abdallah Chaurembo alikuwa achukue uongozi wa EAMWS. Inasemekana nia yake ilikuwa ni kwanza kupata urais wa EAMWS na kisha achaguliwe kuwa Mufti wa Tanzania. 35 Uvumi huu ulidumu kwa karibu mwaka mzima hadi pale Tewa aliporudi kutoka Peking baada ya kujiuzulu ubalozi kuja kugombea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1965. Aliporudi Tewa alihojiwa na waandishi wa habari kuhusu uvumi ule na yeye jibu lake lilikuwa kuwa Muislamu yeyote mwenye sifa ya maadili mema ana haki ya kugombea nafasi yoyote katika uongozi wa EAMWS. Neno alilolitumia Tewa katika kumueleza mtu ambaye angeweza kuwaongoza Waislamu lilikuwa takwa, neno la Kiarabu kueleza mtu mcha-mungu.
Nikuanzia katika matukio haya ndipo tunaweza sasa kuanza kuchunguza jinsi Nyerere akiitumia serikali alivyoanza kuuhujumu umoja wa Waislamu kwa kutumia njama, hujuma za dhahiri na za kificho, magendo na kueneza uongo dhidi ya uongozi wa EAMWS, ambao ulionekana ni tishio kwa utawala wake. Wakati ule serikali nzima ilikuwa mikononi mwa Wakristo. Ukiwatoa Wazanzibari waliokuwa katika serikali ya muungano - Aboud M. Maalim, Waziri wa Biashara na Viwanda; Aboud Jumbe, Waziri Nchi; A.M. Babu, Waziri wa Ardhi, Makazi na Maji; Hasnu Makame, Waziri wa Habari na Utalii; Rashid Kawawa ambae alikuwa mtu wa karibu sana na Nyerere, waziri Muislamu katika baraza la mawaziri kumi na tano alikuwa Said Ali Maswanya, Waziri wa Mambo ya Ndani. Hali kama hii ya Wakristo kushika nyadhifa takriban zote za serikali ilikuja vipi? Jibu la swali hili linapatikana katika historia ya Tanganyika wakati wamisionari wa kwanza walipowasili nchini kuja 'kulistaarabisha bara jeusi' na halikadhalika katika historia ya TANU .
'Mgogoro' wa East African Muslim Welfare Society (EAMWS) wa Mwaka wa 1968
Uchochezi wa 'Mgogoro' wa BAKWATA
Kutokana na katiba ya mwaka wa 1957 lengo kuu la EAMWS ilikuwa ni 'kuutangaza Uislamu katika Afrika ya Mashariki'. EAMWS yenyewe ilikuwa ikijigamba kuwa uti wake wa mgongo ilikuwa ni tabligh, yaani utangazaji wa dini. Jumuiya hii iliyoanzishwa mwaka 1933 ilikuwa ya Waislamu wa mataifa yote katika uanachama na katika uongozi wake.
Katika uhai wake wa miaka thelathini na tano EAMWS ilijiweka mbali sana na siasa. Jumuiya hii ilishughulikia kuutetea na kuueneza Uislamu katika Afrika ya Mashariki. Lakini baada ya kutokea maasi ya Tanganyika Rifles mwaka 1964 yaliyopelekea viongozi wengi wa Kiislamu kuwekwa kizuizini, EAMWS ikawa imepoteza mwelekeo wake na kudhoofika. Baadhi ya matawi yaliyokuwa katika majimbo yakafungwa kwa woga na kukosa viongozi thabiti na kwa matawi mengine yalifungwa kwa sababu viongozi wake walikuwa wakichimbwa chinichini na serikali. Waislamu wengi walihisi vitisho vya serikali kwa hiyo waliogopa kuchukua uongozi wa EAMWS. Wengi waliogopa kuitumikia EAMWS kwa kuwa walihisi ofisi za jumuiya hiyo zilikuwa zikichukuliwa na serikali kama vituo vya upinzani dhidi yake. Kwa zaidi ya miaka mitatu toka ule mkutano wa mwaka 1963, EAMWS haikuweza kufanya mkutano wowote.
EAMWS ilipokuja kuitisha mkutano wake wa mwaka mjini Arusha mwaka 1966 kikajitokeza kikundi kutoka upande wa Tanzania kikidai EAMWS ijigawe, kila nchi iwe na mamlaka yake na ijitegemee yenyewe, yaani Tanzania, Kenya na Uganda zote ziwe mbalimbali. Kikundi hiki kilichokuwa kikidai utengano vilevile kikadai kuwa katiba ya EAMWS nayo iwe ya 'kizalendo'.
Hii ilikuwa na maana kuwa uongozi itabidi uifanyie katiba marekebisho ili kuiwezesha Tanzania kuwa huru ndani ya EAMWS. Wajumbe waliokuwa wanaona mbali kutoka Tanzania na wengine kutoka Kenya na Uganda, na kwa hakika mkutano mzima kwa ujumla walipinga kitendo hicho, wakidai kuwa kwa kufanya hivyo Waislamu wa Tanzania watakuwa wametengwa na umma wa Kiislamu wa Afrika ya Mashariki. Jambo hili likitokea, si tu litakuwa limewadhoofisha Waislam wa Tanzania peke yao, bali Waislamu wa Afrika ya Mashariki nzima. Wajumbe wa Kenya na Uganda walikuwa wanatambua kuwa kulikuwa na shinikizo kubwa kutoka serikali ya Tanzania kwa Watanzania kujitoa kutoka EAMWS. Halikadhalika ilikuwa inafahamika kuwa wajumbe wa Tanzania walikuwa wakifanya kazi chini ya shinikizo kali kutoka serikali ya Nyerere.
Haikuwa siri sana kuwa baadhi ya viongozi wa EAMWS walikuwa kisirisiri wakiandamwa na serikali. Lakini mkutano ule haukuzungumzia matatizo haya kwa kuwa hayo yalichukuwaliwa kama matatizo ya ndani ya nchi. Hata hivyo kwa ule moyo wa Kiislamu wa kuhurumiana, wajumbe wa Kenya na Uganda kwa faragha walionesha masikitiko yao kwa Tewa kuhusu ile hali iliyokuwa ikiwakabili Waislamu wa Tanzania. Wajumbe walipokuwa wakiondoka kurejea makwao, ilikuwa wazi kuwa serikali ya Tanzania ilikuwa ikiingilia kati EAMWS kiasi cha kuifanya jumuiya hiyo ishindwe kufanya kazi yake vyema na kupitisha maamuzi yake. Hali hii ilijidhihirisha wazi pale kwa kipindi kizima cha mkutano, makachero wa serikali walikuwa wamejitokeza kwa wingi mjini Arusha.
Haukupita muda ikadhihirika kuwa serikali ilikuwa imepania kuivunja EAMWS kwa kuwatumia Waislamu wachache walioteuliwa kwa kazi hiyo. Lengo likiwa ni kuanzisha taasisi mpya ambayo serikali itaweza kuiamuru. Ieleweke hapa kuwa kama ilivyokwisha elezwa hapo nyuma, serikali nzima ya Tanzania ilikuwa mikononi mwa Wakristo na watendaji hawa walikuwa wapo chini ya Kanisa. Hii ilikuwa na maana kuwa kilichotakiwa kuwepo ilikuwa taasisi ya Kiislamu ambayo Kanisa itaweza kuiamuru. Hii ilikuwa ni jambo lazima lifanyike ili kuwadhibiti Waislamu kama nguvu inayoweza kuleta mabadiliko ya siasa. Baada ya kuelewa hali hii ndipo sasa tunaweza kuuangalia kile kilichoitwa 'mgogoro' wa EAMWS ambao ulidumu kwa miezi mitatu ya mwisho ya mwaka wa 1968.
Ili tuweze kuuelewa vyema kisa kizima cha 'mgogoro' ni muhimu kwanza kuelewa chanzo chake, hadhi za wahusika wakuu na nafasi zao katika 'mgogoro' ule. Mwisho, ni muhimu kuweka bayana na kuchambua nafasi ya Julius Nyerere, serikali yake, chama cha TANU na vyombo vya dola katika 'mgogoro' ule. Hii itasaidia kuelewa kama kweli ulikuwepo 'mgogoro' katika EAMWS, au 'mgogoro' ulibambukizwa na watu katika TANU, serikali na ndani ya Waislamu wenyewe ili kuwadhoofisha Waislamu kwa nia ya kuwa usije Uislamu ukawa na nguvu katika Tanzania hivyo kuwawezesha Waislamu kushika madaraka ya nchi.
Mwaka wa 1967 Mwalimu Julius Nyerere alitangaza Azimio la Arusha hatua ambayo iliitia Tanzania katika siasa ya ujamaa. Sera hii mpya ya uchumi ilipokelewa vyema na wananchi. Mtu ambae hata alikuwa hajulikani, tena mwalimu wa shule ya msingi akijulikana kwa jina la Adam Nasibu ambae alikuwa katibu wa Bukoba wa EAMWS, alichukua nafasi hii kwa kuongoza maandamano hadi ofisi ya TANU ya Mkoa kumuunga mkono Mwalimu Nyerere na sera yake mpya ya uchumi ya Azimio la Arusha. Adam Nasibu inasemekana kuwa alisema ujamaa ni sawa na mafundisho ya Qur'an Tukufu. Adam Nasibu hakuishia hapo alikwenda mbele zaidi na kutoa 'miongozo kwa viongozi wote wa Kiislamu wa Bukoba akifafanua Azimio la Arusha'. Wasiokuwa Waislam walimuona Adam Nasibu kama Muislam mwenye mwamko mzuri wa kimaendeleo, na kwa kuwa yeye alikuwa ni kiongozi wa EAMWS, kuunga kwake mkono Azimio la Arusha kulionekana kama kitendo rasmi cha jumuiya hiyo kuunga mkono sera hiyo. Lakini kabla ya yeye kufanya haya, hakuna mtu aliyemjua mwalimu huyu wa shule kama mwanasiasa licha ya kuwa msomi mwenye uwezo wa kuchambua mambo.
Katika hali ya kawaida, uongozi wa EAMWS pale makao makuu Dar es Salaam ungelikasirishwa kidogo na kitendo cha Adam Nasibu cha ushabiki wa siasa. Lakini uongozi wa EAMWS haukumuonya kiongozi wake wa Bukoba kuhusu jambo lile ambalo dhahiri halikuwa la kupendeza katika jumuiya. Bila shaka uongozi wa EAMWS ulichelea kuwa kwa kufanya hivyo wangelionekana si uzalendo, hasa ukiichukulia jinsi wananchi walivyohamasika na Azimio la Arusha. Hata hivyo Waislamu siku zote ndiyo waliokuwa mbele katika kuongoza siasa. Makao Makuu walibaki kimya kama vile hakuna kilichotokea.
Tofauti na mwaka wa 1963 wakati Nyerere alipojaribu kufanya mapinduzi dhidi ya uongozi wa EAMWS, mwaka wa 1967 hali ya mambo yalikuwa yamebadilika sana yakimwendea Nyerere vyema. Serikali ilikuwa imedhibiti vyombo vyote vya habari ukiondoa gazeti la The Tanganyika Standard ambalo bado lilikuwa chini ya Lonrho. Nyerere alikuwa amemuweka Martin Kiama kama mkurugenzi wa radio ya taifa, na Benjamin William Mkapa kama mhariri wa magazeti mawili ya TANU, The Nationalist na Uhuru. Adam Nasibu aliandikwa katika magazeti na habari zake kutangazwa katika radio kwa ajili ya kitendo chake, hasa kuhusu yale maneno aliyosema kuwa ujamaa ni sawa na mafundisho ya Qur'an.
Katika hali ya mambo kama yalivyokuwa wakati ule hasa jinsi uhasama ilivyokuwapo baina ya serikali na Waislam, baadhi ya Waislam walimuona Adam Nasibu kama kibaraka anaetafuta umaarufu wa bure kwa kujipendekeza kwa TANU, Nyerere na serikali yake. Juu ya haya yote kile kitendo cha katibu wa Bukoba wa EAMWS kitakuja kuwaathiri vibaya jumuiya hiyo na uongozi wake wote pamoja na Mufti Sheikh Hassan Bin Amir.
Kwa wengine Adam Nasibu alionekana kama mzalendo na Muislamu mwenye 'uoni wa mbali'. Kwa ajili hii basi serikali ikamuona kama kiongozi wa baadae ambayo ingeweza kumtegemea wakati wa shida. Uongozi wa EAMWS makao makuu ukaonekana haupo pamoja na wananchi, wala haujali shida zao na uko mbali sana na sera za serikali. Lakini kwa hakika EAMWS kama taasisi ya dini isingeliweza kujitokeza na kuunga mkono Azimio la Arusha kwa kuwa hayo yalikuwa mambo ya siasa. Kwa kufanya hivyo ingelikuwa inakwenda kinyume na msimamo wake wa kutojiingiza katika siasa. Kwa zaidi ya robo karne toka iasisiwe EAMWS ilikuwa imejiweka mbali sana na mambo ya siasa ikishughulika na masuala ya Uislamu tu. Hata hivyo kuwa nje ya Azimio la Arusha kukaonekana kama kitendo cha kukosa uzalendo na kutoa picha kuwa jumuiya hiyo ilikuwa haijali maendeleo na ustawi wa watu wa Tanzania. Mambo yakawa yamevurugika zaidi kwa kuwa rais wa EAMWS, Tewa Said na makamo wake Bibi Titi Mohamed walikuwa katika baraza la mawaziri la Nyerere na wakapoteza nyadhifa zao za ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka 1965. Kwa ajili hii basi serikali ikawa inaeneza propaganda kuwa kwa kuwa Tewa na Bibi Titi walikuwa katika uongozi wa juu wa EAMWS, walikuwa wanatumia nafasi zao kujijengea himaya mpya kutoka kwa Waislamu dhidi ya Nyerere. Viongozi hawa ikawa lazima washughulikiwe na kuangamizwa. Mtu wa kufanya kazi hii hakuwa mwingine ila Adam Nasibu katibu wa EAMWS Bukoba, mwalimu wa shule ya msingi ambae elimu yake wala haikuwa kubwa. Adam Nasibu alikuwa tayari keshafanikiwa kufanya mapinduzi dhidi ya rais wa EAMWS, Tewa Said Tewa. Kutokana na vitendo vyake alikuwa ameidhihirishia serikali kuwa yeye angeweza kuwa mtumishi bora kwa dola kuliko ule uongozi wa EAMWS uliokuwa pale makao makuu Dar es Salaam ambao ulikuwa ukionekana umechoka.