Kaka yangu Jasusi,
Hakuna asiyefahamu umahiri wa Mwalimu katika hotuba hata kama haijaandikwa.
zomba hataki kuelewa kwa makusudi tu. Muulize kama aliwahi kuona au kusoma kokote hotuba ya Abdulwahid Sykes. Elimu ya Mwalimu na Abdu ilikuwa tofauti kama kichuguu na mlima Kilimanjaro. Mwalimu kwa jeuri yake na kujiamini alikokuwa nako asingeweza kuandikiwa hotuba na mtu kama Abdu ambaye hata elimu yake Mzee
Mohamed Said haiongelei sana zaidi ya kumsifia kuwa alikuwa na akili sana! Hotuba hii ninayoinukuu hapa chini aliitoa mwaka 1995 kwenye Mkutano Mkuu wa CCM ambao hatimaye ulimteua Mkapa kuwa mgombea Urais kwa tiketi ya CCM. Hakuwa ameiandika popote:
"Ukabila bado upo. Kwa hiyo, ukabila lazima uendelee kupigwa vita. Hapana kukaa na kusema "Tanzania hatuna ukabila". Hapana. Watu hatujawa Watanzania bado. Kwa hiyo, lazima tuendelee kuupiga vita. Na watu wana udini dini. Kuna watu kabisa wanatamani nchi hii iwe ya Kikristu, wajinga. Kuna watu wanatamani nchi iwe ya Kiislamu, wajinga. Natumia neno zuri wajinga, sisemi wapumbavu. Wajinga.
Tunataka rais wetu, akiwa Mkristu, ajue hatumchagui kwa sababu ya Ukristo wake. Akiwa Muislam, ajue hatukumchagua kwa sababu ya Uislam wake. Hatumchagui awe rais wa Wakristu wala awe wa Waislam, na tunataka hilo alikubali kwa dhati na alisimamie na ndiye kiongozi wetu. Alisimamie kwa dhati bila woga, ndiye kiongozi wetu.Katika nchi changa namna hii, ambayo watu haraka sana hukimbilia ukabila, haraka sana hukimbilia udini, tunataka kiongozi awe imara kabisa katika mambo haya." Niishie hapo kunukuu na ni mshukuru MSOMAJI RAIA wa Raia Mwema ya leo.