Wanajamvi,
Nimefuatilia mjadala huu nikidhani kuwa tunaijadili mada kama ilivyoletwa. Tofauti, naona takwimu za elimu na mengine yasiyo na uhusiano na mada. Ukifutailia utagundua kuwa MS anakwepa kujibu hoja na kutumbukiza mengine au zile mada zake zimewaingia vema baadhi yetu na kila mara wanazifikiri bila tafakuri.
Wanakosa tafakuri kwasababu makala za MS zinachanganya na zinahitaji utulivu na fikra kuzielewa na kuzinyumbulisha ili upate hitimisho alilokusudia. MS anauwezo sana wa kufanya majumuisho yanayoeleweka kiurahisi sana kwa wale aliokusudia (Conclusion) hata kama hawaielewi mada.
Mathalani, katika hii mada hii hitimisho lake ni uonevu kwa waislam unaotokana na mfumokristo uliowekwa na Nyerere unaowadhalilisha viongozi wa dini kwa kutumia vyombo vya dola vinavyoongozwa na mfumo unaopinga na kupiga vita uislam. Hitimisho kama hilo litamtia hasira asiyebahatika kuelewa maandiko ya MS hili likiwemo.
Wanasaikolojia wanasema njia rahisi sana ya kumshinda mpinzani wako ni kwanza kumfanya dhalili (inferior).
Kwa bahati mbaya MS yeye ndiye anawafanya watu wake inferior na wala si mwingine.
Amefanya Waislam wa Tanzania wajione dhalili(inferior) hata kwa yale wanayoweza.
Udhalili ni kuwafanya wawe wanalalamika, wanadai hata kilicho ndani ya uwezo wao, kuwafanya wajione ni watu duni na wanaohitaji upendeleo maalumu na hata kuwadhalilisha kwa maamuzi yao(hili la mwisho nitalifafanua)
MS amefanya watu wafikiri kuwa ili ufanikiwe ni lazima uwe na waziri mwislam, katibu mkuu mwislam au mkurugenzi mwislam. Unaposhindwa kufanikiwa basi tatizo lako ni dini yako na wala si jitihada zako.
Huku ni kuwapoteza watu na kuwafanya wasijitambue. Matokeo yake ni yale ya wazee wa Bagamoyo kama alivyosema Rais Kikwete.
Wazee wa Bagamoyo walimuomba awasaidie vijana wao kupata kazi na hili wala si kosa ni privilege yao.
Tatizo ni pale Rais alipowaambia walete vyeti, na kwa mshangao watarajiwa wakampelekea vyeti vya udereva!!
Rais akawauliza hivi hili kweli linahitaji msaada! kwamba vijana waliokosa kazi ndio hawa na Rais awatafutie udereva! Hawa ndio wanaolalamika mfumo mbaya! Hawajaliona tatizo kwasababu wana hitimisho- uonevu
Kuna kijana mmoja alikuja Dar es Salaam, baada ya kumaliza shule akapania kuwa mtu wa kompyuta.
Masikini hakujua kutumia key board zaidi ya kubofya herufi. Nia yake ilimpelekea asaidiwe kujiunga na chuo cha Diploma (NIIT). Akamaliza diploma na kujiunga na program ya degree inayotolewa kwa ushirikiano na chuo cha UK.
Kwa nia iliyothabiti akahitimu utaalam na maisha yake leo hii yamebadilika (180 Degree)
Anatafutwa kwa kazi hatafuti kazi, amevuka vizingiti vyote kwasababu ana silaha inayoitwa elimu.
Huyu hakutegemea waziri, mkuu wa baraza la mitihani, wala katibu mkuu mwenye jina la Mohamed, Hussein au William
Tatizo la MS ni kuwapa watu conclusion ili waifanyie kazi. Matokeo ya hayo ni watu kudhani kuwa dunia ya leo bila jitihada unaweza kufanikiwa tu uwe mkristo au mwislam. Kuwaaminisha watu kuwa mtu anayeitwa Juma Abdul katibu wa baraza la mitihani ndiye chachu ya mafanikio ni kuwadanganya.
Wataalam wa Engineering wana misemo yao (nisahihishwe kama nimekosea) ya kupata majibu ya tatizo.
Wanasema ili uweze kupata chanzo cha tatizo ni vema ukajiuliza neno kwanini (why) si chini ya mara tano.
Nitoe mfano;
1. Kwanini (why) kilwa ina umasikini mwingi, jibu ni kuwa hawana silaha ya kupambana na mazingira(elimu)
2. Kwanini (why) hawana elimu, jibu ni kuwa hawakufanya mitihani ya kuwasadia kwenda mbele
3.Kwanini (Why) hawakufanya mitihani, jibu ni kuwa hawakujiandikisha
4. Kwanini (why) hawakujiandikisha, jibu ni kuwa shule ilifungwa
5. kwanini(why) shule ilifungwa, jibu ni kuwa wanafunzi walitoroka wote
6. Kwanini (why) walitoroka, jibu hawana msukumo wa elimu
7. Kwanini (why) hawana msukumo wa elimu, jibu wazazi hawana hamasa
Hadi hapo tatizo la Kilwa si umasikini, tatizo ni wazazi kutokuwa na msukumo wa elimu.
Badala ya kuwaambia Wakilwa kuwa ni masikini eti kwasababu waziri wa elimu tangu uhuru ni mmoja na katibu wa baraza hajawahi kutokea kuwa mwislam, Wakilwa wanapaswa kuelezwa chanzo cha tatizo lao la kukosa hamasa.
Ukishajua tu tatizo basi una ufumbuzi wa tatizo. MS anachowambia watu wa Kilwa ni kuwa uwepo wa waziri mwislam ndiyo suluhisho la matatizo yao na wala si kujenga shule, vyuo vya ufundi na kuwasukuma watoto kama yule niliyemtolea mfano hapo juu wa kompyuta.
Ukirejea hapo juu nimesema MS anawadhalilisha waislam. Anaposema bunge limefanya maamuzi kwa shinikizo la wakristo, anatachotaka kueleza ni hitimisho (conclusion) kwa wasomaji na wasikilizaji. Asichowaambia ni kuwa wabunge hawateuliwi bali wanachaguliwa. Wanachaguliwa kwa hoja zao na wananchi wanaoamini watawawakilisha bila kujali dini zao au makabila.
Asichowaambia Watu ni kuwa chama cha CUF hakikuwa na mbunge wa kuchaguliwa hata mmoja licha ya kujinasibisha na dini. Watanzania wote wanajua kwanini wanachagua kiongozi. Anaposema bunge la wakristo anawadhalilisha waislam waliotumia haki yao kumchagua wanayemtaka. Anachotaka kusema hapa ni kuwa mfumo kristo ndio unawafanya wasiwepo wabunge wengi waislam. Hakika sipendi mada za udini lakini ni vema tuelezane ukweli.
MS tafuta (why) zisizopungua 5 utapata jibu na wala jibu si kumshambulia Nyerere au imani yake! Nitty gritty.
Eleza ukweli,chanzo na sababu na si hitimisho.
Huhitaji kuwa na wakuu wa elimu wa mikoa, unahitaji vijana wliofuzu kada mabali mbali na hao wataijengea jamii yao uwezo wa kuwa na wabunge na mawaziri.
Unahitaji watu wa kupambana na dunia hii ya ushindani na si viti maalumu au nafasi za upendeoe.
Unahitaji technicians 100 na si katibu mkuu mmoja.Haya hayapatikani hadi utakapoeleza ukweli.
Wazungu wana msemo wao ya kuwa
''If you have a problem and you can't solve you're the problem to begin with''