Bazee,
Sikufanikiwa kuona mahali/pahali? ambapo mbunge (kwa kumbukumbu zangu nilidhani Mhe Ibrahim Marwa (as he then was)) alitoa madai/tuhuma/shutuma za ukabila katika asasi zilizo Wizara ya Fedha. Hata hivyo, bado naamini kuwa suala la "madai" ya ukabila lishazungumzwa bungeni, si mara moja, si mara mbili.
Kwa mfano Mhe Lucas Selelii amewahi kuzungumzia kuendelea kutokuwepo kwa uwiano wa maendeleo, na huenda upendeleo wa dhahiri, kwa baadhi ya maeneo nchini, kunakofanywa na serikali kupitia bajeti yake na mipango ya maendeleo. Wakati huo huo, Mhe Selelii alionesha kukerwa kwake na wale ambao hutuhumu wale wanaoonesha shaka hii kuwa "wakabila"!
Nimeona sehemu kama mbili hivi (angalia pia sehemu zinazohusu mikataba ya madini, wanasheria "wetu", hoja ambazo hujadiliwa humu mara kwa mara):
"...Mheshimiwa Spika, lakini Nishati na Madini katika mambo ambayo ni mabaya, ni wenye Mikataba hii ya wachimbaji wakubwa wakubwa. Ni mabaya kupindukia. Nadhani kama ni dhambi kubwa ndiyo kwenye dhambi, mimi nawalaumu sana na kwa kweli nawalaumu Wanasheria wetu wa nchi hii. Kwa kweli nitaendelea kuwalaumu Wanasheria wetu wa nchi hii kwa sababu wanatuingiza kwenye Mikataba ambayo haina maslahi ya Taifa na tunapokuja kusimama kusema, wanaanza kusema tunazungumza mambo ya kisiasa. Sisi tumeanza kulalamikia Mikataba hii ya Madini mwaka 1998, Mheshimiwa Kahumbi yupo hapa ni shahidi.
Serikali ilikuwa inasimama inasema kwamba ninyi mnaleta ukabila, nyinyi mnaleta ukanda, nyinyi sijui mnaleta kitu gani, lakini mbona Mheshimiwa Rais Kikwete sasa hivi anazungumza hamumwambii? Ndiyo! Ilikuwa haki yetu! Mimi wa kwanza kuwalaumu Wanasheria. Kwa kweli ifikie mahali tuwawajibishe kwa jinsi ambavyo wanalipeleka Taifa letu kubaya. Sasa hivi tuanze kurudia Mikataba hii, lakini nchi hii imeporwa raslimali yake yote bila manufaa kwa wananchi wetu. Sisi tunaotoka kwenye maeneo ya madini tunaelewa. Sisi tunaotoka maeneo yenye wachimbaji wakubwa tunaelewa..." (17 Julai 2006).
Link:
http://www.parliament.go.tz/bunge/ContrLst.asp?Menu=Contr&PTerm=2005-2010&vpkey=1226&page=4
Na nyingine:
"..
.Mheshimiwa Spika, napenda tu kutahadharisha kwamba, mimi natoka Kanda ya Magharibi na katika hilo, sioni aibu wala sisiti kutetea Kanda ya Magharibi, hasa kwa upande huu wa miundombinu.
"...Mheshimiwa Spika, barabara zilizopo kwa kweli hapa uzalendo umenishinda, chukua barabara ya kutoka Manyovu kwenda Mwandinga, kule kwa ndugu zetu wa Kigoma, imepangiwa kwenye vitabu vya fedha shilingi bilioni mbili. Ukichukua barabara ya kutoka Ipole kwenda Mpanda, imepangiwa shilingi milioni 600, ukichukua barabara ya kutoka Nzega kwenda Tabora, imepangiwa shilingi milioni 500, ukichukua barabara ya kutoka Sumbawanga kwenda Nyakanazi shilingi milioni 500. Kuna barabara moja, juzi jamaa zangu wale wa Mwanza walilalamika sana mpaka wakawa wanaandika kwenye magazeti, tumewapangia fedha, hazimo humu kwenye kitabu cha hotuba, hakuna na hata kwenye kitabu cha fedha, ile barabara ya Usagara kama sijasokea sana, hakuna.
Mheshimiwa Spika, lakini iko barabara ya kutoka Marangu - Tarekea imepangiwa shilingi bilioni 17. Jamani hivi nchi hii hii moja, barabara moja tu, tena barabara ile ni kama vile kutoka Urambo unakwenda Kaliua, inapangiwa shilingi bilioni 17. Barabara nyingine shilingi milioni 500, nyingine shilingi milioni 300 na nyingine zero; maana yake nini? Hapo ndipo nimenichanganyiwa, kweli uzalendo umeshinda.
Mheshimiwa Spika, ningeiomba Wizara hebu tutende haki, tunaelewa kabisa vipaumbele mnavyo vingi, tunaelewa kabisa sungura ni huyo huyo mdogo, hilo tunalijua, lakini tutende haki twende angalau kikanda. Unapozungumzia Kanda utataja Magharibi, unapozungumzia Kanda utataja Kanda ya Ziwa, unapozungumzia Kanda utataja Kanda ya Kusini ya wakulima wa korosho, ndiyo kanda hizo. Lakini unapozungumzia kutoka Tarekea kwenda Marangu, hivi jamani hiyo ndiyo haki?..." (3Julai 2006)
Link:
http://www.parliament.go.tz/bunge/ContrLst.asp?Menu=Contr&PTerm=2005-2010&vpkey=1226&page=10
Hapo alikuwa "akipambana" na Mramba (wakati huo akiwa Waziri wa Mindombinu) kuhusu kutenga fedha nyingi kwenye barabara hiyo ya "kaskazini".