Barua fupi kwa watanzania wote:
Ndugu zangu watanzania, SIASA ni maisha, na tunapozungumzia maisha hakuna ushabiki. Siasa inamhusu kila mtanzania, mwana CCM, CHADEMA, CUF NA WAFUASI wa vyama vyote ikiwa pamoja na watanzania wengi ambao hawana vyama kwa vile sote tunahitaji kuishi..
Linapotokea janga kama hili walioathirika ni wana CCM , CHADEMA CUF, ACT + vyama vingine na wale wasiokuwa na vyama. Hivyo yanapokuja maswala makubwa yanayohusu MAISHA yetu tuache kabisa ushabiki kwa vile tu wewe ni CCM, tujadili hoja, tuunge mkono hoja, na hoja ile inayolenga kuboresha maisha yetu bila kuangalia nani kaitoa.
Napenda kuwafahamisha watanzania kuwa sasa hivi kuna nidhamu ya uoga, na hii itatugharimu sio pesa tu bali hata maisha yetu. Nasema hivi kwa sababu wapo walioyajua matatizo ya uendeshaji wa Meli hiyo, tena miongoni mwao ni wataalamu wakubwa tu na wapo katika uongozi. Ila ukikosoa utatumbuliwa, hivyo upepo uliopo sasa hivi ni kusifia tu, wewe ndio mzuri na hata ukuu wa wilaya utapewa. Sasa hii sio siasa, kwa vile hayo si maisha. Maisha ni kusifia pazuri na kukosoa pabaya ili parekebishwe.
Ni nani alikuwa hajui kuwa hii meli inachukuwa abiria mara 4 au zaidi kuliko uwezo wake? Ni nani alikuwa hajui madhara yaliyotarajia kutokea huko mbeleni? Unahitaji uchawi kujua hili. Mabasi yanaposimamisha tu , trafiki hamuachii dereva mpaka atoze faini. Hivi abiria wa kwenye mabasi wanathamani zaidi kuliko wa Melini? Kuna aliyelisema hilo.
Kama hatukuweza kuyasema hayo, tujue uoga ni thambi itayotutafuna. Kwa vile uoga umetawala makazini na kwa watendaji wakuu tutegemee vifo kama vilivyotokea huko mwanza vitajirudia katika sekta nyingi tu za serikali. Tumewabana waendeshaji binafsi kwa sheria zote na kuziacha huru sekta za serikali ili tu serikali ya CCM ionekane inaendeshwa vizuri. Hapa ndio kwenye uchawi, sumu na ushetani mkubwa. Mungu ibariki Tanzania.