Ni rahisi kusema ni mapenzi ya Mungu lakini, binafsi hiyo itakuwa ni sababu ya kijinga. Vyombo vya usafiri vimetengenezwa kitaalamu. Vinatakiwa kuendeshwa kitaalamu kwa kufuata utaratibu au sheria zilizojalibiwa na kuonyesha mafanikio. Wanaoviendesha ni watu waliofunzwa na kusomea taratibu za kuviendesha. Ndivyo ilivyo kwa Ndege, magari pamoja na meli kama hii MV Nyerere iliyozama.
Tatizo liko wapi hadi tuwe na ajali za aina hii? Tujiulize kwa nguvu sana kwa ajali kama hii ya meli ambayo siyo mara ya kwanza. Ilikuwa hivyo na MV Butiama, MV Kipepeo, MV spice sasa ni MV Nyerere! Napenda niseme haya yote yanatokana na ujinga wa waliosomea kuendesha vyombo hivyo. Kila wakati sababu inayotolewa ni kuzidisha uwezo wa vyombo hivyo. Sisi ni watu wa aina gani tusiweza kujifunza kutokana na makosa ya nyuma? manahodha hawa ni wajinga kiasi gani kuliko wanayama wa kufugwa wanaoweza kujifunza kutokana na matendo?
Ni aibu kuona mtu amesoma na kuelewa idadi ya abiria pamoja na uzito wa mizigo unaostahili kubebwa na vyombo hivyo. Nahodha anafahamu zana za uokoaji zilizoandaliwa kutokana na idadi ya abiria wanaobebwa na vyombo hivyo. Nahodha anafahamu uwezo na madaraka aliyonayo kuzuia abiria walio nje ya uwezo wa chombo chake. Sasa tuseme wazi kwamba watu hawa wanasomea unahodha lakini, wana viendesha kwa ujinga wao. Yaonekana wanashindwa kufuata mafunzo yao badala yake wanaongeza vipaji vyao vya kijinga na kuleta ajali kama hizi. Hii ni kwa wote. Hata magari yanaendeshwa kwa ujinga huo na wakati mwingine kujaribu kuonyesha kwamba watengenezaji hawakuelewa uwezo wa vyombo. Ukiwaangalia wakiwa kwenye kazi zao hizi, wanaonyesha umwamba wa kijinga na ufahamu wa kijinga, na mikogo ya kijinga kabisa kiasi kwamba wangeelimika, tusingekuwa na ajali kama hizi zambazo wakati mwingine, tunalazimisha kutoa majibu ya kiroho, eti ni mapenzi ya Mungu. Ajali hizi hazitokani na mambo ya kiroho!