Kulingana na ripoti ya BoT ya robo ya mwisho ya 2024, mzunguko wa fedha Tanzania unaonyesha ukuaji wa kushangaza, lakini pia unaonesha mapungufu ya kiuchumi yanayohitaji uchunguzi wa kina. Pesa taslimu iliyo nje ya mifumo ya benki zimepanda kutoka Trilioni 4.5 mwaka 2020 hadi Trilioni 7.3 mwaka 2024, ongezeko la 62.2%, huku amana za wateja benki zikiongezeka kutoka Trilioni 23 hadi Trilioni 40, sawa na 73.9%. Hali hii inaweza kuonekana kama ishara ya ukuaji wa kiuchumi na kufanikiwa kwa sera jumuishi za kifedha, lakini ukiitazama vizuri, inaweza kumaanisha kuna pengo kubwa na hatari kwa uchumi.
Kwanza, suala la utitili wa noti za Shilingi 10,000, ambazo zinachukua 85.8% ya pesa zote taslimu, ni wa kushtua na unauibua maswali mengi juu ya afya ya uchumi wetu. Ongezeko hili linaweza kuwa dalili ya mfumuko wa bei (inflation), licha ya kuwa takwimu zinaonesha kuwa mfumuko wa bei bado ni 3.1 kufikia Januari 2025 , ambao umefanya noti za thamani ya chini kama Shilingi 5,000 zipungue thamani yao kwa 15.7% tangu 2020. Hii ni onyo la kina kwamba gharama za maisha zinaongezeka kwa kasi, na serikali na Benki Kuu zinashindwa kuleta uwiano wa bei thabiti. Zaidi ya hayo, utegemezi wa pesa taslimu nje ya benki unapunguza uwezo wa Benki Kuu kudhibiti fedha katika uchumi, jambo linaloweza kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi ikiwa hali hii haiwastukiki.
Pili, sehemu ndogo ya sarafu (2% tu ya mzunguko) na ongezeko lao la 20% hadi Bilioni 163 inaonyesha upungufu wa mkakati katika kusambaza fedha za mzunguko. Ingawa sarafu za Shilingi 500 zinachukua 36.8% ya sarafu zote, ni 0.7% tu ya fedha taslimu zote, hali inayodokeza kuwa miamala ya kila siku inategemea noti za thamani kubwa zaidi kuliko inavyofaa. Hii ni hitimisho la kushangaza kwamba miundombinu ya kidijitali bado haijafikia ngazi ya kutosha kuondoa utegemezi wa pesa taslimu, jambo linaloweza kuwa ni kosa la upungufu wa mipango ya serikali.
Hatimaye, ongezeko la 238% la thamani ya noti kwenye mzunguko (kutoka Bilioni 199 hadi 674) ni ishara ya hatari kubwa. Hili linaweza kuashiria kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi zisizo rasmi au hata utapeli wa fedha, hali ambayo inahitaji uchunguzi wa mara moja. Aidha, kuongezeka kwa amana za benki ni pengine tu sura ya nje ya mafanikio; bila mikakati ya kudumu ya kuimarisha miamala ya kidijitali na kupunguza pesa taslimu, uchumi unaweza kukwama katika mzunguko wa hatari wa inflation na ukosefu wa udhibiti.
Ukuaji wa mzunguko wa fedha ni wa kuvutia, lakini unatiashaka kama unaamaanisha ukuaji au mfumuko wa bei. Serikali na Benki Kuu zinapaswa kuchukua hatua za haraka kuboresha miundombinu ya kifedha na kuzuia utegemezi wa pesa taslimu ili kuepuka hatari za kiuchumi zinazokithiri. Bila hili, ukuaji huu unaweza kuwa ni mwanzo wa tatizo katika mfumo wetu wa kifedha badala ya mafanikio.