Wanaukumbi mjadala umekuwa mkali sana. Ghadhabu zinapanda ni wajibu wetu kuzipoza. Naweka hapa chini siku za mwanzo za TANU ilipokuwa inajaribu sasa kuvuka mipaka yake kutoka Dar es Salaam pale New Street na kwenda katika majimbo. Katika majimbo ya mwanzo kwa TANU kwenda ilikuwa Jimbo la Kusini. Soma kwa furaha:
Jimbo la Kusini, 1955
TAA mjini Lindi ilikuwa chini ya uongozi wa Suleiman Masudi Mnonji aliyekuwa Rais na Katibu wake alikuwa Mohamed Waziri. Mnonji alikuwa fundi cherahani na Waziri alikuwa mchoraji wa ramani za nyumba. TAA ilichelewa kuanza mjini Lindi. TAA ilianzishwa Lindi mwaka 1953 wakati uongozi wa TAA mjini Dar es Salaam si tu ulikuwa unaigeuza TAA kuwa chama cha siasa bali ulikuwa ukifanya mipango kumpeleka mjumbe wake Umoja wa Mataifa kudai uhuru. Masudi Mnonji alikuwa na uzoefu wa kutosha katika siasa. Baada ya Vita Kuu ya Pili alikuwa amejaribu kuanzisha vyama vya wafanyakazi katika mashamba mbalimbali ya mkonge kusini mwa Tanganyika. Vilevile aliwakusanya wapishi na madobi mjini Lindi waanzishe umoja wao. Ilikuwa kupitia juhudi zake binafsi TAA ijapokuwa ilichelewa, ilikuja kuanzishwa mjini Lindi na Mnonji alijitolea nyumba yake katika mtaa wa Makonde kama ofisi ya chama. Mnonji kwa kutambua umuhimu wa kuwa na uongozi ulioelimika vizuri, alimleta Nangwanda Sijaona kutoka Nachingwea aje aishauri TAA jinsi ya kufanya mambo kwa utaalamu.
Wakati huo mjini Lindi kulikuwa na chama cha wafanyakazi bandarini Dockworkersí Union chini ya uongozi wa Mussa Athumani Lukundu, chama ambacho kwa kiasi chake kilianzisha vuguvugu la siasa za vyama vya wafanyakazi. Ingawa vyama hivi viwili, yaani TAA na Dockworkersí Union vilikuwepo katika mji mmoja, siasa za hiki chama cha pili cha wafanyakazi bandarini hazikupitia TAA kama ilivyokuwa mjini Dar es Salaam. Hii kidogo ilidhoofisha mwamamko wa siasa kwa wananchi. Jimbo la Kusini lilikuwa katika usingizi mzito wakati sehemu nyingine Tanganyika zilikuwa zikipiga hatua kwenda mbele zikiandaa vita dhidi ya utawala wa kikoloni. Chanzo cha usingizi huu mzito huko kusini ulikuwa na asili yake katika historia ya Tanganyika.
Vita vya Maji Maji vilipoanza kusini ya Tanganyika mwaka 1905 kwa nia ya kuwafukuza Wajerumani kutoka Tanganyika, zile sehemu zenye Wakristo wengi zilikataa kujiunga na vita na badala yake wakajiunga na majeshi ya Wajerumani na kupigana bega kwa bega na dhidi ya wazalendo. Hii ilitokana na sababu ya kuwa uasi dhidi ya dhulma wa Wajerumani ulianza katika maeneo yenye Waislam wengi na vita vikachukua sura ya vita vya Kiislamu dhidi ya Wazungu ambao dini yao ni Ukristo. Kwa kuwa wamishonari walikuwa washirika wa wakoloni, walichukuliwa kama maadui na hivyo ikawa vituo vyao vinashambuliwa na wapiganaji wa Maji Maji. Kutokana mashambulizi haya, Wakristo walivichukua Vita Vya Maji Maji kama vita dhidi ya Ukristo. Harakati za Maji Maji zilishindwa na Wajerumani walifanya fisadi kubwa dhidi ya wananchi na viongozi wao. Jambo hili liliacha kovu kubwa katika fikra za wananchi na kwa upande wa Wakristo ambao walinusurika na ghadhabu ya Wajerumani, wengi wao wakajiweka mbali na aina yoyote ya kupinga ukoloni.
Kufuatia historia hii Waafrika waliokuwa kusini ya Tanganyika sasa wakiwa chini ya utawala wa Waingereza na kuwa chini ya himaya ya wamishonari walipumbazwa kiasi kwamba waliogopa siasa. Baada ya Waafrika kushindwa vita kwa silaha kali za Wazungu sasa Kanisa likaona ndani ya fadhaa ile fursa yao kutawala sehemu hiyo kwa kutoa vishawishi kama vile shule na hospitali. Kwa hiyo Wamishionari na Waingereza walionekana kama mabwana wema wenye kuwajali raia zao kinyume na serikali katili na ya kidhalimu ya Wajerumani. Vuguvugu la siasa kama ilivyokuwa Vita vya Maji Maji, lilianza katika maeneo ya Waislam kufuatia mfumo ule ule kama ilivyokuwa katika upinzani wa ukoloni wa Wajerumani. Wakristo katika Jimbo la Kusini waliiona TANU kama walivyoviona Vita Vya Maji Maji, kama harakati nyingine za Waislam zilizowa zinakuja tena kwa mara ya pili kuvuruga amani na utulivu. TANU ilipoanza ikawa inavuma kuwa safari hii Waislam walikuwa wamemua kuanzisha vita dhidi ya Waingereza kama walivyoanzisha vita na Wajerumani.
TANU ilipoanzishwa mjini Dar es Salaam na hisia za utaifa zilipokuwa zikipanda pole pole katika fikra za wananchi katika sehemu nyingi za Tanganyika, Jimbo la Kusini lilikuwa bado usingizini likiishi katika zama za kale. Mnonji na Waziri, kwa sababu ya utu uzima wao, daraja yao katika jamii na hasa kutokana na kuhusika kwao katika siasa za pale mjini, walikuwa na nguvu kubwa katika TAA. Wakati TANU imeshachukua nafasi ya TAA, uongozi wa TAA Lindi haukutaka kufungua tawi la TANU. Mtu wa kwanza kuutanabaisha uongozi wa TAA mjini Lindi juu ya mageuzi yaliyokuwa yakitokea Tanganyika na kuanzishwa kwa chama kipya cha siasa mjini Dar es Salaam alikuwa Abdallah Juma Makopa, kijana kutoka Tanga akifanya kazi ya ukarani Posta ya Lindi. Makopa aliwaendea Mnonji na Waziri na kuwajulisha kuhusu kuanzishwa kwa TANUmjini Dar es Salaam na aliwashauri waanzishe TANU pale Lindi. Jambo hilo lilipingwa moja kwa moja na Mnonji, Waziri, Said Nassoro, Abdallah Mhuji na wanachama wengine wa TAA.
Chama cha Waafrika ambacho kilianzishwa siku nyingi mjini Lindi na kwa hakika ndicho kilikuwa chama cha pekee kushughulikia maslahi ya Waafrika sehemu za kusini kilikuwa African Welfrare Association ambacho mlezi wake alikuwa John Nevi, Mjaluo kutoka Kenya na katibu wake alikuwa Casian Njunde, Mngoni wa Songea. Makopa aliposhindwa kukishawishi kile kikundi cha wazee wa TAA aliwaendea Yusufu Chembera na Rashid Salum Mpunga. Chembera alikuwa na umri wa miaka thelathini na nne na Mpunga alikuwa kijana wa miaka ishirini na saba. Chambera alikuwa amesoma hadi shule ya msingi na Mpunga alikuwa amemaliza madras. Chembera alikuwa akifanya kazi katika kantini ya Lindi Welfare Centre, wakati Mpunga alikuwa dereva wa lori aliyeajiriwa na mfanyabishara wa Kihindi. Makopa aliwashauri Chembera na Mpunga juu ya uwezekano wa kuwahamasisha wananchi wawaunge mkono ili tawi la TANU lifunguliwe pale mjini. Aliwaambia alitaka sana kufanya hivyo yeye mwenyewe lakini asingeweza kwa sababu yeye alikuwa mtumishi wa serikali na hakuwa akifahamika sana mjini. Uongozi kama wao ndiyo ungeweza kuaminiwa na wananchi na usingetiliwa mashaka. Makopa, Chembera na Mpunga walikubaliana kuwa kabla ya kuanza kufanya kampeni waziwazi kwa ajili ya TANU, lazima wawaandikishe wanachama wachache kama waasisi wa chama. Mpunga na Chembera walimwandikisha kijana mmoja akiitwa Abdallah Faraj na katika muda mfupi waliweza kuwapata takriban wanachama kumi na tano walioridhia kujiandikisha kama wanachama waasisi wa TANU.
Baada ya kuandikisha wanachama waasisi mkutano wa siri uliitishwa katika Welfare Centre ambako ndiko alikokuwa akifanya kazi Chembera. Chembera aliwaeleza kwa ufupi wale wanachama wa mwanzo kuhusu malengo na madhumuni ya chama hicho kipya cha siasa. Mkutano huo ulichagua kamati ya watu watatu yaani, Makopa, Chembera na Faraj ili kuwakabili Mnonji na Waziri kuwaleza kuwa TAA haipo tena nchini Tanganyika. Lengo lilikuwa kuwasadikishia kuwa ilikuwa kazi bure na kupoteza wakati kujaribu kuihuisha TAA mjini Lindi wakati ambapo Tanganyika nzima ilikuwa ikisonga mbele na TANU. Baada ya mjadala mrefu sana na mkali wa wale vijana watatu na ule uongozi wa TAA wa wazee, walikubaliana TANU lazima isajiliwe mjini Lindi.
Uchaguzi ulifanyika na Shaaban Msangi, kijana wa Kipare akifanya kazi kwa Smith Mc Kenzie, alichaguliwa rais na Ahmed Seif, katibu. Mpunga, Chembera, Mnonji na Idd Toto walichaguliwa wajumbe wa kamati. Ahmed Seif alikuwa kijana ambaye ndiyo kwanza amemaliza shule, yeye alikabidhiwa kuendesha ofisi kwa niaba ya uongozi. TANU mjini Lindi ilimwajiri ili kukiandaa chama kiweza kufanya kazi zake kwa ufanisi. Hassan Mohamed Kinyozi aliajiriwa kama mhudumu wa ofisi. Hawa wawili walikuwa ndiyo wafanyakazi wa kwanza wa TANU waliokuwa wakilipwa mshahara katika Jimbo la Kusini na wakawa miongoni mwa wafanyakazi wachache sana walioajiriwa na TANU kwa wakati ule. Mnonji alitoa nyumba yake katika mtaa wa Makonde kuwa ofisi ya kwanza ya TANU Jimbo la Kusini. Baada tu ya kuanzishwa kwa TANU, Athumani Mussa Lukundu, kiongozi wa Lindi Dockworkersí Union, aliunganisha chama chake na TANU. Jambo hili, kwa TANU lilikuwa la kuitia moyo sana kwa sababu Dockworkersí Union ilikuwa na wananchama wengi na hatua ile iliongezea TANU nguvu.
Baada ya muda mfupi tu toka kufunguliwa kwa TANU Mkutano Mkuu wa Kwanza wa TANU wa mwaka 1955 ulifuatia. Tawi la Lindi lilikuwa tayari lina uhusiano na makao makuu ya TANU mjini Dar es Salaam, na lilikuwa likitarajia kuhudhuria mkutano huo na kukutana na Julius Nyerere na uongozi mzima wa TANU pale makao makuu Dar es Salaam. Mpunga, mwanachama muasisi wa TANU, na Ali Ibrahim Mnjale waliteuliwa kuhudhuria mkutano huo kama wajumbe kutoka Jimbo la Kusini. Halmashauri ya TANU ya Lindi iliwaelekeza wajumbe hawa wafikishe ombi rasmi kwa makao makuu ili Julius Nyerere aje kufanya ziara kusini kwanza, kukutana na wananchi na kufanya kampeni kwa ajili ya TANU na pili aje kupambana na propaganda dhidi ya TANU zilizokuwa zikitawanywa na Yustino Mponda. Mponda akitumia uhusiano wake na serikali ya kikoloni na nafasi yake kama mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria kutoka Newala; na vilevile akitumia ushirikiano wake wa muda mrefu na kanisa ambao bila shaka yoyote lilikuwa serikali ndani ya serikali kule kusini, alikuwa ameanza kampeni yake ya kuipinga TANU. Hili lilikuwa likiathiri msukumo wa uanachama. Mponda alikuwa mmoja wa wajumbe waliotumwa na Gavana Twining kwenda Umoja wa Mataifa Februari, 1955 kwa niaba ya serikali ya kikoloni kwenda kuipinga. Uongozi wa TANU huko Lindi ulitaka Nyerere aende kupambana na Mponda akiwa katika uwanja wake mwenyewe, ndani kabisa ya ngome ya Ukristo wa Kikatoliki katika Tanganyika.
Mkutano mkuu wa mwaka wa TANU ulifanyika katika ukumbi wa Hindu Mandal mjini Dar es Salaam. Siku kabla ya mkutano TANU ilimwalika Gavana Edward Twining kwenye tafrija katika Ukumbi wa Arnatouglo lakini alikataa kistaarabu na akamtuma Chief Secretary, Bruce Hutt, kumwakilisha. Baada ya mkutano, wakati wajumbe wengine wanaondoka kurudi kwenye majimbo yao, Mpunga na Mnjawale walibakia nyuma kukutana na uongozi wa makao makuu wa Julius Nyerere, Sheikh Suleiman Takadir, John Rupia, Ali Mwinyi Tambwe, Said Chamwenyewe, Oscar Kambona na wengineo. Mpunga na Mnjawale waliwafahamisha viongozi wa makao makuu kuhusu hali mbaya ya siasa Jimbo la Kusini. Mbali na kampeni za kuipinga TANU za Mponda, katika ziara yake Lindi Gavana Twining aliwatahadharisha Waafriika wa Tanganyika wasijihusishe na wafaanya fujo wanaotaka kuzusha vuruguí. Twining alikuwa akitoa onyo hili akiikusudia TANU ambayo ilikuwa imeanzishwa mwaka uliopita. Hotuba hii ya Gavana iliwatisha wananchi kujiunga na TANU. Mpunga na Mnjawale walisisitiza kuwa kuja kwa Nyerere mjini Lindi kulitakiwa haraka sana kukabiliana na vyote viwili, kwanza ile hotuba ya gavana na pili zile kampeni za kupinga TANU zilizokuwa zikiendeshwa na Liwali Yustino Mponda.
Wakati huo Abeid Amani Karume aliyehudhuria ule mkutano alimwalika Nyerere afanye ziara Zanzibar. Kitu cha kustaajabbisha ni kuwa, Nyerere alionekana kuiafiki zaidi ziara ya Zanzibar kuliko ile safari ya kwenda kusini kuiimarisha TANU. Mpunga alimsisitizia Nyerere umuhimu wa yeye kwenda Lindi ambako kunaweza kuwa ndiyo chanzo cha TANU kupata ufanisi Newala, Songea, Tunduru na Masasi ambako kulikuwa na upinzani mkubwa dhidi ya TANU. Kanisa lilikuwa likiwazuia Wakristo kujiunga na TANU. Sheikh Suleiman Takadir, Said Chamwenye, John Rupia, Ali Mwinyi Tambwe wote waliunga mkono ule ujumbe wa Lindi juu ya suala hili. Baada ya kufikia makubaliano, Mpunga na Mnjawale walipewa barua ya kuthibitisha safari ya Nyerere. Ziara ya Nyerere ilikuwa ianze muda mfupi kutokea hapo kwa kuwa ilikuwa ndiyo siku za mwisho za kiangazi. Barabara sehemu ya kusini ya Tanganyika zilikuwa hazipitiki wakati wa masika, zikiitenga kabisa kusini toka sehemu zilizobaki za nchi. Ali Mwinyi Tambwe na Rajab Diwani walifuatana na Nyerere kwenda Jimbo la Kusini kuondoa wasiwasi na woga uliozushwa na Gavana Twining na kibaraka Yustino Mponda.
Nyerere na msafara wake ulipokelewa na uongozi wa TANU wa Lindi huko Mbanji, kijiji kidogo nje ya mji. Msafara wa Nyerere ulipowasili Mbanji ilikuwa kiasi cha saa moja jioni hivi na giza lilikuwa linaanza kutanda. Mbali na Mpunga na wale wajumbe wawili waliokutana na Nyerere mjini Dar es Salaam mwezi uliopita, hakuna hata mtu kati ya umma ule uliokuja kupokea ujumbe kutoka makao makuu ya TANU aliyekuwa anajua Nyerere anafanana vipi. Mpunga, dereva wa lori, alijibagua kutoka kwa lile kundi la watu akawa amesimama pembeni ili Nyerere apate kumuona. Baada ya Nyerere kumtia Mpunga machoni, Mpunga alimwendea kumsalimu Nyerere, Tambwe na Diwani; kisha aliligeukia lile kundi la watu kumtambulisha Nyerere kwa wananchi akilitaja jina lake kwa sauti kubwa. Baada ya hapo aliutambulisha ule ujumbe wa Nyerere. Nyerere na ujumbe wake ulisindikizwa kwa shangwe na kundi la watu hadi ofisi ya TANU kwenye nyumba ya Mnonji. Kupakana na ofisi ya TANU ilikuwepo nyumba ya seremala mmoja, Issa bin Ali Naliwanda. Hii ndiyo nyumba iliyochaguliwa alale Nyerere na ujumbe wake, si kwa sababu ilikuwa nzuri kupita zote. Ilichaguliwa na kupewa heshima hii kwa sababu ilikuwa karibu sana na ofisi ya TANU na hivyo basi ilirahisishia TANU kazi ya ulinzi wa Nyerere. Siku iliyofuata ilikuwa Jumapili na Nyerere aliwaomba wenyeji wake apelekwe kanisani kwa ajili ya ibada.
Kanisa Katoliki mjini Lindi ni jengo la fahari lililoko ufukweni katika Bahari ya Hindi. Lindi ulikuwa mji wa Waislam. Mbali na mlio wa kengele za kanisa hakuna mtu pale mjini aliyekuwa akishughulishwa na kile kilichokuwa kikifanyika kwenye viwanja vya kanisa. Watu wachache waliokuwa wakienda kusali kanisani walikuwa Wakristo waliokuja Lindi kutoka sehemu nyingine za Tanganyika kufanya kazi katika ofisi za serikali. Ghafla mahala hapa palipokuwa pweke, palipopuuzwa kwa miaka na Waislam wa mjini, pakawa muhimu kwa sababu rais wa TANU ambae alikuwa Mkatoliki alikuwa na haja ya kuhudhuria ibada pale kanisani. Hakuna mtu katika uongozi wa TANU wa Lindi aliyejua ndani ya kanisa lile kulikuwa vipi wala hapakuwa na yoyote kati yao aliyewahi kuingia ndani ya kanisa, si Lindi wala mahali popote pale. Uongozi wa TANU wa Waislam mjini Lindi haukumwamini Mkristo yoyote kumsindikiza Nyerere kanisani ili kumpa ulinzi. Baada ya kujadili suala hilo kwa urefu hatimaye iliamuliwa kuwa Mpunga na wanachama wachache Waislam wenye kuaminika lazima wamsindikize Nyerere kanisani na wengine wabakie nje kulinda mlango.
Jumapili hiyo Nyerere aliingia ndani ya kanisa Katoliki mjini Lindi akifuatwa nyuma na walinzi wake Waislam wakiongozwa na Salum Mpunga, dereva wa lori shupavu. Misa hii ëmaalumí ilidumu katika fikra za wale Wakristo waliokuwepo pale kanisani kwa miaka mingi kwa kuwa tukio hilo liliwagusa sana Wakristo walioshuhudia mkasa ule ndani ya kanisa la Lindi. Hii huenda ilikuwa mara ya kwanza na ya mwisho kwa Nyerere kumsalia Mungu wake huku akiwa amesimamiwa na Waislam.
DC mkoloni alikataa kutoa kibali kwa TANU kufanya mkutano wa hadhara. Akiwa amekasirika sana, Shabaan Msangi aliitisha mkutano wa dharura wa tawi uliohudhuriwa na Nyerere na Tambwe. Baada ya mkutano huo Tambwe alikwenda kumwona DC. Ruhusa ilitolewa, na adhuhuri hiyo siku ya Jumapili, katika kiwanja ambacho Wazungu walikuwa wakicheza gofu, ambako mwaka mmoja uliopita Gavana Edward Francis Twining alitoa hotuba iliyowavunja moyo Waafrika, Nyerere alihutubia mkutano wa hadhara. Kamwe haijapata kutokea kabla ya siku ile katika historia nzima ya Jimbo la Kusini, watu wengi kiasi hicho kujumuika mahali pamoja. Wazungu na Wahindi pamoja na askari, watu wakiwa wamekaa na wengine wamesimama katika jua kali walikuja kumsikiliza Nyerere akihutubia. Ili kuhakikisha amani na usalama pale mkutanoni serikali iliweka askari waliouzunguka uwanja mzima wa mkutano. Nyerere aliwafikishia watu ule ujumbe wa TANU wa kuwa, kutawaliwa ni fedheha, na Waafrika wa Tanganyika lazima wadai uhuru wao. Uingereza ilikuwa ikiitawala Tanganyika chini ya udhamini kwa niaba ya Umoja wa Mataifa, na wakati ukiwa muafaka inabidi Uingereza ikabidhi nchi kwa wananchi wenyewe. TANU ilikuwa imewasili Jimbo la Kusini.