Mimi ni mkatoliki nisiyeunga mkono uwepo wa masanamu kanisani... Na ijumaa kuu huwa sijiangaishi kubusu msalaba. Sisali rozari kwakuwa naamini bikira Maria hawezi kusikia sala zangu...
Ntabakia mkatoliki kwa msimamo wangu.
Ijumaa Kuu hutumika kwa maadhimisho ya mambo mengi sana ambayo wakristo wanayafanya katika siku hii pamoja na kufunga na kubusu msalaba ila Ijumaa Kuu hii tutakaloliangalia ni kuhusu msalaba kitendo cha kuubusu ni kuuabudu au kuuheshimu.
Ili tuweze kuelewa vizuri lazima tujue ibada ni nini na kuna mambo gani yanahitajika katika ibada na kinachotusumbua wengi ni kushindwa kutofautisha kati ya kuheshimu na kuabudu.
Kwa maana hiyo maana ya Ibada ni utaratibu uliowekwa na kundi la watu kwa ajili ya kufanya sala na maombi kwa ajili ya kuabudu mbele ya yule anayeabudiwa na watu husika na huyo ndiye Mungu wa kweli mbele yao.
Utashangaa nikisema kuwa Mungu huyo anaweza kuwa jua, jiwe, mti au chochote kile kilichoandaliwa na watu husika jambo kubwa nikuhakikisha shida zao zinapokelewa na kufanyiwa kazi na kujibiwa kama walivyotarajia.
Kwa hiyo penye ibada pana mungu yaani kile kinachoabudiwa na ili ikamilike na kuitwa ibada kuna mambo saba yanahitajika navyo ni Kuheshimu, kutukuza, kuabudu, kutoa sadaka, kusujudu, kusifu na kushukuru.
Kubusu
Neno Kubusu lina maana nyingi tofauti kutokana na kila Taifa likiwa na tafsiri yake lakini kuabudu ni ishara au dalili ya upendo, Heshima na Furaha.
Biblia inatuambia kuwa hata wakristo wameagizwa wasalimiane kwa busu takatifu (2 Wakorintho 13:12) na tunaona viongozi mbalimbali wanapokutana wanakumbatiana na kubusiana kadhalika hata wazazi huwabusu watoto wao wachanga ili kuwafurahisha.
Kuabudu
Neno kuabudu maana yake kuwa mtu au watu wanakisujudia au kukitukuza kitu fulani na kupeleka shida zao na kwa madai kuwa watapona au kupata faraja kutoka pale wanapozipeleka shida zao kwa yule wanayemuabudu na kutegemea kuwa matatizo yao yataisha kupitia kwake.
Mfano kila mmoja duniani anamuabudu yule anayedhani ni Mungu na Mitume wake kutokana na imani za kila mtu kwa kupelekea shida zake kwa njia mbalimbali na kujua yeye pekee ndiye atakayemsaidia katika matatizo yake.
Kuheshimu
Heshima inayozungumzwa katika mada hii ni ile ya kujishusha na kumwinua Mungu. si heshima ya juu juu tu, bali ni heshima yaenye 'ADHAMA'. Ndani yake kuna adhimisho. Adhama maana yake ni ukuu na enzi. Tunapomwadhimisha Mungu, tunaweka juu yake heshima, ukuu, mamlaka na utukufu kuwa ni yeye tu anayestahili kuwa navyo. (1 Nyakati 16:27, Mithali 8:18).
Je Kubusu Msalaba ni Ibada ya sanamu?
Inaonesha kuwa Mungu ndiye aliyekataza ibada ya sanamu na wakati huo huo Mungu alimuagiza Musa atengeneze sanamu ya nyoka wa shaba kule jangwani.
"Bwana akamwambia Musa, jifanyie nyoka wa shaba ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi. Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti. (Hesabu 21: 4-9)
Baada ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo inawafanya wakristo kujua kuwa Yesu ndiye nyoka wao wa shaba. Na ukimtazama yesu juu ya mti wa msalaba, utapona majeraha yako yote uliyotiwa na shetani. Yeye anakualika akisema;
"Niangalie mimi mkaokolewe, enyi nchi zote za dunia, maana mimi ni Mungu, hapana mwingine." (Isaya 45:22).
Pia Mtume Paulo naye anawaambia wakolosai kuwa,
"Basi vivifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uuasharati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu." (Wakolosai 3:5).
Kumbe, matendo maovu ndiyo namna ya kisasa ya ibada ya sanamu. Ni bure kuendelea kufikiri kuwa kubusu msalaba ni kuabudu sanamu. Wakristo lazima waelewe kinachosema.
Siku zote maadui wa ukristo wamekuwa wakijaribu kupotosha imani ya asili na kuleta mafundisho yenye kutia mashaka mioyoni mwa waumini. Wasipotambua hayo, watakuwa watu wa kuyumbishwa siku zote katika imani.
Ibada ya sanamu
Tangu mwanzo Mungu alichukia sana ibada ya sanamu. wapinzani wa imani ya makanisa ya Kikatoliki na Kiapotoliki wanaitumia sababu hii kupinga taswira ya msalaba.
Amri ya pili inasema hivi.
'Usijifanyie sanamu ya kuchonga wala mfano wa kitu chochote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini majani chini ya dunia, usivisujudie wala kuvitumikia....'(Kutoka 20:4-5).
Neno la mwisho
Tumekwishaona jinsi msalaba ulivyo mti wa muhimu katika maisha ya wakristo, mengi tumezungumza juu ya mti huo, wengine wamefundisha juu ya kufanya ishara ya msalaba katika vipaji vya nyuso zao. Hiyo yote ni kutaka kuonesha kuwa msalaba siyo kitu cha kawaida.
Kama ni mfuasi wa Kristo unacho cha kujivunia nao ni msalaba wa Yesu....! Waambie watu juu ya mti huo uzaao matunda yake kila siku usiojua kiangazi wala masika hata usiku wala mchanani wa ajabu sana unaookoa siku zote.
Basi wanapoutazama au kuubusu msalaba si kama wanauabudu bali ni kuonesha heshima na upendo wao juu ya mti ambao ni kielelezo cha mti uliotumika kuwakomboa watu wengi.
Kwa maana hiyo tulichojifunza kutoka katika makala hii kuwa wakristo hawaiabudu sanamu ya Yesu ila wanaiheshimu kwa kuwa ndani ya mioyo yao wanajua hakika ya kuwa hawaiabudu ile sanamu bali sanamu ile inabaki kuwa kielelezo tu.
Wao wanamwabudu Mungu tu na Yesu kristo mwana pekee wa mungu na Roho Mtakatifu katika umoja usiogawanyika wenye nafsi tatu.
Wakristo waliojaaliwa kuijua siri ya thamani iliyomo katika msalaba, waoneshe kwa vitendo heshima na upendo wao kwa kuubusu ni tendo la furaha, upendo na uondoe tashwishwi, hofu kwa kuwa tendo hilo ni safi tena ni takatifu na lenye heshima mbele za Mungu.
MUNGU AKUTIE NGUVU ILI USIMAME KATIKA IMANI ILE ILE.