Ukweli ni upi kuhusu Oscar Kambona?

Ukweli ni upi kuhusu Oscar Kambona?

Afadhali na wenzagu pia mmeona udhaifu huoa katika maandishi ya Maggid.

Nilionya siku chache zilizopita kuwa maandishi ya ndugu Mjengwa yako based na hisia zake tu na wala hayafuati msingi halisi wa maarifa kuwa yawe factually correct hata kama hatupendi kusikia facts hizo. Nikasahihisha kauli yake moja kuhusu suti neckess za Nyerere kuwa hazikuigwa kutoka kwa Mao Tse-Tung kama alivyodai. Ni jambo la kusikitisha sana kuwa Mggid kama mwalimu alitakiwa awe anafundisha facts badala ya kufundisha propaganda. Fortunately, nina record nzuri sana kuhusu mgogoro baina ya Nyerere na Kambona ambayo nitaitoa mara baada ya Maggid kumaliza makala zake ambazo zimekuwa na habari nyingi za kutunga tu. Nadhani inapotokea mtu anataka kutoa historia tuwe tunalazimisha kuwa aje na verified references kusupport maneno yake.

Kichuguu ndugu yangu,
Wala huna sababu ya kunisubiri nimalize halafu ndio uje na unayodhani unayajua kuhusu Nyerere na Kambona kuliko wengine. Mie nimejitahidi tu kujua na naendelea na kujitahidi kujua. Hivyo basi, simulizi zangu hizi hazishi leo wala kesho maana ni kazi endelevu. Kajisemea Mzee Jongo; " Kijua ndio hicho kinawaka, anika muhogo wako kisha uutwangwe. Ukisubiri sana itanyesha mvua. Anika Kichuguu anika!
 
Tunachotaka ni historical facts kuthibitisha hayo madai yako, siyo simulizi au hadithi tu. Since you brought up these things, the onus of proof is on you. Huwezi kuandika thesis halafu ukategemea Wakosoaji au Wasomaji watakuwa na ushahidi wa kuthibitisha hoja au madai yako.

Hebu jazia hicho unachokifahamu wewe kwani hakuna sehemu nyingi ambayo taarifa hii imeandikwa. Labda kwenda kwenye hansard za bunge kama issues hizi zilifikishwa bungeni. Au taarifa za vikao vya TANU katika kipindi kile kama zitapatikana.
 
nakubaliana sana na hili la wakati, nimeshawahi kusema tena , kwenye blog yako kwamba mambo mengi yanakwenda na nyakati.
Dunia nzima ilikuwa imejaa woga miaka hiyo, nakumbuka UK watoto tulikuwa tunafundishwa namna ya kujikinga na bomu la nyuklia, kukaa chini ya meza nk.
mapinduzi kila kukicha in africa. COLD WAR, uKOLONI ULIKUWEPO BADO SEHEMU NYINGI AFRICA, , wakoloni walikuwa hatari sana, hasa kwa Tanzania.


-JE NI NCHI NGAPI ZILIENDELEA NA MFUMO WA VYAMA VINGI BAADA YA KUJIPATIA UHURU?

-JE WATANZANIA WA MIAKA YA 1965 WANGECHUKULIAJE MALUMBANO KAMA HAYA YA CCM VS CHADEMA?

-JE MAANDAMANDO KAMA HAYA YA CHADEMA/CCM/CUF TUNAYO YAONA SASA YANGEFANYIKA, MWAKA 1965 USALAMA UNGEKUWEPO?

- George washington rais wa kwanza wa marekani 1789- 1797 hakuwa na chama. sio Republican wala Democratic. nchi chaga inataka malezi kwanza, sio vyama vingi.

Thanks God Tanzania Changa ilipata Mtu salama- Julius nyerere (lakini sio malaika)
 
Kichuguu ndugu yangu,
Wala huna sababu ya kunisubiri nimalize halafu ndio uje na unayodhani unayajua kuhusu Nyerere na Kambona kuliko wengine. Mie nimejitahidi tu kujua na naendelea na kujitahidi kujua. Hivyo basi, simulizi zangu hizi hazishi leo wala kesho maana ni kazi endelevu. Kajisemea Mzee Jongo; " Kijua ndio hicho kinawaka, anika muhogo wako kisha uutwangwe. Ukisubiri sana itanyesha mvua. Anika Kichuguu anika!

Tukifanya hivyo, wewe uandike huku nami niandike kule tutakuwa hatuwafanyii wasomaji haki ya kusoma na kutafakali. Ingawa kuna sehemu ya maandishi yetu ambayo tutakuwa tunakubaliana na hivyo kupanua wigo wa ufahamu kwa wasomaji wetu, ni wazi kuwa tutakuwa sehemu nyingi ambazo hatutakubaliana na hivyo kuwa kama tunashindana, jambo ambalo litakuwa siyo zuri kwa msomaji. Acha tu twende kwa utaratibu huu wa makala kwa makala. Itakusaidia sana iwapo utakuwa unatoa references katika maandishi ya aina hii, kwani inakuwa inakuondoa kwenye responsibility ya kutetea ushahidi kwa uliyoandika
 
Maggid, Maggid, Kaka yangu Maggid. Nimesoma nakumbuka kusoma unayoyasema wakati nasoma Nairobi, pale maktaba ya University of Nairobi, huweka magazeti ya zamani - Nation enzi hizo alivyotoroka tu walimhoji. Tujuze.
 
Ni mwalimu aliyemjenga Titi na si Kambona. Uhasama wa mwalimu na Kambona haukuwa na tija kwa taifa lakini ukimlaumu mwalimu unakuwa biased, pale wote walitaka madaraka. Kambona angekuwa rais wa Tanganyika leo tungekuwa nchi tajiri? Nani kama Kambona aliweza kuifanya nchi ya kiafrika kuwa mahiri? Usisahau pia kuwa kulikuwepo uchonganishi mkubwa wa wazungu waliopelekea mtu kama Lumumba wa nchi jirani kuuwawa kikatili. Ulitegemea Nyerere angekaa tu kama zuzu? Oscar alijitahidi, lakini historia ndio iliyomkataa na sio Mwalimu Nyerere.
 
Na mbona unaleta mada vipande vipande? Au na wewe una hila kama mpendwa wako Oscar?
 
Kichuguu,
Tunakusubiria ndugu yetu. Naona Nyerere bado ni mwiba kwa wengi.

Usiwe na wasiwasi ndugu yangu, somo hili litakamilika sawasawa. nina bahati moja kuwa kutokana na majukumu yangu huwa ninajitahidi kuwa thorough sana. Nitaleta reference zilizo kamili kabisa kama ambavyo huwa nafanya siku zote ninapoleta hadithi ambayo mimi siyo mwanzilishi wake.

Take your time and remain actively engaged in the traditional JF fact-based discussions, not the this kind of mushrooming propaganda.
 
Na Maggid Mjengwa,

OSCAR Kambona aliondoka nchini na kuacha nyuma yake vumbi zito. Kulikuwa na kamata kamata iliyoendelea. Hakukuwa na habari kamili, bali uvumi ulioshamiri.



Na katikati ya vumbi na uvumi huo ulioshamiri kulikuwa na kimya kikuu. Kulijengeka hofu miongoni mwa wananchi, hususan wale wenye fikra za upinzani. Wengi walikuwa wapinzani kwa kunong’ona. Na utaratibu wa kila nyumba kumi kuwa na balozi wake kimsingi haukuwa na maana nyingine zaidi ya Chama tawala kuwa na udhibiti wa mambo ikiwamo fikra za wananchi.


Balozi wa nyumba kumi aliogopewa. Nje ya nyumba ya Balozi kulipepea bendera ya TANU. Utaratibu wa kuwa na balozi wa nyumba kumi ungekuwa wa maana zaidi kama ungekuwa ni wa mawasiliano ya dhati ya njia mbili. Balozi wa nyumba kumi ilikuwa na maana ya balozi wa TANU katika kila nyumba kumi badala ya kuwa balozi wa wananchi kwa TANU.


Balozi alitumika kupenyeza kwa watu wake yale yanayotoka juu. Na kutoka chini, kazi ya balozi mara nyingi ilikuwa ni kuwaripoti kwa viongozi wa juu wa TANU; ’ wakorofi’ walio katika nyumba zake kumi. Ndio chanzo cha wananchi kumwogopa hata balozi wao wa nyumba kumi.


Si ndio, na balozi wa nyumba kumi nae alikuwa kama ’ shushushu’, jJina walilopewa wale waliokuwa wakifuatilia nyendo za wananchi wenye kupinga mambo ya Chama na Serikali. Hii nayo ni historia yetu, imechangia katika kutufikisha hapa tulipo. Kujaribu kuikana historia hii ni kujaribu kujikana wenyewe.


Turudi kwa Oscar Kambona. Hatimaye baada ya kuikimbia nchi, Kambona akaishia London, Uingereza. Alikimbilia ’ Kwa mama’. Huko akapewa hifadhi ya ukimbizi wa kisiasa. Vumbi aliloliacha nyuma likachukua muda mrefu kutuama. Maana, huko alikokuwa, Kambona bado aliendelea kumtimulia vumbi rafiki yake Julius Nyerere. Oscar akawa mmoja wa ’ maadui wa nje’.


Mengi hayajulikani juu ya maisha ya Kambona akiwa Uingereza na hasa harakati zake za chini chini dhidi ya rafiki yake wa zamani Julius Nyerere. Na mara kadhaa, ulipotokea uvumi wa jambo baya au hujuma dhidi ya Serikali ya Tanzania, jina la Kambona lilisikika likitajwa.


Ni Kambona yule aliyeimbwa kwenye nyimbo za mchakamchaka mashuleni ; kuwa ’ aliolewa Ulaya’ kwa vile wivu ulimkereketa! Mathalan, katika kesi ya uhaini ya mwaka 1970, Oscar Kambona alituhumiwa kuwa nyuma ya mpango wa kumpindua Julius Nyerere. Miongoni mwa waliotuhumiwa kuhusika na mpango huo ni Bibi Titi Mohammed.


Jina la Oscar Kambona liliibuka tena na kuzungumzwa mitaani mara ile, mwaka 1982, vijana akina Memba na wenzake wanne walipoiteka ndege ya Shirika la Ndege la Tanzania, ATC, Boeing 737. iliyokuwa ikitokea Mwanza kwenda Dar. Waliilazimisha ndege hiyo chini ya kapteni George Mazola itue Nairobi. Hapo ikajaza mafuta, kisha ikaruka na kutua Jeddah, Athens na hatimaye uwanja wa Stansted, Uingereza.


Watekaji wa ndege, akina Memba na wenzake walitaka Oscar Kambona afike uwanjani hapo ili aongee nao. Kambona, alifika na kuongea na watekaji ndege wale. Hawakuwa na madai mengine bali kutaka wasaidiwe wabaki Uingereza. Na kuna abiria wengine pia waliotaka wabaki Uingereza.


Machoni mwa dunia ilionekana, kuwa Watanzania mfano wa akina Memba na wenzake walikuwa tayari kutumia mbinu zote alimradi waondoke kwenye nchi ambayo inadai imefanikiwa sana kwenye sera zake za Ujamaa. Hivyo basi, tukio lile lililotangazwa sana kimataifa kwa namna fulani liliudhalilisha utawala wa Julius Nyerere.


Juu ya yote, Oscar Kambona alikuwa nje ya mipaka ya Tanzania. Alipoteza mengi ikiwamo mmoja wa watoto wake aliyefia London. Na jina la Oscar Kambona likazidi kusahaulika kwa Watanzania wa vizazi vilivyofuata.


Na kuna Mtanzania aliyekuja na kuanza taratibu kufungua milango ya uhuru wa Watanzania kuongea ikiwamo kumshutumu mkuu wa nchi, Chama na Serikali, hadharani na kwa sauti. Si kwa kunong’ona. Mtanzania huyu anaitwa Ali Hassan Mwinyi. Kama Urusi ya zamani ilikuwa na Mikhael Gorbachev aliyefungua milango ya uhuru wa kuongea na kushutumu hadharani, basi, kwa Watanzania, Ali Hassan Mwinyi ndiye Gorbachev wetu.


Nilikuwa na Othman Nyamlani pale viwanja vya Ukumbi wa Diamond siku ile Nyerere anang’atuka rasmi na kumwachia mikoba ya Chama na Urais Ali Hassan Mwinyi. Mimi na Nyamlani tulikuwa wanafunzi wa Kidato cha Pili pale Tambaza Sekondari. Othman Nyamlani sasa ni Makamu wa Kwanza wa Rais, TFF.


Hotuba ile ya kwanza ya Ali Hassan Mwinyi pale Ukumbi wa Diamond ilifungua ukurasa mpya kwa nchi yetu. Mwinyi alionekana kuwa mnyenyekevu na mtu asiyejikweza. ” Ndugu zangu, kama mtanilinganisha mie na Mwalimu, basi, Mwalimu ni sawa na Mlima Kilimanjaro na mie ni kichuguu!” Alitamka Ali hassan Mwinyi huku akiwaacha wajumbe wa mkutano wakimshangilia .


Haukupita muda nikakiona ’ Kichuguu’ kile; Ali Hassan Mwinyi, katika nafasi ya Urais. Alasiri moja nilimwona Rais wa nchi, Ali Hassan Mwinyi akiwa amechuchumaa pale Mtaa Kongo, Kariakoo na kuongea na akina mama wauza mayai. Mwinyi alitembea kwa miguu akiongea na wananchi huku magari yasiyozi manne ya msafara wake yakiwa yameegeshwa kando ya Ukumbi wa DDC Kariakoo. Ndio, Mwinyi yule niliyemwona, alishuka chini na kuanza kuwasikiliza wananchi badala ya kusimama tu majukwaani na kuhutubia.


Na ni Mwinyi huyo huyo katika uongozi wake, akasikia, kuwa Oscar Kambona yuko njiani kurudi nyumbani. Kuna nguvu zilizokuwa zikitaka kuhakikisha Kambona hatui Dar es Salaam, lakini, yaonekana Ali Hassan Mwinyi hakuona ubaya wa Kambona kurejea nchini.


Maana, mwaka ule wa 1992, zilipokuja habari za kuaminika kuwa Kambona yuko njiani kuja, tulimsikia redioni Augustino Mrema akitamka kwa Kama Kambona angetua Dar Es salaam angekamatwa kwa vile alikuwa ana kesi ya uhaini.


Ikafika siku, Kambona akatua, hakukamatwa na wala hakuitwa mahakamani. Kama Rais Mwinyi angekuwa Rais mwenye chuki na kisirani, basi, angemwacha Mrema atume FFU Uwanja wa ndege. Waende wakamkamate Kambona na kuwapiga virungu wafuasi wake.


Oscar Kambona wa 1992 hakuwa tena Kambona wa 1967. Miaka 25 ya ughaibuni ilimpoteza hata kwenye fikra za watu wa kizazi alichokikuta. Akiwa London alianzisha chama cha siasa; Democratic Alliance. Chama ambacho kingekuwa mwevuli kwa wote wenye kuipinga CCM na mfumo wa chama kimoja. Na baada ya kuanzishwa kwa sheria ya vyama vingi Julai 1992 ndipo Kambona akafanya uamuzi wa kurudi nyumbani.


Hapa nyumbani Kambona akaandamwa na wahafidhina wa CCM. Kosa lake? Alionyesha nia ya kutaka kushindana kisiasa. Mathalan, Kambona akaambiwa si Mtanzania. Ni Kambona yule yule aliyeaminiwa na rafiki yake Julius Nyerere hata akapewa Uwaziri wa Ulinzi achilia mbali kuwa Katibu Mkuu wa kwanza wa TANU.


Na tangu siku ile alipotua Dar, Nyerere hakusema lolote hadharani kumhusu rafiki yake wa zaman na jirani yake pale Msasanii; Oscar Kambona.
Ndio, Kambona wa 1967 hakuwa tena kambona wa 1992. Oscar Kambona alionekana kuzeeka. Alikuwa mgonjwa pia. Hakuonekana kuwa na nguvu za kupambana majukwaani. Hatimaye akarejea tena London kwa matibabu. Alifia London mwaka 1997.


Jeneza lenye mwili wake likasafirishwa kuja Dar. Na pale Uwanja wa Ndege kulikuwa na ujumbe wa maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje uliokwenda kuupokea mwili wa marehemu. Na unajua ni nani aliongoza ujumbe huo wa wizara?


Nisikuumize kichwa; ni Jakaya Mrisho Kikwete. Wakati huo alikuwa Waziri wa Mambo ya Nje. Kikwete , hata katika mazingira ya wakati huo, alikuwa na ujasiri wa kisiasa wa kwenda kuupokea mwili wa ’ shetani’ wa kisiasa wakati waziri mwingine asiyejiamini angefunga safari ya kikazi nje ya Dar kuepuka ’ dhambi’ hiyo.


Kuna mengi ya kuandika. Lakini, kufanya hivyo itakuwa ni sawa na kuchapa kitabu gazetini. Kama nilivyobainisha kwenye makala ya kwanza, kuwa makala haya ni jaribio la kuvunja ukimya wa yaliyotokea miaka 50 iliyopita.


Na ni zaidi ya mahusiano ya Nyerere na Kambona. Kuna mengi mengine tunayopaswa kuyasema. Maana, kwa miaka 50 sasa, tumekuwa ni watu wa kuimba nyimbo za kutukuza. Kuyasema mabaya tuliyoyapitia haina maana hakukuwa na mazuri, bali, ni muhimu na mabaya nayo yakasemwa ili tujifunze.
Na kama nilivyobainisha huko nyuma, kuwa moja ya chanzo cha matatizo yetu ya sasa ni dhambi ya ubaguzi wa kisiasa iliyoasisiwa kwa miaka mingi iliyopita. Na kuwa hata uozo wa kimaadili na ufisadi uliotamalaki katika nchi yetu ni matokeo ya dhambi hiyo ya ubaguzi wa kisiasa inayoendelezwa. Si tumeisikia nyimbo hii; " Wapinzani, tuwakatekate, tuwatupe!| CCM, tuwakumbatie , tuwabusu!" Nahitimisha.


Mungu Ibariki Afrika, Mungu Ibariki Tanzania.
MJENGWA - Picha, Habari & Matangazo
 
Ahsante sana kaka Maggid! Hakika you made my day....unajua si wengine ni wa kizazi cha dot com, kwahiyo tunapopewa vitu kama
hivi ni faida kubwa sana kwenye maisha yetu. Pia tunajifunza kuwa hizi siasa za chuki na majitaka hazikuanza leo kwenye chama cha magamba
 
yaah....kastori katamu inagawa kanaumiza hisia za wapenda demokrasia...suala la Vasco da Gama II kwenda kupokea mwili wa Kambona halina ubishi kwa kuwa Vasco alikuwa na uadui na Mwalimu tokea ile ishu yake ya Monduli
 
Oscar Kambona was one of the best presidents Tanzania never had.
 
Oscar_Kambona-1.jpg

Na shaka sana na tabia ya baadhi ya wanaojiita "wachambuzi" jinsi wanavyoshindwa kutetea wanachokiamini kwa hoja, orodha ni ndefu sana ya maandiko ya kihistoria ya miaka ya karibuni yanaoonyesha dhahiri kutokuwa na ushahidi(Rejea ndoto ya Mwanakijiji Tanzania Daima na Udhaifu wa Maandiko ya Mohamed Said Kwenye Kitabu Kuhusu Nyakati Za Abdulawaheed Syskes).

Mara nyingi wanahistoria wetu wanapenda kutumia neno "INASEMEKANA"ambalo kimsingi halina uzito wa kimantiki bali limejengwa kiimani na kimasimulizi hivyo linakosa uhalali kwenye jamii iliyoamua kuishi kwa misingi ya kisayansi (iwe sayansi ya jamii, historia n.k)

Hoja yangu leo ni kuhusu aliyewahi kuwa waziri wa mambo ya nje wa Tanganyika na baadaye Tanzania pia katibu mkuu wa Tanu Marehemu Oscar Salathel Kambona.

Nimepitia maandiko mbalimbali, nimejaribu kuonana na watu mbalimbali (wazee) na hata baadhi ya wanataaluma ila nimekosa kupata hoja za msingi kwanini Oscar Kambona anapambwa na baadhi ya waandishi? Katika hilo nimepata simulizi zifuatazo...;

1. Haijawahi kutokea Mtanganyika/Mtanzania anayependwa kama Oscar Kambona(watu walimwiga hadi style ya nywele zake)
2.At least alikuwa Mtanganyika wa kwanza kuthubutu kumpinga Nyerere waziwazi
3.Alimwoa Miss Tanganyika wa mwaka 1960 aliitwa Flora yungalipo mpaka leo(ndoa ilifanyika Anglican catherdral London Nyerere alikwa best man wake)
4.Alikuwa anapenda sana mambo ya kizungu ndiyo maana alipokwenda nje na Nyerere, Nyerere hakupenda kumpa nafasi ya kuongea kwasababu alihofia atasifia wazungu tu mfano ziara ya Marekani kuonana na rais Kennedy 1963 Kambona alikuwa msikilizaji tu.
5.Alipokuwa Uingereza aliendeleza mashambulizi yake dhidi ya Nyerere na aliporejea Tanzania alitangaza azma yake ya kueleza maovu ya Nyerere lakini hakuthubutu(labda alikuwa hana)
6.Siri zilkuja kufichuka kuwa huko Uingereza aliishi mitaa ya hohehohe na aliishi kwa kufanya kazi za kawaida tu

HITIMISHO NA MASWALI YA MSINGI
a. Ni lini Oscar Kambona alikuwa mwandishi wa BBC? na je alikuwa na taaluma gani? na alisoma shule zipi? na vyuo gani? nchi gani?
b.Kwanini Oscar Kambona aligombana na Nyerere? ni tofauti za kiitadi au mitazamo?
c.Kati ya Oscar Kambona na Kawawa nani alikuwa bora kwenye maswala ya uongozi?
d.Je ukweli ni upi? tatizo alikuwa Nyerere au Oscar Kambona? kiini hasa ni nini?
e.Kwanini Oscar Kambona alipokufa , Kikwete akiwa waziri alienda kupokea mwili wake pale Airport? na nini kilimuua Oscar Kambona?
f.Je Oscar Kambona anastahili sifa anayopewa na baadhi ya waandishi? kwa nini? na je kwanini watanzania walikuwa wanampenda sana? na je watoto wake na mkewe (aliwahi kuwa mwenyekiti wa TADEA)wako wapi? na wanafanya nini? waingereza wanamwongeleaje Oscar Kambona?
FINALLY I WANT TO KNOW WHO IS OSACR KAMBONA? NAHISI KAMA BADO SIJAMWELEWA KIUNDANI...........! (NAWASILISHA JF)
 
JE, UNAMFAHAMU OSCAR KAMBONA?


Wakati mjadala unaendelea sehemu mbalimbali Tanzania,kuhusu vigezo vilivyotumika katika kuwatunuku baadhi ya watanzania nishani za heshima wakati wa maadhimisho ya miaka 50 ya Tanganyika,nimejikuta namkumbuka Oscar Kambona,miongoni mwa watu ambao hawajapata nishani hizo zilizotolewa na Rais Kikwete.Ni ngumu sana kujua kwa usahihi kwanini watu kama Oscar Kambona hakuweza kuwa miongoni mwa watu waliopata nishani hiyo,mtu ambaye anatajwa kuwa mtu muhimu sana katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika,na pengine mtu maarufu zaidi katika historia ya taifa letu (Tanganyika) nyuma ya Mwalimu Nyerere.

Tuachane na mambo ya nishani.Lakini ni Watanzania wangapi wanamfahamu au kufahamu historia ya Oscar Kambona?Kama ambavyo nimewahi sema kwamba tatizo letu kubwa watanzania sio wakweli,hata watu tunaowategemea sana waweze kutujuza mengi,hawafanyi hivyo,na hata wakifanya wanapotosha ukweli kwa masilahi ya baadhi ya watu.Mengi sana yamesemwa (mazuri na mabaya) kuhusu Oscar Kambona.Hivyo si rahisi sana kueleza kwa ufasaha historia ya Oscar Kambona,na maelezo hayo yakakubalika na watu wote,kwani kuna watu walimwona Kambona kama mpiganaji,mwenye msimamo usiyoyumba,aliyewapenda watanzania,na wengine wanamwona kama Msaliti na mnyonyaji au mwizi wa mali za umma.

Oscar Salathiel Kambona alizaliwa mnamo tarehe 13/08/1928 katika kijiji cha Kwambe karibu na Mbamba Bay huko Mbinga Ruvuma,akiwa ni mtoto wa David Kambona (baba) na Miriam Kambona.Kama inavyofahamika kwamba shule kwa wakati huo zilikuwa chache,Oscar Kambona alipata elimu ya msingi kijiji kwao ambapo alikuwa anafundishwa na Baba na mjomba yake ambao walikuwa walimu.Aidha Kambona alisoma shule ya kati ya St.Barbabas na shule ya sekondari ya Alliance iliyokuwa Dodoma,kabla yajajuinga na High School (Tabora Boys) ambapo alikutana na Mwalimu Nyerere ambaye kwa wakati huo alikuwa anafundisha shule ya St.Mary’s huko Tabora.

Inasemekana Mwalimu Nyerere na Oscar Kambona walikuwa marafiki sana kabla hawajakorofishana baada ya kupata uhuru.Urafiki wao ulianzia Tabora ambako inasemekana walikuwa wanakutana mara kwa mara na kujadili jinsi ya kuikomboa Tanganyika katika mikono ya wakoloni.Na hata Oscar Kambona alipokuwa anaoa,Mwalimu Nyerere ndiye aliyekuwa best man wake.Mara kadhaa Mwalimu Nyerere,alikuwa anamwita Kambona kama rafiki yake mkubwa.

Oscar Kambona alikuwa Katibu wa chama cha TANU,wakati Mwalimu Nyerere akiwa Rais wa TANU.Wakati huo nafasi ya Ukatibu ilikuwa nyeti sana.Hivyo Oscar Kambona alikuwa bega kwa began a Mwalimu Nyerere katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.Inahitaji kuwa mwendawazimu kushindwa kumtaja Oscar Kambona katika harakati za kudai uhuru.Aidha Kambona anasemwa kuwa ni mtu ambaye alikuwa anapendwa sana na watu hasa vijana,ambao hata wengi wao waliamua kuiga mtindo wake wa nywele.Kambona pengine alikuwa mtu maarufu nyuma ya Nyerere,na ndiye aliyekuwa waziri wa kwanza wa mambo ya kigeni katika serikali mpya ya Tanganyika huru.

Baada ya kupata uhuru,tofauti za kimtazamo na kiitikadi zilianza kujitokeza kati ya Mwalimu Nyerere na Oscar Kambona.Inasemekana Oscar Kambona alikuwa anampinga waziwazi Mwalimu Nyerere juu ya sera zake,wakati mawaziri wengine walikuwa wanakubali kila kitu walichokuwa wanaambiwa na Mwalimu Nyerere.Ni Oscar Kambona na Chief Abdallah Said Fundikira 111 (waziri wa kwanza wa mambo ya Katiba wa Tanganyika huru,japo hakudumu kwenye baraza kwa sababu ya kutofautiana na Mwalimu Nyerere).Na mara kadhaa Oscar Kambona alikuwa anamtuhumu Mfaume Kawawa (wakati huo akiwa makamu wa rais) kuwa alikuwa anawachonganisha na alikuwa ni mtu wa kuchukua kila kitu ambacho alikuwa anasema Mwalimu Nyerere.

Tofauti kubwa zilianza kujitokeza kati ya Oscar Kambona na Mwalimu Nyerere baada ya jeshi la Tanganyika kuasi tarehe 18/01/1964.Katika uasi huo wa jeshi,Mwalimu Nyerere na Kawawa walijificha kwa hofu ya kuwawa,ni Kambona tu ambaye alikuwa waziri wa ulinzi kwa wakati huo,aliyejitokeza hadharani na kuongea na waasi hao.Kutokana na ushawishi wake,wanajeshi hao waliamua kusitisha mpango wao kwa vile walikuwa wanamkubali sana Kambona kuliko Mwalimu Nyerere.

Kuna watu wengine wanaamini kwamba uasi huo ulikuwa umepangwa na Kambona ili aweze kumpindua Mwalimu Nyerere ambaye alianza na kuwa na tabia ya haambiliki.Wanaoamini hivyo wanasema Kambona na baadhi ya wazanzibar kama vile Kassim Hanga walikuwa wamepanga kufanya mapinduzi kwa pamoja kwa Zanzibar na Tanganyika,lakini kiherehere cha John Okello kilifanya mpango huo kushindwa kwa vile aliwaisha mapinduzi ya Zanzibar yaliyotokea tarehe 12/01/21964.Hivyo hata Mwalimu alianza kuingiwa na wasiwasi kuhusu mwenendo wa Oscar Kambona,hasa baada ya kufaulu kuzima uasi wa jeshi.Huenda Mwalimu Nyerere alikuwa anajiuliza iweje wanajeshi wafanye uasi huo na wakati huohuo wamsikilize kwa haraka sana Oscar Kambona ambaye naye alikuwa ni sehemu ya serikali ya Mwalimu Nyerere?

Si rahisi sana kusema Oscar Kambona alishiriki katika kupanga mpango huo,ama hata kusema hakushiriki.Lakini zaidi inatakiwa kufahamika kwamba uasi wa jeshi ulitokea katika nchi zote za Afrika Mashariki,na madai yao walikuwa yaleyale,mafao zaidi na kuondolewa kwa wazungu waliokuwa na vyeo vikubwa jeshini wakati nchi ilikuwa imepata uhuru.Uasi wa jeshi ulianza kuonyesha wazi ufa ulioanza kujitokeza katika urafiki wa siku nyingi sana kati ya Nyerere na Kambona.

Suala la pili lililofanya Kambona na Mwalimu Nyerere kutofautiana ni suala la chama cha TANU kushika hatamu baada ya tangazo la kuvuta mfumo wa vyama vingi ambao ulikuwa upo tangu enzi za mkoloni.Kambona aliona suala hilo ni sehemu ya kudidimiza demokrasia nchini na kuifanya TANU ishindwe kujirekebisha kwa makosa yake.Madai ya Mwalimu Nyerere kuhusu kufuta vyama vingi ilikuwa ni kujenga taifa lenye mshikamano.Lakini kuanzia hapo chama kilikuwa kimeshika hatamu,na kuwa ni kila kitu katika maamuzi.NEC ya TANU ilikuwa na nguvu kuliko hata baraza la Mawaziri.Na ikumbukwe katika hilo,TANU iliamua kuwafukuza wanachama wake ambao walikuwa wabunge kwa madai kwamba walikuwa wanakihujumu chama kwa harakati zao za kudai uhuru wa Bunge.Waliofukuzwa uanachama ni pamoja na Mh.Choga (mbunge Iringa),Eli Anangisye (Rungwe mbunge),Mwakitwange (mbunge),Oscar Kambona (mbunge) n.k.Huo ulikuwa mwaka 1967 katika mkutano wa TANU Taifa uliofanyika Tanga.

Kubwa zaidi lililofanya urafiki wa Mwalimu Nyerere na Kambona kuwa uadui ni Tangazo la Kuanzisha Azimio la Arusha.Azimio la Arusha ndio ukawa mwisho wa safari ya urafiki kati ya Nyerere na Kambona.Wakati azimio la Arusha linatangazwa huko Arusha ilibidi Mwalimu Nyerere,Kawawa na Kambona kukaa chemba ili kuweza kumaliza tofauti zao zilizojionyesha wazi katika mkutano huo.Kikao hicho hakikuweza kumaliza tofauti zao.Na hapo ndio uadui hasa wa Kawawa na Kambona ukakolea.Kambona alikuwa anamtuhumu Kawawa kuwa hawezi kufikiria kama yeye,muda wote alikuwa anamuunga mkono Mwalimu Nyerere.

Tofauti kati ya Mwalimu na Nyerere ilikuwa ni itikadi zaidi.Wakati Mwalimu alikuwa anataka kuanzisha vijiji vya ujamaa kila sehemu ya nchi hii,Kambona alishauri kuwa ni vema wangefanya majaribio kwanza kwa kuanzisha vijiji vya mfano,ili kama vijiji hivyo vingefanikiwa katika mipango hiyo ndipo sasa wangeanzisha nchi nzima.Azimio la Arusha lilikuja miezi michache tu baada ya Mwalimu Kutoka katika ziara huko Uchina ambapo kulikuwa na vijiji vya ujamaa.Hivyo Kambona aliona Mwalimu Nyerere ameiga,na kwa kuwa mazingira yalikuwa tofauti kati ya China na Tanganyika hivyo isingekuwa vyema kuiga kila kitu.Lakini Mwalimu Nyerere aliamua kushikiria wazo hilo.

Baada ya kuona tofauti zao zinazidi kukua,Kambona aliamua kuondoka nchini na kwenda uhamishoni nchini Uingereza,miezi sita baadae baada ya kutangazwa Azimio la Arusha.Kambona alisema aliondoka nchi mke wake pamoja na watoto wake,kutokana na kuhofia usalama wa maisha yake.Huku nyuma,baada ya Kambona kuondoka,kukawa na maneno mengi ya kumtuhumu Kambona kuwa amekimbia na fedha nyingi sana,na serikali ikiwa mstari wa mbele katika kumtuhumu,lakini wakati huohuo inasemekana serikali ilikuwa inajua safari ya Kambona,lakini bado hawakumkamata.Hata watoto wa shule walikuwa na nyimbo za kumkashifu Kambona.

Baada ya Kambona kuondoka,Mwalimu Nyerere akiongea na wazee na Dar Es Salaam na radio RTD alinukuliwa akisema Kambona aliondoka na fedha nyingi sana ambazo hazikuendana na mshahara wake.Lakini Oscar Kambona alijibu mapigo kwa kuitisha mkutano na waandishi wa habari London mwaka 1968,kwamba kama kweli yeye alikuwa ameiba fedha,basi serikali ifanye uchunguzi dhidi yake,kitu ambacho serikali haikufanya.Lakini pia kuna habari nyingine zinasema,Kambona aliishi maisha ya chini sana nchini Uingereza,kwa kufanya kazi za ujira mdogo ili familia yake iweze kuishi,hivyo kama kweli alikiwa ameiba basi asingeishi maisha ya chini hivyo.Kambona alimtuhumu mara kadhaa Mwalimu kwa alikuwa dikteta .

Katika sera ya kutaifisha mali za watu binafsi,serikali kupitia Makamu wa Rais Kawawa ambaye ndiye aliyekuwa mkuu wa shughuli za serikali bungeni,alilitarifu bunge kwa Kambona alikuwa ana miliki majumba na mali mbalimbali katika mikoa mbalimbali,hivyo serikali iliamua kutaifisha mali zote za Kambona.Aidha Kawawa aliwaambia wabunge kuwa Kambona alikuwa na fedha nyingi sana,na kuonyesha transactions zilizokuwa zinafanyika na Kambona mwaka 1967 za kuhamisha fedha.Lakini baadae madai mengi yalianza kuonekana ya uongo na kutungwa ili kuweza kumchafua Kambona mbele ya umma wa Watanzania.Baadhi ya majumba yaliyokuwa yanasemwa ya Kambona,na ambayo yalikuwa yametaifishwa yalirudishwa kwa wenye nyumba hizo japo kisirisiri.

Kambona alirejea nyumbani Tanzania mwaka 1992 baada ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi.Serikali ilianza kuweweseka kuhusu ujio wa Oscar Kambona.Serikali ikatangaza kwamba Oscar Kambona hakuwa Mtanzania,alikuwa ni mtu wa Malawi au Msumbiji.Hata akanyang’anywa passport ya kusafiria,japo baadae walimwachia.Baada ya hapo,Kambona naye alijibu mapigo akisema Mwalimu Nyerere,Kawawa na Malecela hawakuwa watanzania.

Kuna wananchi ambao bado walikuwa wanampenda sana Kambona hasa ambao walikuwa wamemchoka Mwalimu Nyerere,hivyo kurejea kwa Kambona kuliwapa matumaini,japo kuwa Kambona wa mwaka 1992 hakuwa Kambona yule wa enzi za uhuru.Kambona alionekana amechoka sana.Kuna wakati aliahidi kuwa ataongea mambo mengi kuhusu rafiki yake wa zamani Mwalimu Nyerere hasa mali alizokuwa anamiliki,lakini akashindwa kudhibitisha madai yake,na hivyo kupunguza imani yake kwa wananchi.

Oscar Kambona alifariki dunia mwaka 1997,lakini hadi anafariki hawakuweza kuonana na Mwalimu Nyerere ili kuweza kumaliza tofauti zao.Na kibaya zaidi Mwalimu Nyerere hakuweza hata kuhudhuria mazishi ya rafiki yake wa zamani.

Pamoja na tofauti za kiitikadi kati ya Mwalimu Nyerere,Kambona anabaki kuwa mtu muhimu sana katika harakati za kudai uhuru wa Tanganyika.Oscar Kambona alikuwa mtu maarufu sana na alipendwa sana na watu hasa vijana,na iliaminika kwamba baada ya Mwalimu Nyerere kustaafu,basi Kambona angeweza kuwa rais wa Tanzania.Tunajifunza nini katika ugomvi wa Mwalimu Nyerere na Oscar Kambona hasa katika mfumo wa vyama vingi na katika harakati za kujenga taifa moja?

Je,wewe unamfahamu vipi Oscar Kambona?na unafikiri hastahili kuenziwa kama mmoja wa watu muhimu sana katika uhuru wa Tanganyika?Ni nini tafsiri yake,kwa Rais Kikwete kumnyima nishani Oscar Kambona na watu wengine ambao tunaona wana umuhimu sana katika historia ya taifa letu?
 
Back
Top Bottom