Simbachawene: Sijawahi kuona mchakato wa uchaguzi CCM kama wa mwaka huu.
Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene.
"Baadhi ya wagombea walifanya kampeni kama vile ni wanachama wa vyama vya upinzani," alisema Simbachawene.
Simbachawene ambaye hata hivyo aliyetangazwa kuwa mshindi wa kinyang'anyiro hicho alijizolea kura 18,158.
Matokeo hayo yalitangazwa na Katibu wa CCM wa Mkoa wa Dodoma, Albert Mgumba.
Jumla ya makada wanane wa CCM waliwania nafasi hiyo katika jimbo hilo huku aliyemfuatia Simbachawene akiwa ni Gabriel Mwikola, aliyepata kura 6,901.
Simbachawene alisema inaelekea mfumo wa wanaogombea uongozi kwa kudhaminiwa na vyama vya siasa, sasa umepitwa na wakati.
Alisema Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, inaelekeza mtu anayetaka uongozi kwa kupigiwa kura na wananchi, awe mwanachama wa chama cha siasa, sharti ambalo hata hivyo, alisema limeanza kupoteza umuhimu wake ndani ya jamii ya Kitanzania.
Alisema ni bora Katiba inayopendekezwa ambayo ina kipengele kinachoruhusu mgombea binafsi ipitishwe ili wananchi wapate fursa ya kupima ubora wa aina mbili za viongozi; wanaotokana na vyama vya siasa na wale wanaojidhamini wenyewe.
CHANZO: NIPASHE_7th August 2015