Niseme ukweli, japo mchungu, kuwa upinzani tulionao hauwezi kujitoa maana wapinzani wengi nao wanapigania vyeo si mabadiliko. Wanasema siasa inalipa! Wako tayari kushiriki uchaguzi wanaouita uchafuzi, batili na haramu ilimradi waambulie udiwani, ubunge na kura za urais za kuongezea ruzuku za vyama vyao. Wengi (si wote) wanagombea maslahi yao binafsi, si maslahi ya umma!
Mara kadhaa nimewahi kuwashauri kwamba tupiganie tume huru kwanza, katiba mpya kwanza, wagombea huru kwanza na mifumo mingine mipya kwanza ndiposa tuingie kwenye uchaguzi, lakini wapi. Ni dhahiri kuwa bila uwanja sawa wa kisiasa, bila kuwa na refa (tume huru) asiyeegemea upande wowote ni kushiriki kwa hiari uchafuzi, ubatili na uharamu. Wasilalamike!
Kenya na Malawi walimwengua rais aliyepitishwa na tume za upendeleo kwasababu walibadili mifumo ya uchaguzi na kuruhusu matokeo kuhojiwa mahakamani. Lakini wapinzani wetu wanataka vyeo kwanza na marupurupu yake!
Nawaomba baada ya uchaguzi wakae kimya, wasilalamikie dosari zozote zitakazojitokeza, maana wamekubali kushiriki uchaguzi chini ya tume na mifumo mingine wanayodai batili na haramu. Ukikubali kushiriki kula chakula unachojua kina sumu na haramu, usilalamike utakapoanza kuharisha!