Tanzania ya "Shamba la Bibi " ilianzia kwenye CCM shamba la bibi na Upinzani shamba la bibi, kwa ujumla vyote vilizaa matunda ya Ufisadi, wizi, uhuni, utapeli, ukosefu wa maadili na kustawisha shamba la bibi kwa muonekano wa kitonga na kufanya maisha ya wajukuu wa bibi kuwa mepesi sana, kiasi cha kumiliki visima vya mafuta, vitalu katika mbuga zetu, biashara za magendo na kujiita wenye Shamba na kusema wao ndio watengeneza "Mabwana Shamba".
Shamba la bibi lililea na kusomesha wajukuu ambao baadae waligeuka wezi na kuiba katika shamba hilo hilo la bibi, Wajukuu hao wasomi waliliingiza Shamba la bibi kwenye mikataba feki, mibovu na ya kibeberu kwa faida ya matumbo yao, uhuni katika vitengo walivyopewa wakiaminiwa kwa maslahi ya Umma.
Ifike mahali tuseme imetosha, tumechoka kuwa shamba la bibi,tuwakemee watu kama Zitto anayesema anautaka urais ili watu wale bata.
Zitto anataka kuturudisha kwenye Tanzania ya "Shamba la bibi "ambapo baadhi ya watu walipewa dhamana na Serikali katika nyadhifa mbalimbali wakakosa maadili ya uongozi kwa makusudi ama kwa bahati mbaya na wakasababisha uzembe ambao umeligharimu Taifa.
Hasara kubwa ambayo watanzania wameipata ni kupoteza fedha nyingi ambazo zingeweza kuisaidia Serikali kuboresha maisha ya watanzania katika nyanja mbalimbali za kielimu.
Fedha ambazo zimepotezwa na Wajukuu katika "shamba la bibi" leo hii zingeweza kusaidia kuinua maendeleo katika nyanja mbalimbali za kielimu, afya na kiuchumi kwa lengo la kusogeza karibu maendeleo kwa wananchi katika maeneo mbalimbali hususani maeneo ya vijijini.
Juhudi kubwa zinazoonyeshwa na Rais John Magufuli kupigania na kuzilinda rasilimali za nchi ambayo ilikuwa "Shamba la bibi" kwa maslahi ya Taifa ni jambo ambalo litasaidia kuchangia kwa kasi harakati za kimaendeleo.
Kwa jicho la kifalsafa na kwa uwanda mpana na mrabaha wa kibeuzi inatupa fasiri yakinifu kuwa CCM isipokuwa safi, basi hata taifa hili litanuka kwa uchafu na utakatifu hautakuwapo Lumumba hata Magogoni, kwa maana upigaji wa wajukuu wasomi waliotuingiza kwenye mikataba mibovu,utaendelea kuliumiza taifa hata pale atakapopatika wa kuisafisha Lumumba na kuifanya safi na nyeupe kama karatasi.
Ni kwa msingi huo, nathubutu kumpongeza Rais John Magufuli kwa kuamua kusafisha nyumba yake (CCM), kwani huku ndiko tunakopata viongozi wa kisiasa wanaokwenda kushika madaraka Serikalini.
Namuona Membe katika mlingayo wa kuhusianisha falsafa ya Lowassa pale makundi mbalimbali ya watu yalipojitokeza kwenda kumshawishi agombee urais akiratibu kundi la bodaboda,Mama ntilie,Mashehe na Wachungaji na kundi la 4u Movement, Kwa fasiri jadidi Membe anakopi ya Lowassa na kutaka kuwafanya Watanzania ni majuha kwa kutaka kuirudisha Tanzania ya "Shamba la bibi " Kwa ufupi Malumbano, misigano na mitafaruku yote ni kupata suluhu ya kufanya maisha bora na kula bata kama atakavyo Zitto na kuifanya Tanzania kama imefika kilele cha mafanikio ilihali tumefunikwa na wimbi la umasikini.
Kiini na kitako cha kutoa cha gumzo hili ni kukumbusha tulipotoka kwa maana anayesahau historia basi hajui aendapo, Nakumbusha enzi za watu kutamba kwa kusema "hii nchi tumeiweka mfukoni" unanijua Mimi ilihali wasijue wanayemtambia kuwa ni yule mzee aliyejenga reli ya kati kwa fimbo na kwa malipo ya thumuni.
Nimejitahidi kuumba fikra kwa ufupisho ili kukidhi matakwa ya hadhira ya jamii.
Ni rahisi kutamba upo juu ya Chama,lakini ni vigumu na inachukua miongo na falsafa ngumu sana kumpata "Mao Zedong wa Taifa la China ama Julius Nyerere wa Taifa la Tanzania" mumpatapo mpeni ushirikiano kama wachina walivyompa ushirikiano Mao Zedong na kukifuma upya chama na Taifa na sasa wachina wanatembea kifua mbele duniani.
Kikundi cha watu wachache ndani ya CCM,Chadema,ACT wanaotaka kuirudisha nchi yetu kuwa Tanzania ile ya Shamba la Bibi kamwe tutawapinga na hatutaruhusu wamhujumu rais wetu Mzalendo wala kuihujumu Tanzania iwe ndani ama nje ya nchi, Tunahitaji Magufuli wengi kuanzia ngazi ya shina, mtaa, Kata, Wilaya na Mkoa ili kuweza kuitengeneza upya Tanzania kutoka Tanzania iliyokuwa "Shamba la bibi".
Niwatakie tafakuri jadidi na ubeuzi mwema wa gumzo hili na kuwapiga Vita wale wote wanaotaka kuturudisha kwenye ile iliyokuwa Tanzania ya Shamba la Bibi.