Habari za Jumapili waungwana
Uchaguzi mkuu wa Urais, wabunge na madiwani unatarajiwa kufanyika 2020 hapa nchini. Ni kiasi cha kama miaka miwili tu ijayo
Kwa mtazamo wangu huu ndio muda muafaka kwa wale wote wanaotaka kugombea hasa nafasi ya Urais wawe ndani ya Chama tawala au Upinzani wajitokeze mapema na kutangaza nia zao za kuomba ridhaa ya vyama vyao kugombea nafasi hiyo
Kwa kufanya hivyo watakua wanatutendea haki Watanzania kwa sababu tutakua na muda wa kutosha kuwapima uwezo wao wa kila nyanja
Miaka miwili ya kumsoma mtu mwenye nia ya kua Rais wa nchi yetu inatosha kabisa kufahamu utimamu wa afya yake ya akili, uwezo wake wa kiuongozi, uwelewa wake wa masuala muhimu ya ndani na nje ya nchi, kuchimba historia yake, uadilifu wake kuanzia ngazi ya familia na uzalendo alionao kwa nchi.
Itatupa pia nafasi ya kumpima uwezo na utayari wake wa kuunganisha nchi hii ambayo inamchanganyiko wa matabaka mbalimbali ya kijamii. Pia itatupa fursa ya kumjua mtia nia anauelewa gani kuhusu dunia ilivyo, uchumi unaendeshwaje na kama anatambua kinaga ubaga changamoto zainazoikabili dunia yetu na mikakati yake ya kuivusha salama nchi yetu katikati ya changamoto hizo
Huu ndio utaratibu uliopo katika nchi hasa zilizoendelea. Ni utaratibu ambao unahakikisha kua Rais ajae anakua ni mtu mwenye uwezo hasa wa kua kiongozi wa nchi na sio kituko
Tatizo tulilonalo kwenye nchi yetu ni kwamba tunataka surprises za dakika za mwisho. Tena tatizo hili lipo kwa vyama vyote vya siasa. Wanatuletea tu wagombea huku wanatuona Watanzania ni mazwazwa, tutamchagua tu hata watuwekee jiwe ilimradi chama kimempitisha! Utamaduni wa kuteua wagombea kama bahati nasibu ipo siku utatugharimu kama Taifa!!! Tutakuja kumpata Rais wa ajabu haijawahi kutokea, atakaekua ni aibu na fedheha kwa Taifa
Binafsi sijamsikia Bernard Membe akitangaza nia ya kugombea Urais lakini yalipoletwa madai kama anayo nia hiyo yametokea maoni tofauti ambapo watu wengine wanamuunga mkono na wengine wakimpinga na hata kumkashifu na mwenyewe hajakubali wala kukataa madai hayo
Kwa mtazamo wangu kama kweli Bwana Membe anayo nia ya kugombea nadhani kafanya jambo zuri sana. Huu mjadala unaoendelea kumuhusu naona kama ni mjadala wenye afya sana ambao unaweza kutuonyesha uwezo na mapungufu ya Membe ili wananchi wamjue na waamue
Badala ya kusema hana haki ya kugombea(kwa utamaduni wa CCM?) mjadala ungejikita katika kuchambua uwezo wake na mapungufu yake na kama hafai basi mapungufu yake yasemwe waziwazi na kama anafaa basi isiwe nongwa kwa yeye kutia nia ya kugombea
Ningependa na watu wote wenye nia hiyo kutokea vyama vyote wangefanya hivyo na wao ili watupe fursa na muda wa kutosha wapiga kura wa kuweza kuwachambua na kuwajua na isije kua tena mambo ya kushangazana dakika za mwisho