Katika kipindi cha kati ya mwaka 1959 hadi 1961 China ilikumbwa na tatizo kubwa la uhaba wa chakula, tatizo ambalo lilisababisha madhara makubwa ya kiuchumi na kijamii na hata vifo kwa watu wengi. Tatizo la uhaba wa chakula nchini China lilitokana na ukame na hali mbaya ya kijiografia, na hata sera zisizo rafiki kwa maendeleo ya kilimo. Lakini miaka 40 baadaye, sio tu China imetokomeza tatizo la uhaba wa chakula, bali pia imekuwa ni msafirishaji mkubwa wa chakula nje ya nchi.
Bara la Afrika ni bara ambalo bado linasumbuliwa na changamoto ya usalama wa chakula, hali ambayo kwa kiasi fulani inafanana na hali ilivyokuwa wakati China ilipokumbwa na baa la njaa. Ndio maana China inaposema inafahamu na kuelewa uchungu wanaopata watu wa Afrika kutokana na njaa, ni uelewa unaotokana na uzoefu iliopitia, na inaposema inashirikiana na nchi za Afrika kuondokana na tatizo la njaa inasema hivyo kutokana na uzoefu iliopata katika kuondoa tatizo la njaa.
Tangu mwaka 1978 China ilipoanza kutekeleza sera ya mageuzi na kufungua mlango, sekta ya kilimo na hasa kushughulikia tatizo la ukosefu wa chakula ilipewa kipaumbele. Mageuzi yaliyofanyika kwenye sekta ya kilimo yalihusu utaratibu wa kumiliki ardhi, biashara ya mazao ya kilimo na hata faida inayotokana na mauzo ya mazao hayo. Kwa upande mwingine serikali ilifanya juhudi ya kuhimiza matumizi ya mashine, sayansi na teknolojia katika uzalishaji wa kilimo. Kwa hiyo China inaposema inafahamu changamoto ya njaa barani Afrika na inaweza kutoa mchango katika kuisaidia Afrika kuondokana na changamoto hiyo, ni kutokana na uzoefu.
Mmoja wa wachina wanaotajwa kutoa mchango mkubwa katika kuondoa uhaba wa chakula nchini China ni Bw. Yuan Longping, anayeitwa "baba wa mpunga chotara.” Baba huyu aliyekahikisha kuwa kila mchina anaweza kupata mchele wa kutosha kwa gharama nafuu, anafahamikwa kwa watu wengi duniani. Lakini sio wengi wanaofahamu kuwa mbali na dhamira yake binafsi, serikali ya China ilimpa uungaji mkono wa kila aina, ikiwa ni pamoja na fedha, maeneo ya ardhi, na hata mafunzo ili kufanikisha tafiti zake. China pia inaendelea kutoa mafunzo kwa wataalam wa Afrika, na hata kugharamia baadhi ya vituo vya mfano kwenye mambo ya kilimo.
Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China Bibi Mao Ning hivi karibuni alisema China imehakikisha usalama wa chakula kwa watu wake bilioni 1.4 baada ya juhudi za miongo kadhaa. Alisema kupitia ushirikiano na nchi za Afrika, China itazisaidia nchi za Afrika kuongeza uzalishaji wa nafaka, kuhimiza kampuni za China kuongeza uwekezaji wa kilimo Afrika, na kuimarisha ushirikiano katika teknolojia ya mbegu na maeneo mengine ya teknolojia ya kilimo, ili Afrika iweze kuondokana na tatizo la njaa kama China ilivyofanya.
China imekuwa ikitekeleza kivitendo hadi zake kwa Afrika kuhusu kukabiliana na tatizo la njaa. Tangu mwaka 2012, China imetuma zaidi ya wataalamu 400 wa kilimo barani Afrika na kutoa mafunzo kwa zaidi ya wataalamu 70,000 wa kilimo kwa bara la Afrika. China pia imetangaza mipango ya kusaidia nchi za Afrika katika kuendeleza aina bora za mazao na mbinu za kilimo, kuboresha utumiaji wa mashine na kuongeza kasi ya ongezeko la mazao makuu ya nafaka.
Katika muongo mmoja uliopita, China pia imeanzisha vituo 24 vya mfano wa teknolojia ya kilimo barani Afrika, na kuingiza mbinu mpya za kilimo zisizopungua 300, kwenye maeneo ya ushirikiano wa kilimo imeweza kusaidia kuongeza mazao ya wakulima kwa wastani wa 30 hadi 60 na kunufaisha wakulima zaidi ya milioni 1. Hadi sasa, zaidi ya makampuni 200 ya China yanaendelea kuwekeza katika sekta ya kilimo ya Afrika.