O: DHANA YA NDOA (Presumption of Marriage)
Je, Nini maana ya dhana ya ndoa?
Dhana ya Ndoa ni ile hali ambayo watu huitwa wanandoa kwa kuwa wameishi pamoja kama mume na mke kwa kipindi cha
miaka miwili na kuendelea;
Wanawake wengi wamekuwa wakiaminishwa vibaya kuwa
akikaa na mwanaume kwa miezi 6 tu basi hapo mwanamke anatambulika kama mke halali wa huyo mwanaume, jambo hili si sahihi, sababu Sheria inatambua kipindi cha miaka miwili (2) mfululizo kuishi kama mke na mume, hapo ndipo dhana ya ndoa hutambulika.
Dhana ya Ndoa humalizikaje? Je nayo huombewa talaka?
HAPANA, dhana ya ndoa huvunjwa na mahakama kwa kutolewa kwa amri ya kubatilisha dhana hiyo (
decree of annulment) na sio talaka. Talaka hutolewa kwa wanandoa rasmi tu.
Vipi kuhusu mali na mgawanyo wa watoto waliopatikana katika dhana ya ndoa?
Mgawanyo wa mali, na uangalizi wa watoto pamoja na matunzo yao hufanyika kwa kuzingatia mambo yaleyale yanayozingatiwa wakati wa utoaji wa talaka.
P: UANGALIZI WA WATOTO NA MATUNZO YAO:
Wakati wa kutoa talaka au utengano Mahakama ina uwezo wa kuamuru mtoto akae chini ya uangalizi wa baba au wa mama na ikiona mazingira hayaruhusu kwa mtoto kukaa kwa baba au mama yake mzazi, basi inaweza kuamua mtoto akakae kwa ndugu yeyote wa mtoto au kwenye kituo cha kijamii kinacholea
watoto;
Mahakama katika kuamua ukaaji wa watoto
huzingatia maslahi ya mtoto kwa kuangalia;
- Maombi ya wazazi wenyewe;
- Maombi ya mtoto ikiwa ana umri wa kuweza kujielezea;
- Mila na desturi za mahali wanapoishi wanandoa;
Mtoto wa umri chini ya miaka saba hudhaniwa kuwa ni vyema akikaa kwa mama yake, ingawa sio lazima akae huko kulingana na mazingira yatakavyokuwa;
Sambamba na hilo, mahakama itaangalia:
- Haki za kimasomo za mtoto, kama kumhamisha kutaharibu masomo yake au la;
- Itaweka utaratibu wa mzazi aliyenyimwa uangalizi kumtembelea mtoto huyo;
- kuweka zuio la mtu aliyepewa uangalizi wa mtoto kutoka naye nje ya Tanzania bila ruhusa ya mzazi mwenza na pia ya Mahakama.
Q: DHANA YA KIFO (Presumption of death):
Wakati mwingine watu hupotea na kutopatikana waliko au habari zao, jamii hufikia kuamua kuwa mtu huyo alishakufa huko alikopotelea na baadhi ya jamii hufanya ibada ya mazishi kana kwamba wana mwili wa huyo mtu (marehemu). Hii fikra ndio inayoitwa dhana ya kifo
Kisheria, mtu asipowasiliana na mtu yeyote ambaye kwa kawaida wangepaswa kuwasiliana mfano baba, mke, kaka nk kwa kipindi cha
miaka 5 na zaidi, basi
kutakuwa na dhana kuwa mtu huyo alikwishafariki dunia.
R: MAKOSA YA JINAI YAHUSIANAYO MAMBO YA NDOA
- Ukizuia isivyo kisheria kufungwa kwa ndoa ambayo wanandoa tarajiwa wamepitia hatua zote na wana sifa za kufunga ndoa, ama ukienda kufanya vituko kwenye sherehe ya harusi ya wanandoa kwa lengo la kuwadhalilisha au kuwafedhehesha unakuwa umefanya kosa la jinai na likithibitishwa unaweza kuapata adhabu ya kifungo cha miezi 3 jela.
- Kuolewa na mtu ambaye uhusiano wake umekatazwa kisheria;
S: Sheria za Kimila za mwaka 1963 – Tangazo la Serikali (GN.) Na. 279 la 1963
Hizi zilipangwa kutumika katika wilaya za Handeni, Kahama, Kondoa, Lushoto, Musoma, Ngara na Pangani –
Lakini kwa sasa zinachukuliwa kutumika kwa jamii yote Tanzania.
Vipi sasa watu wakikaa pamoja bila ndoa na kuamua kutengana kabla miaka 2 haijafika?
Ikiwa watu watakua na mahusiano ya kimapenzi yenye muelekeo wa kindoa, wakakaa pamoja na kuvunja mahusiano yao
kabla ya miaka 2 ambayo wangetambulika kuwa wanandoa ksheria (
kwa dhana ya ndoa) basi mali walizochuma pamoja hutambulika kama
mali za ushirika ( partnership properties).
Mali hizi za ushirika hugawanywa na Baraza la Kata kwa kuzingatia taratibu za kijamii za mahali husika. Kwa kuwa sheria ya kimila iliyorasimishwa ni hili
tangazo la Serikali namba 279 la 1963, basi ndio linalozingatiwa wakati wa ugawaji.
Mgao huwa ifuatavyo:
Mifugo, vyakula vilivyomo ghalani, mazao ya biashara, mazao ambayo hayajavunjwa, hugawanywa sawa sawa kwa hao watu wawili.
Nyumba hupewa mwanamume na mwanamke huchukua vyombo vya jikoni.
Baada ya mavuno, shamba huwa mali ya mume.
Kila mtu atachukua vitu vyake binafsi anavyovimiliki kama vile nguo mapambo n.k. pamoja na zawadi alizopokea toka kwa mwenziwe.
Kama mwanamke amemfuata mwanamume katika nyumba yake na wakaishi pamoja na kama wote wawili wameshirikiana kuendesha kazi hapo kwao na kupata mali, ama kama wote walikuwa na kazi rasmi, basi mwanamke ana haki ya kupata robo ya vitu vyote au mali zote zilizopatikana kwa msaada wake isipokuwa vitu vyake mwenyewe (mali binafsi)
Kama mwanaume amemfuata mwanamke katika nyumba yake na wakachuma mali pamoja, ana haki ya kupata robo ya vitu vyote vilivyopatikana kwa msaada wake isipokuwa vitu vyake binafsi.
T: MIRATHI
Hili ni somo pana ambalo litahitaji siku nyingine kulizungumza, ila hapa nitazungumza kwa ufupi sana kuhusu mirathi ya mali za marehemu kwa wajane na watoto.
Je, ikiwa anayefariki ni mume, kina nani wanastahili kuwa warithi wake?
Sheria inasema kuwa warithi ni wale watu walioandikwa katika wosia wa marehemu. Ikiwa marehemu hajaacha wosia, basi watu wa karibu ya marehemu (ndugu) wanaweza kuwa warithi wake. Watu hao ni mke, watoto, wazazi na wengine ikiwa ni pamoja na wale waliomuuguza kipindi cha mwisho cha uhai wake.
Je, ni kila mke anayeweza kurithi mali za marehemu (mume)?
Hapana. Sio kila mke atakuwa na uhalali wa kurithi mali za marehemu, bali ni mke halali tu wa marehemu ndiye atayeweza kurithi.
Ikiwa wamejitokeza wake wawili wa marehemu na wote wana vyeti vya ndoa, yupi atakuwa ni mke halali?
Ikiwa ndoa ilikuwa ni ya mke mmoja, mke aliyeolewa kwanza ndio atakua halali na ndiye atakastahili kurithi. Huyu mwingine hatahesabika kama mke wa marehemu bali kama
hawara tu. Ikiwa walichuma pamoja na marehemu basi atapata mali hizo kwa mtindo wa ushirika (
partnership) na sio kwa mtindo wa mirathi.
Je, watoto waliozaliwa hapo kwenye ndoa inayoonekana kuwa ni haramu, watahesabiwa urithi?
Kwa mujibu wa
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009 (The Law of the Child Act, CAP 13 R.E 2019) , watoto hawa wataweza
kutumia na kufurahia mali za baba yao, sheria hiyo haijawekwa wazi kama wataweza kurithi (
kumiliki) pindi baba atakapokufa. Maamuzi ya karibuni ya mahakama kuu ya Tanzania chini ya
Jaji Mlyambina yalionesha kuwa watoto hawa (
maarufu kama haramu) wanaruhusiwa kurithi mali za marehemu baba yao.
Hata hivyo maamuzi haya bado yanaendelea kufanyiwa tathmini ya kisheria kwa kuwa tayari kulikuwa na maamuzi ya Mahakama ya Rufaa ambayo yalitamka wazi kuwa mtoto wa nje ya ndoa hawezi kurithi isipokuwa tu kama baba wa mtoto huyo alimkomboa huko kwao na kumtambulisha kwenye ukoo wake kwa tamaduni za ukoo husika, na kwamba mtoto huyo alikuwa akihusika na shughuli za kijamii kwa ukoo wa baba yake.
Mahakama ya Rufaa kupitia kesi ya
VIOLET ISHENGOMA KAHANGWA AND JOVIN MUTABUZI v THE ADMINISTRATOR GENERAL AND MRS. EUDOKIA KAHANGWA 1990 TLR 72 (CA) - (KISANGA JJA, MAKAME JJA na MFALILA JJA) iliamua kuwa mtoto haramu anaishia kufurahia mali za baba yake mpaka pale baba yake atakapofariki dunia na hataweza kugusa mali hizo mara baada ya kifo cha baba yake. Wazee wa Mahaka ya Rufaa wakasema kama baba anapenda mwanae wa nje ya ndoa asisumbuliwe pindi yeye baba atakapokufa, basi amfanyie mwanae mambo yote akiwa hai, maana hakuna mtu anayeweza kumzuia baba kufanya vitu kwa mwanawe. Hukumu hiyo mpaka leo hii haijabatilishwa, hivyo ndio msimamo wa Sheria Tanzania.
Ahsanteni sana ninaishia hapa.
Ninakaribisha maoni, mjadala, maswali, ufafanuzi, nyongeza nk ruksa kuja DM na Whatsapp