Utajiri wa rafiki yangu ulivyofanya nikamuamini Shetani - 03
Nilisimama pale kando ya lile jengo la Ubungo Plaza huku nikiendelea kuwa makini sana,baada ya muda wa nusu saa kuna namba nisiyoifahamu ikanipigia.
Mimi "Hallo"
Yeye "Hallo,mambo vipi"
Mimi "poa,nani?"
Yeye " Ah mh! Wewe si ndiye mgeni wa Mzee Nicolaus?"
Mimi "Ndiyo"
Yeye "Ameniambia upo Ubungo Plaza nije nikuchukue"
Aliendelea "Umesimama eneo gani?"
Mimi "Nipo mbele ya hili jengo kaka,mbele kabisa ya mlango wa kuingia"
Yeye "Ok sasa vuka barabara uje upande wa pilipili unaiona hii gari nyeusi Prado imepaki hapa pembeni?"
Aliendelea "wewe si ndo umevaa shati la damu ya mzee na suruali ya kaki?"
Mimi "Ndiyo kaka,umeniona?"
Yeye "Nishakuona,vuka uje nakusubiri"
Nilivuka ile barabara kwa umakini mkubwa huku nikiendelea kushangaa magari namna yalivyokuwa mengi barabarani,wakati nimefika jiji la Dar es salaam hii barabara ya kutoka Manzese hakukuwa imejengwa miundombinu ya Mwendokasi,hivyo haikuwa rahisi kuivuka ile barabara kwasababu magari yalikuwa rafu sana!.Nilipofika kwenye ile gari jamaa aliyonielekeza niliisogelea kisha nikamgongea kioo akawa amekishusha.
Jamaa "Shwari?"
Mimi "Swari kaka"
Jamaa "Ok Ingia twende"
Nilipanda kwenye ile gari nikaa mbele ili iwe rahisi kuyatazama maeneo ya jiji kwa uzuri zaidi.Wakati tupo kwenye gari hatukuwa na stori sana kwasababu jamaa muda wote alikuwa akiongea na simu.
Baada ya dakika kadhaa tukawa tumefika kwenye nyumba nzuri mno iliyokuwa na geti,ndipo jamaa alipiga honi akawa amefunguliwa geti,baada ya mimi kutelemka jamaa aliondoka na ile gari.Kiukweli ile nyumba ilikuwa nzuri sana na nilipokuwa mwenyeji ndipo niligundua Anko Nico alikuwa akiishi eneo la Ununio -Bahari beach.
Historia fupi ya Anko Nico.
Kiukweli mimi tangu nimekuwa,wajomba zangu nimekuwa nikiwaona Tarime wakiwa wamepita kumsalimia dada yao(Mama yangu),sikuwahi kuzifahamu familia zao na hata makao yao,na mara zote wakati wanapita hapo Tarime huwa wanakuja wenyewe.Hivyo ilikuwa tu ni eidha mama atuambie kuna mjomba wako anaishi sehemu fulani na mwingine yupo sehemu fulani.
Kaka zake mama ambao ni wajomba zangu,wapo wanne(4),Mmoja yupo Serengeti ni muajiliwa wa Tanapa,Mwingine ni Mwanajeshi aliwahi kuwa hapo Lugalo lakini sikuhizi amehamishiwa Kigoma,mwingine anaishj na familia yake huko Botswana,na mwingine ndiye huyu ambaye nilikuwa kwake,kwa bahati nzuri wote nimewahi kuwaona ila sikuwahi kuishi nao.
Kumekuwa na sintofahamu mara zote katika familia mbili na huwa sifahamu shida ni nini,kwa upande wa kina Baba nilikuwaga nikizingua au kufanya kosa lolote,wakati baba akiniadhibu alikuwa akiniambia nimechukua akili za kipumbavu za ujombani,vilevile mama nae alikuwa akisema upande wa kina baba wana roho mbaya na tabia za kipumbavu,sasa sikuwahi kufahamu ni kitu gani kilikuwa kinaendelea kati ya familia hizi mbili.
Anko nico alikuwa ni Contractor na Mkewe hadi leo ninapoandika yupo anafanya kazi wizara ya Afya,Anko Nico kwasasa ni marehemu,hivyo mkewe ndiyo kila kitu kwenye familia yake kwasasa.
Nimeona nitoe historia fupi kidogo ili huko mbele maswali yapungue.
Basi baada ya kuachwa pale ndani ya fensi kulikuwa na ukimya wa ajabu,ni ndege tu ambao nilisikia wanalia kwenye miti,kiukweli mazingira yale ungedhani wanakaa mawaziri au viongozi wenye vyeo vikubwa serikalini kwasababu kulikuwa kuzuri na kutulivu mno!.Baada ya muda nikiwa nashangaa,mlango ulifunguliwa akawa ametoka nje binti mmoja aliyekuwa amevalia mavazi ya jikoni(Yale mavazi yanavaliwa na wapishi wakiwa jikoni wanapika).
Yule binti "Karibu"
Mimi " Ahsante"
Yule binti "Unaitwa nani?"
Mimi "Umughaka"
Yule binti "Kumbe ndiyo wewe!"
Tulipofika ndani nikaa kwenye kochi nikawa nashangaa namna watu walivyokuwa wakiishi,wakati naendelea kushangaa mara simu ya mezani ikawa inaita,yule binti akawa amekuja kuipokea.
Yule binti " Eeh amefika baba"
Aliendelea "sawa baba"
Baada ya yale maongezi yule binti akawa ameikata ile simu na kuondoka kwenda kuendelea na alichokuwa anakifanya.
Yule binti alipoivishwa chakula kilitengwa na kunitaka niende nikajisevie,nilinyanyuka zangu nikaenda kupakua msosi na kuanza kula,nilipomaliza kula yule binti alinionyesha chumba ambacho nilipaswa kwenda kuoga na ndipo ningelala kwa siku hiyo,sasa nilipofungua na kuingia ndani nilimkuta mzee mmoja akiwa amelala huku ikionekana kabisa afya yake imedhoofika kwasababu nilikuta amewekewa mpira wa kukojolea,yaonyesha hata kokojoa mwenyewe tu alikuwa hawezi.
Nilipoufungua ule mlango na kuingia ndani akawa ameshituka na kugeuka kwa shida kunitazama.
Mimi "Shikamoo"
Mzee "Marhaba"
Baada ya salamu sikuwa na stori zaidi ya kuendelea kumshangaa mzee huku na yeye akinitazama kwa umakini.Kwakuwa alikuwa amewekewa mpira wa kukojolea nilifahamu kabisa ni mgonjwa na hivyo ikabidi nimpe Pole.
Mimi "Pole sana mzee wangu"
Mzee "Pole ya nini mwanangu!"
Mimi "kwa maumivu mzee"
Mzee "Aaah haya nilishayazoea muda tu"
Aliendelea "wewe ni nani?"
Mimi "Mimi naitwa Umughaka,Nicolaus ni mjomba wangu"
Mzee "Oooh sawa"
Kwa namna mzee alivyokuwa akiongea alionyesha kabisa ni mtu kutokea pande za kaskazini mwa nchi yetu.
Nilivua nguo nikawa nimeingia bafuni kuoga,sasa wakati nikiwa bafuni nikawa nasikia simu yangu inaita mpaka ikakata,nilipomaliza kuoga moja kwa moja nilienda kuitazama na ndipo nikakuta ni mtoto wa baba mkubwa Kileri alikuwa akinipigia.Nilibadili nguo kisha nikampigia.
Kileri "Mwanangu nisamehe sana,uko wapi?"
Mimi "Nipo kwa Anko Nico"
Kileri "Maeneo gani kaka nije kukuchukua"
Mimi "Usijali niko salama kabisa kaka,nadhani nikitoka huku nitakufahamisha"
Kileri "Daaah nisamehe sana kaka,simu yangu huwa inasumbua betri,jana ilizima"
Mimi "Ungetumia hata simu ya mtu kaka"
Kileri "Tatizo namba yako sijaikariri kaka!"
Mimi "Usijali kaka hakuna kilichoharibika"
Kileri "Poa mwanangu lakini hakikisha huchelewi ili tupambane"
Mimi "Nikitoka huku nitakushitua"
Baada ya yale maongezi na kileri nilitoka mle chumbani nikarudi zangu sebuleni.Nilikaa pale sebuleni huku nikiendelea kutazama luninga,mida ya saa 9 alasiri kuna mabinti wawili waliingia ndani,mmoja akiwa mkubwa na mwingine mdogo,japo kuwa wote walikuwa na miaka zaidi ya 18 lakini kuna mmoja alikuwa mkubwa kuliko mwenzie,wale mabinti walikuwa watoto wa mjomba Niko na kiukweli sikuwahi kuwafahamu na wao walikuwa hawanijui,waliniangalia na mmoja akanisalimia ila mmoja alikula buyu na kuzama ndani!.
Ilipofika mida ya saa 1 usiku,kuna gari iliingia ndani ya fensi ya ile nyumba na haukupita muda akawa ameingia ndani mke wa Anko Nico ambaye nimewahi kumuona mara moja tu pale Tarime wakiwa wamekuja mmewe kumsalimia mama.
Mke wa Anko "Habari ya siku"
Mimi "Nzuri,shikamoo"
Mke wa anko "Marhaba"
Aliendelea "Tarime wazima?"
Mimi "Wazima kabisa"
Mke wa anko "Wifi yupo?"
Mimi "Yupo mzima kabisa"
Mke wa anko "Karibu"
Baada ya salamu yule mke wa anko alizama ndani kwake huko.Ile familia ilikuwa ni familia ambayo ilikuwa haijali kabisa na kila mmoja alijali mambo yake.
Ilipofika mida ya saa 2 mjomba nae akawa amefika.Tuliongea mambo mengi sana na Anko Nico na alitaka kufahamu nimekuja Dar es salaam kufanya shughuli gani kwasababu aliniambia huu mji bila kuwa na kazi ni vema ningerudi Tarime kuliko kudhani kungekuwa na mteremko wa maisha mazuri.Baada ya kumwambia kilichokuwa kimenileta alielewa na akawa kimya.
Maisha ya hapo nyumbani kwa Anko yaliendelea kama kawaida na sasa nikaambiwa niwe namuangalia yule mzee na kumbadilishia mpira,kumuogesha na hata kwenda chooni nihakikishe niwe namtazama,ingawa alikuwa akijiweza kwa kujikokota lakini alihitaji uangalizi,sasa kumbe yule mzee alikuwa ni baba yake na mke wa mjomba Nico.
Niliona nikiondoka pale kwa Anko na kwenda kwa Kileri nitakuwa kama nimewadharau na niliona naweza kupata tatizo halafu ikala kwangu kwasababu ya kuondoka kwa ujuaji,nilisubiri Anko aniambie sasa ni muda wa kuondoka nikaendelee na shughuli zangu baada ya kunifadhili kwa makazi kwa muda.
Kwakuwa muda na siku zilikuwa zimekwenda,Kileri aliniambia kama inawezekana nimuelekeze maeneo nilipokuwa aje achukue ile hela ili akanunue mzigo wa kutosha aongeze kwenye duka kama tulivyokuwa tumekubaliana ili biashara iendelee kufanyika,sikuwa kabisa na shaka kwasababu niliamini ni mtoto wa baba yangu mkubwa na kwetu anafahamika na mimi kwao nafahamika,hivyo niliona ni vema nimwambie aje mpaka Ununio kuchukua ile hela akaendelee kufanya biashara na faida tuwe tunagawana.
Mipango yote ya ufanyaji wa biashara na upatikanaji wa faida tulikuwa tumeisuka tangu nikiwa Tarime,basi jamaa alikuja nikawa nimempatia ile yote milioni 9 akawa ameondoka.
Maisha yalisonga na jamaa akawa ananipa mrejesho kuhusu biashara na kiukweli kwa mujibu wa maelezo yake ilikuwa inachanganya vibaya hivyo sikuwa na shaka.
Pale kwa Anko walikuwa wakiondoka asubuhi nilikuwa ninabaki mimi na yule binti wa kazi huku mimi nikiendelea kumuangalia yule mzee na kuwa kama mtu wa usafi nje ya nyumba.Kadiri siku zilivyokuwa zinasonga ndipo na mambo yalianza kubadilika,kuna siku nilikuwa nikimsalimia mke wa anko anajifanya hajasikia salamu anasepa,nilidhani uenda ilikuwa ni kawaida kwa mtu mzima kuwa na mawazo kumbe haikuwa kama nilivyodhani.
Kuna siku aliporudi kutoka kazini kwake nikawa nasikia anamgombeza sana mjomba huko chumbani kwao na sikufahamu ni kitu gani kilikuwa kikiendelea.
Itaendelea....