Utii Ulikuwa Njia ya Kuishi, Mpaka Pale Alipokua C.E.O Kisha Kuua Kampuni - Biograph ya Tedi

Utii Ulikuwa Njia ya Kuishi, Mpaka Pale Alipokua C.E.O Kisha Kuua Kampuni - Biograph ya Tedi

Camo

Member
Joined
Jul 15, 2025
Posts
14
Reaction score
70
Alizaliwa kwenye familia ambayo haikuamini katika mazungumzo, haikuamini katika kuelewana, haikuamini katika maoni mbadala. Bali heshima ni utii usiohoji, na upendo ni zawadi inayotolewa tu kwa wale wanaofuata mstari. Baba alikuwa mwepesi wa hasira, mzito wa kusikiliza. Kosa dogo lilimaanisha viboko, na kosa kubwa lilimaanisha kufukuzwa ndani ya nyumba. Hakuulizwa kwa nini alikuwa amekosea, bali alielezwa kuwa yeye ni kosa. Hapo ndipo roho yake ilipoanza kujifunga. Alijifunza kuwa sauti yake haina nafasi, na hivyo akaanza kuwaza kimya kimya, kuhisi kimya kimya, na kuishi kwa tahadhari.Mazingira haya hayakumfundisha Tedi kufikiri – yalimfundisha kutii ili asiadhibiwe.

Nje ya mlango wa nyumba yao, hali haikuwa tofauti. Mtaa wao uliendeshwa na hofu isiyoandikwa. Hakuwezi kusemwa kwa sauti kubwa kwamba mtu fulani anafanya vibaya – hata kama ni kweli. Kulikuwa na vijana waliotawala barabara na mitaa, lakini mmoja kati yao, anayejulikana kama "Bingo", ndiye aliyekuwa na nguvu ya kweli. Alikuwa mtu wa maamuzi ya haraka, asiyeulizwa maswali. Hakutisha kwa silaha, bali kwa sifa ya kufuatwa na kila mmoja. Bingo alikuwa kipimo cha usikivu: usimpinge, usimuulize, usimtazame kwa shaka. Na Tedi, akiwa mdogo aliyejaa kiu ya uelewa, alinyamazishwa kabla hajakomaa. Alijifunza kuwa kutosikika ni usalama.

Shuleni, mazingira yalizidi kuimarisha itikadi hiyo. Walimu walikuwa wakaguzi wa utiifu, si waelimishaji. Hakukuwa na nafasi ya kuuliza maswali yenye changamoto. Mwanafunzi aliyesema “Lakini mwalimu, si inawezekana...?” alikatishwa, kubezwa, na mara nyingine kupewa adhabu ya mfano. Elimu ilikuwa zoezi la kukariri, si kufikiri. Tedi alifaulu mitihani yote lakini hakuwahi kujifunza jinsi ya kuheshimu mtazamo wa mtu mwingine. Shule ilimwandaa kupita kwenye mfumo, si kuubadili. Alijifunza ukimya wa kusalimika.

Kazi ya kwanza ilikuwa ya chini – msaidizi ofisini. Lakini hata hapo, mazingira yalikuwa yale yale: hakuna nafasi ya kupendekeza mabadiliko. Kiongozi wa idara alikuwa kama mfalme, na wafanyakazi wengine walikuwa watumwa wa saa na taratibu zisizopingika. Tedi, akiwa ameumbwa na kulelewa katika hewa ya kukosa uvumilivu, aliona hilo kama kawaida. Hakuwahi kuuliza kwa nini wengine wanaonewa – alijifunza kuwa huo ndio mchezo wa kusonga mbele. Na alipoanza kupanda cheo, alibeba mtazamo huo kama silaha. Si kwa sababu alitaka kuwa mbaya, bali kwa sababu alifundishwa kuwa huo ndio uongozi.

Baada ya miaka kadhaa, aliteuliwa kuwa Mkurugenzi Mtendaji(C.E.O) wa kampuni kubwa. Ofisi yake ilikuwa ya kisasa, lakini akili yake ilibeba kale ka-usimba ka kale. Kila alipoona mfanyakazi mwenye mawazo tofauti, alihisi ni tishio. Aliamini kiongozi mzuri ni yule anayejenga utii wa kipofu, si kushirikiana katika hoja. Mara kwa mara, wafanyakazi waliotoa pendekezo lililopingana na lake waliondolewa kwenye nafasi walizokuwa nazo. Wengine waliondolewa kimyakimya – kwa barua ya kushushwa cheo au kutoongezewa mkataba. Aliunda timu ya watu waliokubaliana naye tu – si kwa sababu walikuwa sahihi, bali kwa sababu walikuwa wapole kimawazo.

Hali ya kazi ikawa kama vazi la kijeshi – kila mtu aliingia kwa tahadhari, aliongea kwa hofu, na alitoka kwa ahueni. Na Tedi aliendelea kuamini kuwa hiyo ni nidhamu. Hakuona kuwa anaua ubunifu. Hakuona kuwa anapunguza ufanisi. Alidhani kimya ni ishara ya mafanikio. Hakujua kuwa kimya kinaweza kuwa kilio cha hofu kisicho na sauti. Kampuni ikaanza kudumaa, mawazo mapya yakapotea, watu wenye vipaji wakakimbilia mashirika mengine.

Lakini tatizo halikuwa cheo cha Tedi. Tatizo halikuwa kampuni. Tatizo lilianzia pale alipokuwa mtoto – pale alipoambiwa kuwa tofauti ni kosa, kuuliza ni dhambi, kupinga ni uasi. Alijengwa kuwa mzalishaji wa utii, si mzalishaji wa fikra. Na hivyo, alipofikia nafasi ya juu, alikuja na marundo ya hofu yaliyovaa suti nzuri.

Na hii ndiyo sumu ya kutokuvumilia(Ideological tolerance): hujificha kwenye maadili, lakini ndani yake kuna uoga wa kutoeleweka. Hujificha kwenye nidhamu, lakini ndani kuna jeraha la kuamini kuwa maoni ya wengine ni hatari. Hujenga viongozi waliojeruhiwa, wanaojeruhi wengine kwa jina la ufanisi.

Uvumilivu si udhaifu. Ni ujasiri wa kusikiliza kile ambacho hujakizoea. Na bila ujasiri huo, kila mafanikio hutawaliwa na hofu – hofu ya kupingwa, hofu ya kusahihishwa, hofu ya kupoteza udhibiti. Ambapo mwisho wake ni upweke wa mamlaka na kushuka kwa ubora.
 
Back
Top Bottom