Katika kipindi cha miaka 10 iliyopita, China imehimiza uwekezaji katika nchi mbalimbali za Afrika unaolenga kutatua moja kwa moja changamoto zinazowakabili watu wa Afrika. Kupitia kauli mbiu yake ya “kujenga jumuiya ya binadamu yenye hatma ya pamoja”, China imeweza kuanzisha programu na miradi mbalimbali yenye thamani ya mabilioni ya dola za kimarekani ambayo imekuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa watu wa kawaida, makampuni na hata serikali za nchi za Afrika.
Uwekezaji wa China barani katika kipindi cha miaka 10 iliyopita umekuwa na mafanikio kutokana na uratibu makini wa serikali za pande mbili. Upande wa China umeweka program mbalimbali za uwekezaji zinazoweza kutumiwa na nchi za Afrika, na nchi za Afrika zinaangalia zinaweza kupata nini cha kuhimiza maendeleo katika nchi zao kupitia miradi hiyo.
Mwaka 2014 Benki Kuu ya China (PBOC) kwa kushirikiana na Benki ya maendeleo ya Afrika (AfDB) waluianzisha mfuko wa pamoja wenye thamani ya dola za kimarekani Bilioni 2, ulioitwa Africa Growing Together Fund (AGTF). Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka jana mfuko huo ulikuwa umetumia zaidi dola bilioni 1 katika kutekeleza miradi 36. Miradi hiyo iko kwenye nchi 19 za Afrika ikiwa ni pamoja na Tanzania, Kenya, Zambia na Tunisia, ikihusisha sekta za kilimo, usafirishaji, uzalishaji wa umeme, mifumo wa usambazaji wa maji na kushughulikia maji taka.
Mfuko mwingine ambao umetoa mchango mkubwa kwenye maendeleo ya Afrika ni mfuko wa China-Africa Development Fund (CAD-Fund) wenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 10. Hadi kufikia mwezi Juni 2021, mfuko huo ulikuwa umewekeza zaidi ya dola za kimarekani bilioni 5 kwenye nchi 37 barani Afrika, na kuhimiza uwekezaji wenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 26 kutoka kwa makampuni ya China kwenye nchi hizo, na kuongeza nafasi za ajira laki 2.7 zikiwa ni za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja.
Kupitia mifuko hiyo, nchi za Afrika zinaweza kuwasilisha miradi zinayoona inafaa kwa ushirikiano na kuijadili na upande wa China. Endapo miradi hiyo inakuwa na tija na maslahi mapana kwa nchi za Afrika, basi pande mbili zinapanga na,mna ya kutekeleza miradi hiyo.
Jambo la kutia moyo zaidi katika kipindi hicho cha miaka 10, ni kwamba China imetambua kuwa sekta ya kilimo, ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi kwenye nchi nyingi za Afrika inatakiwa kupewa umuhimu katika ushirikiano. Pamoja na kuwa si lazima kuwa sekta hiyo ndio imekuwa ikiingiza mapato mengi kwa nchi za Afrika, ukweli ni kwamba ni sekta ambayo imewaajiri watu wengi na ina uhusiano wa moja kwa moja na watu wengi wa Afrika. Kwa hiyo ni ukweli usiofichika kuwa kuhimiza maendeleo ya sekta ya kilimo katika nchi nyingi za Afrika, ni kugusa moja kwa moja maisha ya watu wa kawaida. Kuanzia mwaka 2012 China imetoa msukumo mkubwa kwenye eneo hilo, na hadi sasa ushirikiano kwenye sekta ya kilimo umekuwa na maendeleo ya kasi.
Kupitia miradi mbalimbali ya kutoa mafunzo, China imetoa mafunzo kwa wataalam wa kilimo zaidi ya elfu 50 wa Afrika, ikiwa ni pamoja na karibu 7,500 waliopata mafunzo nchini China. Pia kumekuwa na mradi wa vituo 23 vya mfano kuhusu kilimo. Mwaka 2019 mkutano wa kwanza wa ushirikiano wa kilimo kati ya China na Afrika ulifanyika mjini Sanya, na kuandaa mpango wa utekelezaji wa kufanya sekta ya kilimo iwe ya kisasa. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2020, makampuni ya China yalikuwa yamewekeza zaidi ya dola bilioni 1 kwenye sekta ya kilimo kwenye nchi 35.
Katika miaka miwili mitatu iliyopita kumekuwa na matokeo mazuri kwenye ushirikiano kwenye sekta ya kilimo. Kupitia ushirikiano kati ya makampuni binafsi ya China na Afrika, bidhaa za kilimo kutoka nchi za Afrika zimekuwa zikiingia kwenye soko la China, hatua ambayo sio kama tu inachangia kutatua tatizo la ukosefu wa soko kwa bidhaa za kilimo kwa Afrika, bali pia kuziingizia mapato ya fedha za kigeni nchi za Afrika.