JE, UZALENDO NI NINI NA NI WAKATI GANI HASA MTU UNATAKIWA KUONYESHA UZALENDO WAKO KWA VITENDO?
Ndugu wanajukwaa poleni kwa kwa kazi ya kuijenga Tanzania yetu. Kama kichwa cha habari kilivyo hapo juu, kipo kwa mtindo wa swali naomba mnisaidie kunipa ufafanuzi wake.
Mara kwa mara nikipitia post mbalimbali humu jukwaani, na mijadala mbalimbali kwenye media zetu na hata vijiweni watu wamekuwa wakijinasibu kuwa wao ni wazalendo, au kuwaelezea watu wengine ambao ni wa kundi lao kuwa ni wazalendo wa kweli.
Akitokea mtu akawa hakubaliani na tafasiri yao kuhusu uzalendo au kutokubaliana nao juu ya uzalendo wao au wa watu wao basi mtu huyo anaweza kubatizwa majina ya msaliti, na au kibaraka wa Mabeberu.
Wanajukwaa naomba mnisaidie ufafanuzi kama maswali ya kichwa cha habari yanavyouliza. Ili uweze ku-qualify kuwa mzalendo unatakiwa kufanyaje? Na ni wakati gani hasa unatakiwa ku-practice huo uzalendo?
Kwa mfano watu wengi wamekuwa wakimwelezea Hayati kuwa alikuwa Mzalendo namba 1. Wakitolea mfano jinsi alivyojitoa katika kulinda raslimali za nchi ili ziwanufaishe Watanzania.
Pia, katika kuuthibitisha uzalendo wake alihakikisha hatumii madaraka yake kujinufaisha binafsi bali aliwaletea maendeleo watanzania katika kuboresha miundo mbinu na huduma za kijamii ikiwemo kutoa elimu bure kwa watoto wa wanyonge.
Wakati huo wanapotokea watu wengine kuelezea negativity za Hayati, kama kutokuheshimu katiba, kubomoa demokrasi, kuharibu diplomasia, kuharibu uchumi kwa kuwavuruga wafanyabiashara na badala yake kuwa entertain wamachinga, kufumbia macho vitendo vinavyokiuka haki za binadamu, kama watu kutekwa, kupotea kuuawa, kupigwa risai na zaidi walengwa wakiwa ni wakosoaji wake na serikali yake.
Hao wanaambiwa sio wazalendo. Sasa naomba mnisaidie uzalendo ni nini, na ili uitwe mzalendo unatakiwa ufanye nini?
WAKATI GANI NDIO MUAFAKA WA KUONYESHA UZALENDO WAKO?
Je inawezekana kuwa mzalendo ukiwa ni raia wa kawaida au hata kama upo kwenye wadhifa mdogo ambao haukupi nafasi ya kufanya maamuzi yoyote kwa ajili ya nchi yako?
Najaribu kuuliza swali hili japo linaweza kuonekana la kijinga hii ni kutokana na historia ya Hayati. Akiwa mtumishi wa serikali tena kwenye ngazi ya uwaziri kwa takribani miaka 20, ukiachana na bidii ya kazi aliyokuwa nayo, lakini hakuwahi kuuonyesha uzalendo wake waziwazi kwa kukemea vitendo vya ubahilifu, rushwa na ufisadi kufuatia kashfa mbalimbali zilizokuwa zimetokea kipindi cha uongozi wa Rais Mkapa na Kikwete.
Tofauti na ilivyokuwa kwa akina Dr. Slaa, Zito Kabwe, Kafulila, Selelii, Lembeni, Sendeka, Mwakyembe, Lissu, Mnyika, Filikunjombe, Mpina na wengine wengi, Hayati hakuwahi kufumbua kinywa chake kukemea hivyo vitendo.
Kuna baadhi ya watetezi wake wanasema kama angethubutu kufanya hivyo asingeweza kupata nafasi ya kuwa mgombea na hatimae rais. Sasa swali ni je ili kuwa Mzalendo unatakiwa usubiri mpaka uwe rais? Kama jibu ni ndio je hawa wengine wote wanaojiita Wazalendo wakati kumbe uzalendo ni wa rais peke yake wanapata wapi huo ujasiri wa kujiita wazalendo?
Na uzalendo ni sifa anayoweza kuwa nayo mtu yeyote, kwanini basi Hayati alizinyamazia kimya kashfa zile za akina Kagoda, Tegeta Escrow, Richmond nk?