Miaka ya hivi karibuni mimi na familia yangu tulihamia katika nyumba mpya. Tulipohamia hatukuweza kuchagua nani wawe majirani zetu. Tulijikuta tumezungukwa na watu waliokuwa wakiishi katika sehemu hiyo tangu zamani.
Upande wa kulia kulikuwa na jirani Heri Hamisi na mkewe Fatma Hamza.
Hamis alikuwa mtu wa makamo anayetegemea biashara ya kuuza samaki kwa ajili ya riziki yake. Alikuwa na mke mkarimu ambaye mara kwa mara alikuwa akifika nyumbani kwetu na kuongea na sisi kuhusu maendeleo ya kijiji chetu.
Watoto wao, Neema na Pendo walikuwa wema kama wazazi wao. Pia, walikuwa wanakuja kwetu kucheza na watoto wetu kwa furaha na ucheshi.
Mkono wa kushoto jirani yetu Samsoni Mawazo alikuwa akiuza mkaa. Wakati wote alikuwa akionekana mwenye jambo akiliwaza. Alikuwa na mke mpole aliyependa kushirikiana na wenzake ingawa mara kwa mara alikuwa akikaripiwa na mumewe kwa tabia hii.
Hivyo, hakuendelea nayo. Mawazo alikuwa akienda kilabuni kila siku baada ya kufunga duka lake la mkaa. Huko alikuwa akikaa na kurejea nyumbani usiku mkubwa akiwa amelewa. Anapofika hufungua redio yake kwa sauti kubwa iliyokuwa ikisumbua majirani na kuwafanya usingizi ukatike. Siyo hivyo tu mara alimpiga mkewe na kuwafanya watoto walie kwa kelele ili kumzuia asiendelee kumpiga mama yao. Majirani tulipoingilia kati kumuonya asimpige mkewe alikuwa akidai kuwa hicho alichokuwa akifanya ni elimu ya watu wazima.
Ingawa Mawazo alikuwa akipata fedha za kutosha kutokana na biashara yake ya jumla ya mkaa, hakuwanunulia mkewe na watoto nguo nzuri wala kuwapatia chakula kizuri na cha kutosha. Mama na watoto hawakuwa na maisha ya furaha. Wala Mawazo hakuwa akimruhusu mkewe na watoto wake kwenda kwa jirani yeyote.
Tunapolinganisha familia hizi mbili tunapata mawazo gani kuhusu familia yenye furaha. Hapana shaka wote tunakubaliana kuwa katika nyumba ya pili wanafamilia hawakuwa na maisha ya furaha. Lakini tunapotafakari kwa kina hali ya familia ya Mawazo tumegundua ni kitu kinachoingia haraka katika mawazo yetu hata bila kufikiria. Ni mwenendo wa Mawazo.
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.