Ewe mfanyakazi wa sasa ambaye ni mstaafu wa kesho, umepanga kufanya nini baada ya kufikia ukomo wako wa kuajiriwa?
Ni swali ambalo kila mmoja anatakiwa kulitafakari, kwani ajira uliyonayo siyo ya milele bali ni wajibu wa kipindi kifupi na baada ya muda huo, wale waliokuajiri watakupa mkono wa kwa heri, huku kibindoni ukipewa furushi la fedha ambalo katu halina ‘maisha marefu’.
Rais Jakaya Mrisho Kikwete baada ya kustaafu, alikwenda kuendelea na kilimo cha mananasi na ufugaji wa ng’ombe kijijini kwake Msoga.
Siyo huyo tu, hata Rais wa Uruguay, Jose Mujica anayetajwa kuwa ni rais maskini kuliko wote duniani, pindi alipostaafu alikwenda kuendelea na kilimo katika shamba lake la maua.