Kuna mambo mengi ambayo Donald Trump aliahidi kuyatekeleza pale aliposhika madaraka kuwa Rais wa 45 wa Marekani Januari 20 mwaka jana. Pia kuna mengi ambayo hajaahidi kuyafanya.
Alitoa mamia ya ahadi za muhimu na mengine yasiyokuwa na umuhimu sana. Kwa mfano, kwamba ataliongeza jeshi la wanamaji la Marekani kwa kulipatia manuwari dazeni moja zaidi; kwamba ataupiga jeki uchimbaji wa makaa katika nchi hiyo; na kwamba Ikulu ya Marekani itarejea kutuma kadi za Rais na mkewe kuwatakia watu “Krismasi ya Furaha”, tofauti na mtangulizi wake, Barack Obama aliyeandika tu, “Siku ya Furaha ya Sherehe.”
Kati ya ahadi nne kubwa ambazo Trump alizitaja wakati wa kampeni, tatu hazijatimizwa hadi sasa. Ni moja tu kati ya hizo aliyoitimiza. Muda mfupi kabla ya Krismasi iliyopita Bunge huko Washington lilipitisha sheria ya Marekebisho ya Kodi iliyoingiza pia fikra za wabunge wa chama chake cha Republican: Kupunguza kodi kwa matajiri na wafanyabiashara.
Tangazo la kampuni ya Apple kwamba faida inayopatikana katika biashara yake nje ya Marekani sasa itatozwa tena kodi nchini Marekani, inaonyesha kwamba Trump anaweza kutamba sasa kwamba amepata mafanikio. Lakini kwa mambo mengine matatu yaliyobaki ameshindwa vibaya.
Jaribio la Trump kutaka kuifutilia mbali ile sheria aliyoichukia ya Marekebisho ya Bima ya Afya, na ambayo ilipitishwa na mtangulizi wake, Obama, lilishindwa vibaya. Mara tatu Bunge limeyakataa mapendekezo ya Trump, mara tatu hakujapatikana wingi bungeni wa kumuunga mkono.
Ule mpango wa Trump wa kutaka kujengwa ukuta baina ya nchi yake na Mexico ambao utazuia mmiminiko wa wakimbizi haramu kutokea nchi za Amerika ya Kusini kwendea Marekani haujatekelezwa. Mazungumzo hivi sasa yamepungua kusikika kuhusu ujenzi wa ukuta huo ambao umekisiwa ungegharimu dola bilioni 20.
Pia ule mpango mkubwa wa miundombinu ambao utagharimu zaidi ya dola bilioni 1,000 kujengea barabara, madaraja na njia za reli bado hata hauko makaratasini. Inasemekana mwisho wa Februari kutatolewa mapendekezo ya mwanzo. Lakini takwimu juu ya mradi huo zimetajwa bila chochote kuonekana kikifanyika.
Na ilivyokuwa wabunge wa Democratic – ambao kura zao zinahitajiwa na Trump hawatarajiwi kutoa ushirika katika mwaka huu wa 2018 wa uchaguzi wa Bunge, hakuna tamaa kw mpango huo kupitishwa.
Licha ya uhodari wake wa kupinduapindua maneno ulioonekana wakati wa kampeni ya uchaguzi na pia baadaye, Trump amedhihirisha kwamba anautambua ukweli ulivyo kuhusu mambo mengi.
Trump aliahidi atailazimisha Mexico ilipie kujengwa ukuta mkubwa baina ya nchi hizo mbili. Kwa hilo, Trump sasa amenyamaza kimya. Amefumba mdomo. Hasikiki juu ya jambo hilo. “Yote ni upuuzi”, Trump alimhakikishia Rais mwenzake wa Mexico katika mazungumzo yao ya siri ya simu yaliyofanywa siku chache baada ya kuingia madarakani huko Washington. Mazungumzo ya viongozi hao wawili yaliibuka na kujulikana hadharani katika majira ya kiangazi ya mwaka jana.
Pia Trump aliahidi kwa nguvu wakati wa kampeni ya uchaguzi kwamba ataitaja rasmi China kuwa ni nchi inayofanya hadaa kuhusu viwango vya kubadilisha sarafu ya nchi hiyo na zile za nchi nyingine.
Ilani ya Uchaguzi ya Trump ilikuwa na kichwa cha maneno kilichoandikwa “Ifanye Marekani iwe tena Taifa Kubwa.” Mwezi Aprili mwaka jana, Trump katika mahojiano na gazeti la Wall Street Journal, alikiri kuwa “China haifanyi ujanja wala hadaa katika viwango vya kubadilisha sarafu yake na sarafu za nchi nyingine.” Hayo ni mabadiliko ya kauli ya awali.
Hivi sasa kura za maoni hazionyeshi kwamba ni nzuri kwa upande wa Trump. Karibu katika makundi yote ya wakazi wa Marekani ambao kura zao zilimsaidia aingie Ikulu, idadi yao sasa imepungua – hawa ni Wakristo wa madhehebu ya Protestanti, wastaafu na Wamarekani weupe, na hasa ambao hawajamaliza masomo ya chuo.Hao, ni wapiga kura wasiokuwa washabiki wa Trump.
Lakini ni katika hesabu ya wapiga kura wanaoyumbayumba, leo wako upande huu na kesho upande ule na huenda katika miezi ijayo wanaweza kurejea katika kambi ya Trump, pale, kwa mfano, Marekebisho ya Sheria ya Kodi yatakapoonyesha athari nzuri.
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.