UKUMBUKWE KWA LIPI? Takribani miaka mia moja iliyopita, mtu mmoja alikuwa akisoma gazeti litokalo kila asubuhi. Kwa mshangao na wahka mkubwa, aliona kwenye gazeti hilo, jina lake likiwa limechapishwa katika safu ya Tanzia. (Tanzia ni wasifu wa mtu aliyekufa). Gazeti hilo la kila asubuhi, lilichapisha taarifa ya kifo cha mtu mwingine, huku jina la mtu huyo likichapishwa kimakosa. Awali, alipatwa na mshituko mkubwa; akijiuliza, hivi nimekufa kweli, au? Na aliporejewa na utulivu wa nafsi, fikara ya pili ikawa ni kuona namna alivyozungumziwa na watu waluoamini kuwa amekufa kweli. . Tanzia katika gazeti hilo ilisomeka kama hivi: "Mfalme wa milipuko afariki dunia.", huku sehemu nyingine ikisomeka, "Alikuwa ni mfanyabiashara wa kifo!". Kimsingi, mtu huyu alikuwa ni mvumbuzi na muuzaji mkubwa wa milipuko (Mabomu), ambayo hutumiwa kupigania sehemu mbalimbali duniani na kupelekea vifo. Kwa hivi, alipoyasoma maandishi "Mfanyabiashara wa kifo" alitahayari na kujiuliza, "Je, hivi ndivyo nitakumbukwa pindi nitakapokufa kiukweli?". . Baada ya kichwa chake kutaabishwa na fikra juu ya kadhia hiyo, mwishowe alihitimisha mjadala kwamba, hiyo haikuwa njia bora ya kukumbukwa na jamii. Basi tangu siku hiyo, alijitanibu na biashara hiyo, huku akipambana kwa jino na ukucha kuitangaza amani, kwa kauli na vitendo. Mtu huyu aliitwa Alfred Nobel, ambaye leo hii, dunia inamkumbuka kwa ile tuzo kubwa na mashuhuri duniani ya amani ya Nobel (Nobel Prize). . Kama ambavyo Alfred Nobel, baada ya kubahatika kuona utajo mbaya wa jina lake ukisababishwa na mambo afanyayo maisha ni, akajutia na kuazimu kubadilika kabisa na hatimaye kuacha alama na heshima kubwa duniani, nasi tufanye kama yeye. Tusingoje bahati ya kusikia watakavyo tuzungumza jamaa zetu baada ya kutawafu kwetu, bali tujiandae sasa. . Ukifa utaacha hisia gani? Utakumbukwa kwa lipi? Ni upi utakuwa utajo wako? Utakumbukwa kwa upendo na heshima, au kwa uovu na udhalimu? Watu watahuzunika kukukosa, au watashukuru ukiondoka?.