Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Screenshot_2018-02-21-00-27-11.jpg
 
Unaposoma kitabu, unaingiza mwanga kichwani (maarifa) na kuondoa giza (ujinga). Baada ya kwisha kukisoma, ule mwanga uliouingiza kichwani utakuongoza kwa kukumulikia njia, kipindi ambapo kitabu kitakuwa pembeni.
 
KATIKA mkutano mkubwa wa hadhara, bwana mmoja aliyekuwa amesimama katikati ya umati wa wahudhuriaji, alitoa bango kubwa (pana na refu) na kulinyanyua juu akilielekeza jukwaa kuu (mbele). Bango hilo kubwa liliwakera waliosimama nyuma yake, kwa sababu kwanza liliwakinga, na pili hawakuweza kuusoma ujumbe ulioandikwa kwa mbele. Na waliosimama mbele ya jamaa huyo, pia hawakutambua kama kuna mtu nyuma yao amenyayua bango lenye ujumbe f'lani. . Kwa bahati, viongozi walioketi meza kuu ndiyo waliliona vizuri bango hilo na kuusoma ujumbe wake. Kwa ujumbe ule, wapo waliocheka na wapo waliostaajabu. Hali hiyo, ikawafanya waliosimama mbele ya jamaa, kugeuka nyuma na kusoma kilichoandikwa. Nao, kama ilivyokuwa kwa wale wa meza kuu, walicheka ilhali baadhi yao wakistaajabu. Haikuwa rahisi kwa waliosimama nyuma kwenda mbele ya jamaa ili kuusoma ujumbe, hivyo waliendelea kusimama bila ya kujua kilichoandikwa huku wakipata taabu ya kukingwa na bango hilo. . Bango lilisomeka hivi: NIMENYANYUA HILI BANGO ILI TU KUWAKINGA WALIO NYUMA!. . Na kwenye maisha kuna watu wako vivyohivyo wankuwekea bango kubwa maishani ili kukuzuia, bila sababu ya msingi, usifanikiwe. Usipojiongeza hutafanikiwa na hutagundua kama umekingwa na bango kubwa ajabu.
 
INAUMA SANA . Kijana mmoja alifanya maamuzi ya kumpeleka baba yake ambaye, alikuwa amezeeka sana, kwenye makazi maalumu ya kulelea wazee ya Kanisa Katoliki. . Kijana alifanya hivyo, baada ya kushauriwa na mkewe, aliyekuwa akiona kero kumlea baba mkwe wake nyumbani kwao. . Ofisa katika sehemu ya mapokezi, alimuomba mzee huyo achague chumba kama anataka chenye TV na Kiyoyozi, au la; mzee akasema hahitaji chumba chochote Chenye TV wala Kiyoyozi. . Mwanaye alipokwenda kwenye Gari kuchukua begi la baba yake; mkewe aliyekuwa muda wote kwenye gari, akasisitiza kuwa kijana amwambie huyo mzee wake asiwe anarudi nyumbani kabisa, hata siku za Sikukuu, kwa sababu yeye hataki usumbufu wowote wa kumhudumia. . Kijana huyo ambaye ni mtoto wa pekee kwa mzee yule, alishangaa alivyorudi na mizigo ya baba yake, na kumkuta mzee wake akizungumza kwa furaha na bashasha na Padre, tena wakionekana kufahamiana sana. Walionekana wakiongea kwa kukumbushana mambo ya zamani ambapo, mzee alionekana mchangamfu isivyo kawaida. . Mtoto akamuuliza Padre, "Unafahamiana na baba yangu?". . Padre akajibu, "Ndiyo, namfahamu sana mzee huyu. Ni mtu mwema sana; alikuja hapa miaka 30 iliyopita, tukampatia mtoto yatima wa kiume akamlee, maana Mtoto huyo alitelekezwa. Na kwakuwa yeye na mkewe hawakuwa wamebahatika kupata mtoto, wakamchukua.". . Mabegi aliyokuwa kayashika mkononi kijana yule yalimdondoka bila kujijua. Alibaki ameduwaa huku machozi yakimtoka. Kumbe baba aliyemlea kwa wema na upendo hadi naye akafanikiwa maishani, hakuwa baba mzazi, alikuwa ni mlezi tu aliyemsitiri. Lakini yeye ameamua kumuondoa nyumbani kwake kwa sababu ya ushauri wa mke.
 
MAPENZI YA DHATI KATIKATI YA UMASIKINI. . SIKU moja wakiwa wamejilaza kitandani, mke alimwomba mumewe amnunulie chanuo kubwa kwa ajili kuchania nywele nyingi ili kuzipendezesha. Kiuchumi, hali ya mume ilikuwa dhoful'hal, asingaliweza kugharamia chanuo aliloombwa. . Kwa simanzi na huzuni kubwa, mume alimjibu mkewe, "Mpenzi wangu, si kama sitaki upendeze, la hasha. Hali yangu kifedha ni mbaya sana. Hebu tazama, ni zaidi ya mwezi sasa tangu mkanda wa saa yangu ya mkononi ikatike, lakini nimeshindwa hata kununua mkanda mwingine.". . Kama ameshindwa tu kujinunulia mkanda wa saa ulioharibika, ataweza kununua chanuo kubwa? Siku ikapita ilhali mke akiwa mnyonge kabisa. Lakini kwa kawaida, wanamume si watu wa kukubali kushindwa na kuonesha udhaifu mbele ya wake zao. Kwa kuumizwa na kitendo cha kushindwa kumnunulia mkewe chanuo tu, siku iliyofuata baada ya kutoka kazini, mume alipita mjini akaiuza ile saa yake, na fedha aliyopata akaenda kumnunulia mkewe chanuo. . Jioni ya siku hiyo, mume aliingia ndani akiwa na shauku ya kumshangaza mkewe kwa kumletea zawadi ya chanuo alilohitaji, lakini katika hali asiyotegemea alimkuta mkewe akiwa amenyoa nywele zake zote. Kuona chanuo alilonunua kwa gharama ya saa yake, likiwa halina kazi tena, kulimuumiza sana mume. . Alipomuuliza mkewe kwanini aliamua kunyoa nywele zake, akiwa ametabasamu mke alijibu: "Nimeuza nywele zangu ili kukununulia mkanda mpya wa saa yako!". . Mume aliupokea mkanda wa saa huku akibubujikwa machozi ya furaha, wakati huo mke naye akipokea chanuo lake huku machozi yakitengeza mifereji mashavuni mwake. Kila mmoja alikubali kuuza kitu chake cha thamani ili kumridhisha mwenzi wake.Ooh! Mahaba ya sayari gani haya!.
 
Unasema unapenda mvua, lakini ikinyesha unatembea chini ya mwamvuli. Unasema unapenda jua, lakini likiwaka unatafuta kimvuli. Unasema unapenda upepo, lakini ukivuma unafunga madirisha. Ndo maana huwa nina wasiwasi unaposema unanipenda. - Robert Marley
 
Bwana Kasuwi alipoingia mjini akiwa na pesa lukuki, alistaajabu mno kumwona bi Malika, mwanamke mrembo kupita kiasi, akiishi na bwana Makame, mwanamume masikini na dhalili. Kichwani mwake aliamini kwamba, mwanamke mzuri ni kiburudisho kwa mwanamume mwenye pesa. Kasuwi alimwonea maya na ngoa bwana Makame kwa namna alivyoishi na mjoli wake, kwa furaha na mbawazi. Ndipo kwa kutumia pesa zake, akafanyiza ghilba na hadaa hata akafanikiwa kumlaghai Malika na kuivunja ndoa yao. . Kwa fadhaa na uthakili, bwana Makame akatowekea nje ya mji kwenda kuanza maisha mapya ya simanzi na upweke. Watu wenye taamuli husema; mlango mmoja ukifungwa, mwingine hufunguka. Ndivyo ilivyokuwa, huko alikohamia bwana Makame, alipata bibi mwingine na kufunga naye ndoa. Haikuchukua muda, Mola akamruzuku mali; akafanya biashara hata akaingia katika orodha ya matajiri wakubwa. . Ikiwa imekatika miaka kadhaa, siku moja bwana Makame alirejea mjini kwao na kuwakuta Kasuwi na Malika wamefilisika mali. Na kama wahenga wasemavyo; umasikini uingiapo mlangoni, upendo hutorokea dirishani. Kwa hivi, Malika na Kasuwi waliishi kwa magomvi na machukizano. Makame akaona imewadia zamu yake kulipiza kisasi, kwa kutumia karata ya utajiri wake. Ndiyo, kwa pesa zake aliwanyoosha ipaswavyo hata akafanikiwa tena kumtwaa Malika na kuishi naye kinyumba. . Kufilisika kwa Kasuwi, kwa kiasi kikubwa kulisababishwa na hulka yake ya umalaya, ambapo alimwaga pesa kama njugu kwa kila mwanamke aliyemhitajia. Kweli aliwapata na kuwatumia, lakini mwisho wa siku pesa ziliondoka zikamwachia tuzo ya ushindi iitwayo UKIMWI. Kupitia kwa Kasuwi, Malika naye akaukwaa ugonjwa ule hatari. Na kwa kuhendekeza visasi, Makame akajikaribishia nakama; badala ya kumkomoa Kasuwi kama alivyodhamiria, ikawa amejikomoa mwenyewe kwa kujihamishia ugonjwa wa Makame kupitia kwa Malika. Kwa hulka ya umalaya, pesa ilimsababishia magonjwa Kasuwi; na kwa kasumba ya visasi, pesa ikamsulubu Makame. . Kwa ujumbe huu, na watatafakari wenye akili timamu.
 
NJIA BORA YA KULITAZAMA NA KULITENDA JAMBO. . SIKU MOJA Baba akiwa anajisomea gazeti, binti yake mdogo alikuwa akimtaabisha kwa michezo yake ya hapa na pale. Ili kumtuliza, alichukua karatasi ambayo kwa mbele ilichorwa ramani ya dunia, akaichanachana vipande vitano na kuvichanganya. Kisha akampa binti yake, akimtaka akakae chumbani na kuviunganisha ili kuurudisha mchoro wa ramani. Alikuwa na hakika kwamba ingemgharimu siku nzima kuupata mchoro ule. . Muda mfupi baadaye, binti alirejea na karatasi yake mkononi, akiwa amepatia kuupanga upya mchoro wa ramani kwa vipande vya karatasi vilivyochanwa. Kwa Baba alipomuuliza bintiye, ilikuwaje hata akafanikiwa kwa haraka kuipanga upya ramani ile. . Binti alijibu, "Baba, wakati unaichana hiyo ramani, nyuma ya karatasi hiyo kulikuwa na mchoro wa picha ya mtu. Kwa hivyo, nilichokifanya niliipanga vizuri ile picha ya mtu na nilipoigeuza nyuma tayari ramani ikawa imejipanga yenyewe." . Baada ya kumstaajabisha baba yake, binti alikimbia zake nje kwenda kucheza. . . FUNZO: Siku zote, kuna upande wa pili wa utatuzi wa tatizo pale upande mwanzo unapokuwia mgumu. Kwahiyo, ukumbwapo na tatizo au changamoto, na likakushinda kutatua. Usikate tamaa, hakika iko namna nyingine ya kulitazama, kulichunguza jambo lako, ili kulitatua kwa njia mbadala
Good story. Nmekusoma
 
UNAOGOPA NINI? Ukichunguza utagundua, wengi wetu tumejawa hofu bila sababu za msingi; hofu ya kupoteza vile tulivyonavyo, tunahangaika kutumia nguvu nyingi kuvidhibiti visituponyoke ili asitokee mwingine wa kuvigusa. Tunafikiri kwa kuvificha, vitaendelea kubaki nasi na kuwa vyetu milele. Tunajidanganya. Mambo hayako hivyo, hayajawahi kuwa hivyo, na hayatokuwa hivyo kamwe. Kama unafikiri kuna kitu chochote ulichonacho, kitadumu chini yako; iwe pesa, gari, nyumba, mpenzi, ni kujipumbaza akili. Ipo siku isiyokuwa na jina, vyote vinaweza kutoweka kwa pigo moja tu. Pigo moja tu, mtu wangu. Pesa kama ilivyotoka kwa wengine ikaja kwako, pia yamkini ikahamia kwa mwingine; binti yako kipenzi, siku akiolewa atakuacha na kwenda kuwa chini ya milki nyingine; mpenzi wako asipokuacha basi siku atakufa na hatokuwa wako tena. Shida kubwa, wengi tunaogopa kuanza upya pale tunapopoteza vile tulivyokuwa navyo, ndo maana tunajilazimisha kuvizuia visiguswe na wengine. Kama leo umepata kitu cha thamani l, basi weka akilini kwamba, hakuna unachoweza kukipata halafu ukashindwa kukipoteza, hata iwe roho. Ni suala la muda tu. Hata uwe tajiri, bado hujafikia bado ukwasi kiasi cha kushindikana kuishiwa ndani ya dakika tu. Hata upendwe vipi au uwe mzuri vipi, hujafikia ujanja wa kumzuia akupendaye kuondoka muda wowote. Kumbuka: Ulichonacho leo, jana hakikuwa chako na pengine kesho kisiwe chako tena. Kila unachokipata, utakiacha papahapa. Ulikuja mtupu na utaondoka mtupu. Sasa unaogopa nini? Vinavyotaka kuondoka acha viondoke. Madhali mapigo ya moyo yangali yanadunda vizuri, maadamu tundu za pua zingali zikinyonya hewa vizuri, alimradi damu inaendelea kupenya vizuri katika mishipa, basi unaweza kusimama - ukapamabana na kupata zaidi ya ulichopoteza. Kama uliweza kukipata mara ya kwanza, hutashindwa kukitwaa mara ya pili.
 
WEWE NI WA PEKEE. Hivi unajua kwamba, tangu kuumbwa kwa dunia, kati ya mabilioni ya watu waliopita na wajao, hajawahi kutokea na hatotokea mtu kama ulivyo WEWE? Kati ya wote waliopata kuishi juu ya mgongo wa ardhi au watakaokuja kuishi, hayuko mwenye mjumuiko wa vipaji, mwonekano, uwezo, huzuni, marafiki, furaha, maadui na fursa kama ulivyo WEWE. Kama ukuaji wa nywele zako tu, haufanani na wa yeyote; kama alama za vidole (fingerprints) vyako tu hazishabihiani na za yeyote, unashangaa nini kwamba hakuna kama WEWE? Hakuna mwenye siri n dhahiri sawasawa na zako, wala hayuko anayepitia mapito ya kifamilia na kijamii kama WEWE. Baadhi ya wapuuzi wachache wanaokucheka kwa kufanya mambo tofauti na wanavyotaka, wameshindwa kujua kwamba WEWE siyo wao. Acha wakucheke, acha wakununie; duniani hayuko anayependwa na watu walewale wanaokupenda WEWE, na akachukiwa na walewale wasiokupenda WEWE; hayupo, hajapata kuwapo na hatotokea. Sasa, thamini na furahia huo upekee; ni tunu Maanani aliyokutunukia, zawadi kwa ajili yako wewe tu. Haupaswi kuigiza maisha kwa kuongea, kutembea, kuimba, kucheza au kufanya lolote ili tu uonekane kama fulani. Haukuletwa duniani kuja kuwa kama fulani; ndo maana ukaumbwa tofauti na huyo unayetaabika kujifananisha naye. Hakuna popote katika kumbukumbu ya dunia, vitu vilevile unavyowaza na kuvifanya wewe, vikazunguka katika mtindo huohuo, kichwani kwa mwingine. Hakuna anayeweza kufungamana na jamii kwa namna hiyo hiyo unayofungamana nayo WEWE. Hayuko awezaye kuyazungumza maneno yako. Hakuna awezaye kustarehe kwa kiwango kilekile unachostaladhi wewe uwapo stareheni. Hakuna awezaye kuuchukua ufahamu wako na kuupandikiza kwa mwingine. Hakuna anayeweza kuwa na wivu na hasira kama vilivyo kwako. Wewe ni wewe tu. Kama utautumia vema upekee ulionao, katika kuyaenenda mambo yako, hakika utapaa katika kilele cha ubora. Kama unaimba, usijifananishe na Diamond; kama unacheza ndondi, usijifananishe na Mike Tyson; kama unaandika, usijifananishe na Shaaban Robert; kama wewe ni mtangazaji, halafu unajiigiza kwa Masoud Kipanya, si ni bora nizime idhaa unayotangaza - nikamsikilize huyo Kipanya mwenyewe? Itoshe tu kujifunza toka kwao ili kuuboresha upekee ulionao.
 
Back
Top Bottom