Kitendo cha Guardiola kutua kwenye kikosi cha Man City huko Etihad, akaamua kumwondoa Joe Hart na kisha kumchukua kipa wa Barcelona, Claudio Bravo. Joe Hart hakuwa na maisha tena Etihad na alitolewa kwa mkopo wa msimu mzima kwenda Torino inayoshiriki ligi ya Serie A huko Italia. Msimu ulipomalizika alirudi Man City, lakini akatolewa tena kwa mkopo mwingine kwenda West Ham United. Kitu kilichowashangaza wengi ni kitendo cha Guardiola kumwondoa Joe Hart na kumleta Bravo, ambaye kiwango chake kimeonekana wazi kabisa kwamba si cha kufurahisha kihivyo. Guardiola akaamua kufanya mabadiliko mengine kwenye nafasi ya makipa akimchukua Ederson kutoka Benfica, walau sasa kipa huyo anafanya vizuri.