Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

KILIMO CHA PAPRIKA

Zao hili hustawi vizuri mahali penye mwinuko wa mita 1000 hadi 2000 kutoka usawa wa bahari. Wastani wa mvua ni milimita 600 hadi 1200, na halijoto ya nyuzi za sentigredi kati ya 21 na 24. Udongo uwe tifutifu, rutuba nyingi,usiotuamisha maji, na udongo wenye uasidi au uchachu kati ya pH 5.5 na 6.5. Mahali pasipo na mvua za kutosha, ni muhimu kumwagilia shamba kulingana na mahitaji.
 
Mbegu za paprika husiwa kwenye kitalu kilichoandaliwa vizuri kwa kazi hii. Chagua mahali penye rutuba na maji ya kutosha. Epuka mahali ambapo palistawisha mazao jamii ya nyanya, biringanya na pilipili. Hii ni kwa sababu kuna uwezekano wa kuwepo mabaki ya wadudu au magonjwa ambayo pia hushambulia zao la paprika, Maadui wa mazao hayo wanafanana.
 
Kitalu kitayarishwe mapema kabla ya msimu wa mvua. Siha mbegu kwenye vijifereji vilivyonyooka, kisha funika kwa udongo mwembamba. Nafasi kati ya mistari ni sentimita 10 hadi 20. Kilo moja ya mbegu inatosha hekta moja.
 
Ni muhimu kumwagilia kitalu siku moja kabla ya kusia mbegu, halafu endelea kumwagilia kulingana na mahitaji ya udongo. Tuta lenye urefu wa mita 10 na upana wa mita 1, miche yake inatosha eneo la nusu hekta. Tandaza nyasi kavu juu ya kitalu au tumia plastiki nyeusi ili kuzuia uotaji wa magugu na kuhifadhi unyevu.
 
Mara nyingi wakulima hutumia mbegu za chotara (hybrid) ambazo hutolewa na kampuni ya Tanzania Spices Limited. Kwa maana hii haishauriwi kutumia mbegu kutoka kwenye zao la msimu uliopita, kwani ubora wa paprika utakuwa duni na hivyo kushusha bei yake kwenye soko.
 
Miche hukaa kwenye kitalu kwa wiki 6 hadi 8 baada ya miche hiyo kufikia urefu wa sentimita 6 hadi 10. Mwagilia kitalu kabla ya kung’oa miche. Panda kwa nafasi ya sentimita 75 hadi 90 (mche hadi mche) na sentimita 95 hadi 105 (safu hadi safu). Idadi ya miche kwenye hekta moja hufikia 12,500.
 
Iwapo ardhi ni bikira na ina rutuba ya kutosha, hakuna haja ya kuongeza mbolea, hasa kwa mwaka wa kwanza. Kama rutuba ya udongo haitoshi, vema kuweka mbolea ya ogani kiasi cha tani 20 hadi 30 kwa hekta.
 
Ifahamike kwamba, nyakati hizi walaji wengi katika nchi zilizoendelea wanapendelea mazao yaliyostawishwa bila kutumia pembejeo zenye kemikali. Aidha, unaweza kuongeza rutuba shambani kwa kutumia mbolea ya viwandani NPK yenye uwiano wa 4:7:7.
 
Vilevile mkulima anashauriwa kutumia kilo 140 hivi za mbolea aina ya SA au CAN kwa hekta wakati mimea inaanza kutoa matunda. Kitendo hiki huchochea mimea kutoa matunda makubwa na kutoa mavuno kwa kipindi kirefu.
 
Paprika huanza kuvunwa miezi 2 hadi 3 baada ya kupandikizwa. Uvunaji huendelea kwa muda wa siku 30 hadi 70. Chuma matunda yaliyoiva vizuri, yaani yenye rangi nyekundu. Mmea mmoja huzaa matunda 30 hadi 80.
 
Ubora wa zao hili na bei nzuri kwenye soko unategemea: ukomaaji, uwekundu wa rangi, ukaushaji, usagaji, upakiaji na hifadhi yake. Ieleweke kwamba matunda yakivunwa baada ya kukomaa kabisa hadi kuonyesha dalili za kukauka, hupata bei nzuri zaidi.
 
Nchini Tanzania, hekta moja ya shamba inaweza kutoa tani 2.5 hadi 3.5 za zao hili. Hata hivyo, wakulima makini wanaweza kufikisha mavuno ya tani 5 hadi 8. Mara baada ya kuvuna, andaa shamba upya kwa ajili ya mpando mwingine.
 
Paprika ikishavunwa, ianikwe juani na kugeuzwa mara kwa mara ili kuepuka sehemu moja kupauka rangi kwa sababu ya kuunguzwa zaidi na jua. Zao lianikwe kwa siku 2 hadi 4, hii itategemea hali ya hewa.
 
Back
Top Bottom