Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Kila Aprili 25, Shirika la Afya Duniani (WHO) huadhimisha siku ya kimataifa ya malaria. Nchi mbalimbali, wadau na wananchi huungana kuhamasisha katika mapambano dhidi ugonjwa huu hatari.

Siku hii huadhimishwa kila mwaka ili kuongeza hamasa kwa wadau, kwa miaka 70 mfululizo sasa. Takwimu za WHO zinaonyesha malaria ndiyo ugonjwa unaoongoza kwa kusababisha vifo vingi duniani.
 
Inakadiriwa kuwa watu 445,000 hupoteza maisha kila mwaka kutokana na maradhi haya huku zaidi ya milioni 216 wakiugua mwaka 2016 pekee.

Ugonjwa huu hatari unaosababishwa na vijidudu vijulikanavyo kama plasmodium vinavyoenezwa kutoka mtu mmoja kwenda mwingine baada ya kuung’atwa na mbu jike ajulikanaye kama anopheles.
 
Kuna takriban jamii 3,500 za mbu wanaoneza magonjwa mbalimbali lakini hakuna hata mmoja anayeweza kusambaza virusi vya Ukimwi.

Katika kusherehekea siku ya malaria duniani mwaka huu, leo tujifunze sababu kuu za kisayansi zinazotoa ufahamu kwa nini mbu hawawezi kueneza VVU.

Mfumo wa unyonyaji damu unakinyima nafasi kirusi cha Uimwi kuenezwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine inatokana na maumbile na mirija ya mbu.
 
Mdomo wa mbu una sehemu sita, kati ya hizo sehemu nne hukita kwenye ngozi ya mwanadamu au mnyama anayemng’ata.

Sehemu nyingine mbili zina mirija miwili; mmoja huwa na kazi ya kutiririsha mate kwenda kwa mtu anayeng’atwa na mwingine hufyonza damu kurudi kwa mbu.

Mfumo huu wa mirija miwili ndio sababu ya mbu kushindwa kueneza VVU kwani hata akifyonza damu yenye VVU atakapokwenda kwa mtu wa pili atamwingizia mate na si damu yenye VVU aliyofyonza awali.
 
Hivyo, mbu anapong’ata ni lazima acheue mate yatakayoingia kwa mtu kisha kufyonza damu na si kufyonza damu na kuitema kwa mwingine.

Tofauti na wadudu wengine, VVU haviwezi kuzaliana na kuongezeka vikiwa kwenye utumbo wa mbu na vikiingia humo huvunjwa vunjwa.

Ikumbukwe kuwa katika mwili wa mwanadamu virusi vya Ukimwi hujipachika katika chembehai nyeupe zijulikanazo kitabibu kama T-cells na kuanza kutumia malighafi za seli hizo ili kuzaliana.
 
Lakini ndani ya tumbo la mbu hakuna chembe hai hizi hivyo kuvinyima nafasi virusi vya Ukimwi kuzaliana au kuvamia tezi zinazohifadhi mate ya mdudu huyo.

Kama virusi vya Ukimwi vitaingia tumboni mwa mbu humeng’enywa pamoja na damu iliyofyonzwa katika mfumo wa usagaji wa chakula wa mbu. Wakati wa umeng’enywaji damu, virusi hivyo huvunjwa vunjwa kabisa na kuharibiwa.

Kiwango kidogo cha VVU kinachokuwa katika mzunguko wa damu ya mbu ni sababu ya kutoweza kusababisha maambukizi mapya kwa binadamu.
 
Hivyo, hata kama mbu angeweza kusambaza VVU kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine angeshindwa kwani kiasi atakachokibeba hakitoshi kusababisha maambukizi mapya kwa mtu aliyemuuma.

Hata ikitokea kwa bahati mbaya mbu huyo aliyenyonya damu yenye VVU ukamla au akapasukia katika jeraha bichi mwilini kiasi hicho hakitoshi kuleta uambukizi.

Nihitimishe kwa kuwatoa hofu wananchi wanaoishi pamoja na ndugu zao wenye VVU au wagonjwa wanaolazwa katika huduma za afya katika maeneo yenye mbu kuwa wadudu hawa hawaenezi VVU.
 
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…