Akiwa chuo kikuu cha kilimo cha sokoine hii leo,Rais w Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dr John Magufuli ametamka kuwa ameshatoa maelekezo semina zote za serikali zifanyike kwenye kumbi za taasisi za umma na si kwenye kumbi za hotel za watu binafsi.
Kwa sisi tunaoamini katika sera ya ubia tunazidi kustushwa sana na mwelekeo huu wa serikali ya awamu ya tano katika kuzijengea uwezo sekta binafsi.
Ipo wazi kabisa,maeneo mengi nchini Tanzania biashara zinazoendeshwa na sekta binafsi zimeyumba sana,leo ukienda mijini unajionea wazi jinsi biashara ilivyoyumba.
Sekta binafsi ipo hoi,inapunguza wafanyakazi kila kukicha huku ikihemewa na gharama za uendeshaji,bahati mbaya serikali haioni hili kama ni doa kwenye uendeshaji wa uchumi wa nchi.
Leo nimesoma kwenye vyombo vya habari vikiarifu kuwa kampuni ya Max Malipo inapunguza wafanyakazi,haya ni matokeo ya sera za kuuwa sekta binafsi,
Max Malipo wameondoshwa kwenye mradi wa kukusanya mapato kwenye mradi wa mabasi ya mwendo kasi,wamekatwa nguvu kwenye mradi wa kukusanya mapato ya Nishati ya Umeme.
Sera nzuri za serikali zilitakiwa kuhakikisha mtaani kunazaliwa Max Malipo nyingi na siyo kuiona Max Malipo inakufa,sekta binafsi ni injini ya uchumi,bila sekta binafsi imara ndoto ya maendeleo endelevu inakuwa katika mashaka.
Kila kukicha sekta binafsi inatangaza kupunguza watumishi,kampuni moja kubwa ya habari hivi karibuni ilipunguza kwa wakati mmoja watumishi wake zaidi ya 60 na hili halionekani kama ni tatizo zaidi tunasema mambo yapo sawa.Muelekeo huu wa kisera inakwenda sababisha vyombo vingi vya habari binafsi kupunguza watumishi kama siyo kufunga kabisa.
Biashara ya hotel Tanzania sasa imeyumba kwa kiwango kikubwa,kuyumba kwa sekta binafsi sasa kunaanza kuonesha athari zake,baadhi ya bidhaa zinaelekea kupanda bei,huku mtaani bei ya mafuta ya kupikia inapaa kila siku na hakuna mjadala,sukari ilishapanda na hatujaweza irudisha,zipo taarifa mwelekeo wa bei ya sabuni si mzuri kama hatutachukua hatua za kisera kurekebisha hali hii.
Ni hatari kuiua sekta binafsi kisera,si sawa kuiacha sekta binafsi ife kimkakati,si sawa kudhani nchi inaweza kwenda bila kuijenga,kuilea na kuishirikisha sekta binafsi.
Suala la sekta bianafsi si suala la utashi wa mtu,ni suala la kisera na sheria,tulipitisha sera mwaka 2009,mwaka mmoja baadae tukatunga sheria yake,haya yote yalikuja baada ya kuiona athari za kuwa na sekta binafsi dhaifu.
Makosa haya yalifanyika huko nyuma,tatizo la nchi hii lilikuwa ni kushamiri kwa Rushwa,serikali ilitakiwa kuidhibiti Rushwa na kuacha mfumo wa uchumi tuliouchagua uendelee kukua,mfumo wa kuishirikisha sekta binafsi.
Tulijenga mfumo mzuri wa kisera wa ubia kati ya serikali na sekta binafsi mwaka 2009,mfumo huu ulidhoofishwa na Rushwa,kuiua sekta binafsi si sawa,Serikali ilitakiwa kuweka nguvu kwenye kupambana na Rushwa na si kutekeleza sera zinazoizoofisha sekta binafsi,mwelekeo huu wa kiuchumi si sahihi .
Yapo mengi mazuri ya kimaendeleo Serikali inayafanya ikiwemo ujenzi wa miundombinu kama barabara,reli,madaraja,hii ni kazi nzuri sana lakini haitakuwa na faida kama tutakuwa na sekta binafsi dhaifu na fukara.Tunahitaji mjadala kuhusu sekta bianfsi.
Wasalaam.