Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Saluni za mbwa

Nafunga safari hadi katika moja ya saluni maarufu za mbwa huko Poppersdorf mjini Bonn. Hapa kuna shughuli kwelikweli.

Mbwa wengi wenye kamba zao shingoni wako hapa wakiwa wanatengenezwa au wakisubiri kutengenezwa.

Wapo waliokuja kuoshwa nywele, wapo waliofika hapa kukatwa mitindo mbalimbali ya nywele na kucha. Wengine huwekewa mapambo mbalimbali kama riboni au kutobolewa masikio na kuvalishwa hereni.
 
Roswitha Knauher, mkazi wa St Augustin, Bonn anasema yeye ana mbwa na mume wake ana mbwa.

Lakini wana mbwa mwingine wa ziada ambaye ni mdogo.

Anasema matunzo ya mbwa watatu ni makubwa lakini wanakabiliana nayo kwa sababu wanawapenda wanyama hao.

“Naweza kutumia hata Euro 2,500 (zaidi ya Sh6 milioni kwa mwaka) kwa mbwa hawa wote, nikijumlisha na hospitali gharama huweza kuongezeka,” anasema.
 
Kwa mujibu wa sheria ya ulinzi wa wanyama ya Ujerumani, kama mlezi wa mbwa hafuati sheria za malezi ya mnyama huyo anapigwa faini. Wamiliki wa mbwa wanatakiwa kutafuta mtu wa kumuangalia mnyama huyo iwapo hawana muda.

Wakishindwa wanatakiwa kumuuza, kumpa mtu mwingine au kuweka tangazo la anayemtaka. Hii ni kwa paka pia.

Kadhalika sheria zinaeleza wazi kuwa mbwa hatakiwi kukaa peke yake bila kutembezwa kwa zaidi ya saa tano.
 
Iwapo mbwa atabaki ndani, anahitaji mazoezi na ikiwezekana afanyishwe mazoezi hayo na mlezi. Inatakiwa mbwa atembezwe kwa angalau saa moja kwa siku.

Pia, wamiliki wa mbwa hawatakiwi kumfunga kamba awapo ndani ya nyumba au kumfunga kamba na kumuacha katika chumba cha peke yake.
 
Kodi ya mbwa

Mbwa wote Ujerumani wanatakiwa kusajiliwa na kupewa leseni na wapo chini ya ‘Hundesteuer’, maana yake ni kodi ya mbwa. Jonas anasema malipo ya kodi hii yanategemea nchi unayoishi.

“Wazazi wangu wanalipa karibu Euro 80 (zaidi ya Sh200,000) kwa mwezi na fedha hizo zinakatwa moja kwa moja katika akaunti yako,” anasema.
 
Kuasiliwa

Kama watu wengine wanavyokwenda katika vituo vya ustawi wa jamii kuasili watoto, hapa Ujerumani mbwa na paka huasiliwa.

Inakadiriwa kuwa wanyama 300,000 wengi wakiwa ni mbwa na paka wako katika makazi maalumu na wanatakiwa kuasiliwa.

Kama unataka kuasili mbwa unatakiwa kwenda katika kituo maalumu kiitwacho Tierheim, yaani makazi ya wanyama. Huko utajaza fomu maalumu na utachunguzwa kama kweli unaweza kutunza mbwa.
 
Pia, utatakiwa kujaza fomu maalumu, utatoa mawasiliano na kitambulisho. Baada ya hapo mlezi wa mbwa anatakiwa kulipa ada ya uasili kiasi cha Euro 220 (zaidi ya Sh500,000) kwa mbwa na Euro 65 hadi 85 (zaidi ya 150,000 hadi 250,000) kwa paka.

Mbwa katika usafiri wa umma

Nadhani mbwa akionekana katika daladala la Gongo la Mboto kwenda Kariakoo patazuka tafrani, lakini hapa ni kawaida na ni haki. Mbwa ana haki ya kupewa siti na anatakiwa kuheshimiwa pindi anapokaa katika chombo cha usafiri.
 
Hata hivyo, anatakiwa kulipiwa nauli. Iwapo nauli ni Euro tatu (Sh8,000) basi atalipa nusu ya fedha hiyo.

Miongoni mwa yaliyonikumba nikiwa Ujerumani, ni pamoja na mmiliki mmoja wa mbwa kukasirika baada ya mimi kumuogopa mbwa wake.

Alikuwa kapanda kwenye treni na jibwa kuubwa jeusi wale wanaoitwa German Shepherd na akaketi karibu na mimi.
 
Mbwa wake akaanza kunilamba nami kwa woga wangu nikapiga kelele na kuruka. Hapo ndipo Mjerumani alipocharuka na kuhoji kwa nini namuogopa mbwa wake.

Bima ya mbwa

Bima hii inakatwa kila mwezi na ni kiasi cha Euro 80 (zaidi ya Sh170,000). Kama ilivyo kwa kodi, bima nayo inakatwa katika akaunti kila mwezi.

Jonas anasema bima hii inasaidia kwani pindi mbwa akipata ajali au akisababisha ajali inatumika kufidia au kufidiwa. Ni kama ilivyo kwa bima ya nyumba na za magari. Pia inatakiwa kuhuishwa kila mwaka.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…