Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Baadaye kijana huyo anamwacha mlemavu wake na kwenda kwa yule wa Shadrack. Anamuweka vizuri na baada ya dakika takriban tatu, akaja kijana mwingine na kumchukua ombaomba mwingine ambaye alikuwa amelala chini.

Baadaye niligundua anaitwa Pili Iyobhe. Huyu nilipeleleza habari zake hadi nikapata taarifa za kutosha kuwa anatokea mkoani Shinyanga, na hivyo ikawa rahisi kumfuatilia hadi nyumbani kwa wazazi wake.
 
Mtoto huyo wa kike ana tatizo la kichwa kikubwa na muda mwingi anakuwa amefumba macho. Tofauti na wenzake wenye baiskeli, alikuwa amelala chini.

Lakini kijana aliyemfuata, anambeba na kumuweka kwenye baiskeli kisha kwenda kwa kijana aliyekuwa akimrekebisha mtoto anayesukumwa na Shadrack.

Baada ya muda mfupi, vijana wapatao saba wanakusanyika eneo hilo na kujadili jambo fulani, na baadaye kusambaa kila mtu njia yake na dakika 10 baadaye kila mmoja anamchukua mlemavu wake na kwenda naye kupanda basi la mwendokasi.
 
Kutokana na kuwa na walemavu, walipitiliza kukata tiketi badala ya kupanga foleni kama abiria wengine. Wakati naendelea kushuhudia hayo, akatokea Shadrack mnamo saa 1:00 usiku akiwa ameshamchukua yule mlemavu aliyekuwa amemuacha.

Wakati anakata tiketi, nikamuuliza anakoelekea na kunijibu kuwa anapanda basi la Kimara, nami nikapanda basi hilo lakini nikamuona anashukia kituo cha Bakhresa eneo la Manzese. Nami nikashuka na kuanza kumfuatilia kuelekea Tandale.
 
Akaingia kwenye nyumba mmoja ya kulala wageni, ambayo jina tunalihifadhi na juu ya geti kuna namba za simu (ambazo pia tunazihifadhi kwa sababu za kimaadili).

Nyumba hiyo imezungukwa na nyumba nne na nje ya geti kuna mama anapika sambusa.

Baada ya kununua sambusa mbili naanza kumhoji kuhusu nyumba hiyo na wateja wake.

“Hii ni gesti mwanangu na nafasi zipo. Kama unataka wewe ingia tu ndani utawakuta wahusika,” anasema.
 
Samahan uandishi wangu sio mzuri sana.
 
Nami naingia ndani ambako nakuta baiskeli nne za walemavu zikiwa zimesimamishwa kwenye mlango wa kuingilia vyumbani na nyingine tatu zikiwa nje, pia alikuwapo Shadrack aliyekuwa anaongea na simu huku akiwa ameshikilia baiskeli yake iliyokuwa na mtoto mlemavu.

Ndani ya nyumba kulikuwa na sauti ambazo baadaye nilibaini zilikuwa za watu waliokuwa wakizungumza Kisukuma.

Baadaye akatoka kijana mrefu na nilipomuuliza kuhusu vyumba, alinijubu kuwa mhusika anaitwa Jose na akaenda kumuita.
 
Jose amekwenda wapi?” anawauliza wenzake kwa kutumia lugha ya Kisukuma na wanamjibu kuwa ametoka kidogo.

Nikiwa nasubiri, namsikia Shadrack akiendelea kuongea na simu akisema: “Nakwambia jamani, uje unisalimie tu. Kwani ukija kunisalimia ni vibaya? kwa nini hivyo? Uje bwana unisalimie nimesharudi.”

Nyumba hiyo ina korido ndefu yenye vyumba vidogo kila upande. Chumba cha kwanza hakikuwa na mtu aliyepanga ila vyumba vilivyobaki vilikuwa na watu ndani na katika korido kuliegeshwa baiskeli mbili za walemavu.
 
Baada ya kushuhudia hayo, nilienda nje na kukaa eneo ambalo vijana walikuwa wakiuza ndizi, mbali kidogo na nyumba hiyo ya wageni.

Nikiwa nimekaa eneo hilo, alipita mlemavu mwingine akiwa anasukumwa kwenye baiskeli na kijana mdogo anayekadiliwa kuwa na miaka 16.

“Samahani kaka naomba kuuliza mara nyingi nikiwa maeneo haya huwa ninaona walemavu wengi wanapita hapa, wanakwenda wapi?” niliuliza vijana niliokaa nao.
 
Pole dada hujui wanapokwenda? Mradi wa mtu huo,” alijibu mmoja wao huku wengine wakicheka.

Alisema hiyo ni biashara mpya imeingia mjini na kuna watu wanaowachukua walemavu kutoka vijijini na kuwaleta mjini kufanya kazi ya kuombaomba.

“Dili hilo dada,” alisema kijana mwingine.

“Tena mmoja wa wanaofanya biashara hiyo alikuwa maeneo hayahaya. Sijui kaenda wapi? Hii ndiyo biashara inayomuweka mjini.”
 
Siku tatu ndani ya gesti

Taarifa za biashara hiyo zilinifanya niamue kupanga ndani ya nyumba hiyo, nikijifanya mmoja wa wa wageni, kwa lengo la kujua walemavu hao wanaishije ndani ya nyumba hiyo, wametokea wapi, nani anawaleta na wanafanyaje shughuli hiyo.

Siku nilipokuja kuchukua chumba, nilimkuta mwanamke mjamzito akifua nguo na baada ya kumuuliza mhusika, alinipa namba za simu za nyumba hiyo.

Baada ya kumpigia, kijana aliyepokea alijitambulisha kwa jina la Jose na kuniomba nimsubiri na baada ya takriban dakika 10 aliingia.
 
Chumba kimebaki kimoja,” ananiambia na nikamuomba nikakione.

Ni chumba kidogo chenye kitanda cha ukubwa wa futi tatu kilichotandikwa shuka la maua ya rangi tofauti zilizofubaa.

Ndani ya chumba kulikuwa na feni na kiti kilichochakaa cha plastiki, taulo na choo kichafu. Kitanda hakikuwa na neti wala shuka la kujifunika. Kila kona ya chumba imechorwa alama ya msalaba wa rangi nyeusi.

Kuna ndoo moja ya lita 10 kwa ajili ya maji na choo kilikuwa kama kimeziba.
 
Chumba ni Sh7,000,” alisema baada ya kumuuliza na baada ya kumuomba apunguze, alisema kama ningekuwa nakaa zaidi ya mwezi angenifanyia Sh6,000.

Nikamlipa Sh21,000 kwa ajili ya malipo ya siku tatu na nikajisajili kwenye kitabu cha wageni. Baadaye, nikatoka kuchungulia vyumba vingine vilivyokuwa vimeachwa wazi na inaonekana vyote vimefanana.

Katika kuulizauliza, niliambiwa alama hiyo ya msalaba ni kinga dhidi ya watu wanaofanya biashara haramu ya walemavu kwa imani za kishirikina.

Tofauti na sehemu nyingine, vyumba vitatu vilikuwa na vyombo na majiko ya kupikia, kama vile vyumba vya makazi na si vyumba vya kulala wageni
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…