Aingia Flamengo, asaini mkataba
Vinicius alisaini mkataba wa timu ya watoto Flamengo akiwa na umri wa miaka 10 tu na tangu wakati huo akawa anapewa mazoezi ya kibabe na kumfanya awe mahiri zaidi. Aliitwa kuichezea Timu ya Taifa ya Brazil kwa vijana waliochini ya miaka 15 akiwa na miaka 13 tu. Mwaka 2015, Vinicius aliongoza Flamengo kubeba ubingwa wa Copa Votorantim, moja ya michuano mikubwa kabisa huko Brazil kwa timu za umri chini ya miaka 15. Alikuwa mfungaji bora kwenye michuano hiyo akifunga mara sita katika mechi tisa. Mwaka 2016, Vinicius alihamia kwenye timu ya chini ya miaka 17, akiwa mwaka mmoja nyuma kuliko wenzake kwenye kikosi. Akang’ara tena, kwa kufunga mabao 10 na kuongoza kwa asisti na kuifanya Flamengo kubeba ubingwa wa Ligi ya Rio de Janeiro. Kwenye timu ya chini ya miaka 20, aliisaidia Flamengo kushinda ubingwa wa Kombe la Vijana la Sao Paulo, licha ya kucheza mechi hizo akiwa na pungufu ya miaka mitatu tofauti na wachezaji wenzake wengine. Baada ya kufika umri wa miaka 16 tu, haraka sana Flamengo ilimsainisha mkataba wa miaka mitatu wa soka la kulipwa na hapo ikamwekea kipengele cha Euro 30 milioni kwa timu inayotaka kumsajili, huku klabu ikiwa na haki ya umiliki wa mchezaji huyo kwa asilimia 90.