BARUA YA WAZI KWA SPIKA NDUGAI KUTOKA KWA WABUNGE
Mhe Spika, kuhusu suala la CAG, tunaunga mkono dhana ya kutokubali Bunge kudharauliwa. Hata hivyo tunaona sasa unaenda mbali na hili suala. Tunaona ume-overreact kiasi cha kuliondolea Bunge sifa, uwezo na heshima ya kufanya kazi yake. Tunataka Bunge liheshimiwe lakini hatukubaliani kabisa na uamuzi wako wa kuzuia Bunge sasa tusiangalie hata mahesabu ya Serikali na mashirika ya umma na Serikali za Mitaa. Hapa umeenda mbali sana na kuyabaka mamlaka ya Bunge na kuliondolea nguvu Bunge wewe mwenyewe.
Kitendo hiki kimetusikitisha sana kwani kimekosa hekima, busara na utulivu na subira na uvumilivu ambazo ndio sifa za Maspika kote duniani. Tena uamuzi huu umeuchukua bila ushauri wa Kamati ya Uongozi.
Hii dhana kwamba hatutaki kufanya kazi na CAG haina mantiki na haitamzuia CAG kufanya kazi yake. Kwa mujibu wa Katiba, CAG yeye hukagua na kupeleka ripoti kwa Rais. Yeye kazi yake inakuwa imeisha. Rais ndio huleta ripoti Bungeni. Ukisema hufanyi naye kazi na CAG manake ni kwamba unasema wewe ndio hufanyi kazi yako, yeye kazi yake kishamaliza. Unapozielekeza Kamati zisifanyie kazi ripoti ya CAG manake unazielekeza Kamati zisifanyie kazi ripoti iliyoletwa Bungeni na RAIS.
Mhe Spika tunajua utasema kwamba lazima tusikubali Bunge kudhalilishwa na kudharauliwa na kwamba kote duniani hakuna Bunge linakubali hivyo. Sisi tunasema kwamba that’s bullshit. Kila siku wananchi wa aina zote wanatoa maoni yao kuhusu Bunge na wengine wanadiriki kusema kwamba Bungeni tunakuja kulala tu. Hawa hawajadharau Bunge.
Mhe Spika hizi hasira kali tungezielewa kama ungezielekeza kwenye maamuzi ya Serikali kuingilia Bunge: kwenye kupunguza ziara za Kamati, kuzuia Semina, kuagiza baadhi ya Wenyeviti wa Kamati waondolewe (Kafumu, Ghasia), kutupangia Kamati. Je, huu sio udhaifu wa Bunge? Mhe Spika tungekuelewa iwapo hasira zako zingeenda huko kwenye haya mambo ya msingi kuliko kwenye kauli tu ya mtu.
Mhe. Spika ukitaka kujua Bunge linadharauliwa ni pale Serikali iliposema kuonyesha shughuli za Bunge ni gharama lakini vishughuli vidogo vidogo vya Serikali vinaonyeshwa. Hasira yako ielekee huku pia. Hata pale watu na mashirika yaliposema yapo tayari kugharamia matangazo ya Bunge, Serikali ilikataa na Bunge likaufyata. Je huu sio udhaifu?
Mhe Spika, kitendo chako cha kuvunja Kamati za Mahesabu na kuzuia zisiangalie mahesabu yaliyoletwa Bungeni na RAIS kisa tu kauli ya CAG, yaani kauli tu, kilipaswa kupelekea sisi tukuondoe madarakani kwani umekosa busara, hekima, uvumilivu na subira inayohitajika ili kukalia kiti cha Spika. Hata hivyo, tutakusikiliza ukitoa hotuba na mhadhara wa Mabunge kukataa kudharauliwa, tutakusikiliza huku na kupiga makofi. Lakini ndani ya nyoyo zetu tunajua umekosea, umeenda mbali sana, na pia mara nyingi, tena kwa vitendo, umesharuhusu Bunge kudhalilishwa. Tutakusikiliza. Machoni tutaonyesha kukubaliana na wewe lakini nyoyoni sote tunajua, na wewe unajua, kwamba umekosea. Umekosea kuchukua maamuzi makubwa ya kusimamisha kazi ya Kikatiba ya Bunge ya kutazama mahesabu ya umma bila kulishirikisha Bunge. Lakini hatutakuwa na cha kufanya. Unajua kwanini? Kwasababu sisi ni dhaifu. Wabunge dhaifu huzaa Bunge dhaifu.
Ni sisi, Wabunge wazalendo 48 wa Kutoka Vyama Vyote
Kwaniaba yao
Joseph msukuma (Mb)
Mwenyekiti wa ccm Geita
C&P