Ernest Bwire aliwasili Kenya kutoka kwao Uganda akiwa na matumaini makubwa ya kujiendeleza kikazi, lakini yote hayo ni ndoto sasa.
Kwa miaka 29 sasa Bwire amekuwa akitumikia kifungo jela.
Kwa sasa yupo gereza la Kamiti liliopo kilomita 16 kutoka katikati mwa jiji la Nairobi ambako anatumikia kifungo cha maisha kwa mauaji.
Kufikia sasa Bwire ndiye aliyetumikia kifungo cha miaka mingi zaidi nchini Kenya.
Hata hivyo anasema hana hatia kwani hakuhusika na mauaji.
``Huyo kijana aliyenyongwa Nairobi nilikua rafiki mkubwa wa familia yao, na nisingeweza kufanya tendo hilo, lakini nimeikubali hali yangu ya sasa. Kwanza nilihukumiwa kunyongwa kisha baadae wakanihurumia nikafungwa maisha,'' Bwire anasema alipozungumza na John Nene wa Idhaa ya Kiswahili ya BBC huko Kamiti