Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Kanuni ya residual powers haiwezi kutumika kutengeneza mamlaka ambayo tokea asili yake anayedai mamlaka hayo hakupewa na Katiba au Sheria za nchi. Kutokana na kanuni hii inayodhibiti matumizi ya residual powers katika mahusiano baina ya mamlaka za nchi, ndio maana haikutumika katika muungano wa Uingereza.

Pamoja na Uingereza na Scotland kuwa na miungano miwili; ule wa kifalme wa 1603 (Union of Crowns) na ule wa mkataba wa 1707 (Articles of the Union), lakini Mfalme James Stuart baada ya kuwa mfalme wa nchi zote mbili, za Scotland na England, alishindwa kuziunganisha nchi hizo mbili kwa kutumia mamlaka yake kama mfalme, ingawa yeye mwenyewe alihisi ana mamlaka hayo kwa kanuni ya residual powers.
 
Katika kulitekeleza hilo alifikia hata kutengeneza bendera mpya ya Muungano (Union Jack), lakini wenzake walimtanabahisha kwamba hana mamlaka ya kutumia residual powers za ufalme kwa suala hilo chini ya mfumo wa kikatiba wa nchi hizo. Ndio maana muungano wao rasmi ilibidi usubiri kwa zaidi ya miaka mia moja na hatimaye ukaanzishwa kwa kupitia mkataba wa muungano wa 1707, ambao ndio unaoipa Scotland haki ya kupiga kura ya maoni kuamua kama wanataka bado kuendelea kuwemo katika muungano kila wanapoamua kufanya hivyo.
 
Kama Muungano huo ungeanzishwa na Mfalme Stuart kwa residual powers, Waskochi leo wasingekuwa wanafaidi uhuru wa kuamua juu ya hatma yao. Ni vyema kwa Wazanzibari nao kutahadhari sana na hichi kirusi kipya cha Muungano cha residual powers kinachotaka kupandikizwa na Profesa Kabudi.

Siamini kwamba mwalimu wangu hayafahamu haya na zaidi ya haya niliyoeleza. Labda wale viongozi wetu wa Zanzibar waliotuingiza katika mtego wa komba ndio inawezekana wanapata shida kuyafahamu haya na hata wanapofahamishwa, kwa kuwa wazi uchu wa kipande cha ndizi kinawakosesha tafakuri.
 
Inaaminika kwamba kisiwa cha Latham kiliitwa jina hilo kutokana na meli ya Kiingereza iliyokuwa ikiitwa Latham ambayo ilitia nanga katika kisiwa hicho mwaka 1758. Aidha, kinajulikana kwa jina la Fungu Mbaraka kutokana na Bwana Ahmed Mbaraka ambaye alipewa ruhusa na Sultani kuzamia katika mabaki ya meli iliyozama jirani na kisiwa hicho na akapata fedha nyingi zilizomuwezesha kupata utajiri na kununua ardhi kubwa sehemu ya Nyamanzi.
 
Kisiwa hichi kina mnyanyuko wa futi 10 kutoka usawa wa bahari na kinakaliwa na ndege tu hali iliyopelekea kuwa maarufu kwa samadi ya ndege (guano) ambayo watu na makampuni kadhaa wamewahi kuomba kukitumia au hata kwenda kukichukua bila ya ruhusa. Rasilimali hiyo ya samadi nyingi ya ndege ni miongoni mwa mambo yaliyokipa umaarufu sana kisiwa hichi hapo siku za nyuma.
 
Kabla ya mikataba baina ya Waingereza na Wajerumani; ule wa 1886, 1888 na ule wa Heligoland wa mwaka 1890, kisiwa hicho kilikuwa chini ya mamlaka ya Zanzibar bila ya ubishi wala utatanishi wowote. Mikataba hiyo miwili ndiyo iliyozusha utatanishi kuhusu umiliki wa Zanzibar juu ya kisiwa hicho. Sababu za utatanishi huo ni kama zifuatazo:
 
Ibara ya 1 ya Mkataba wa mwaka 1886, iliyatambua mamlaka ya Sultani wa Zanzibar juu ya visiwa vya Zanzibar na Pemba na visiwa vidogo vidogo ndani ya mzunguko wa meli 12. Kwa vile kisiwa cha Latham kipo umbali wa maili 36, ikatafsirika kuwa hakikuweza kuingia katika makubaliano ya ibara hiyo ya 1 ya mkataba wa 1886;

b. Sababu ya pili ni kuwa kwa mujibu wa ibara ya XI ya Mkataba wa Heligoland wa 1890, Ujerumani ilikubali kuyatambua mamlaka ya Sultani juu ya visiwa vya Zanzibar na Pemba na mamlaka nyenginezo zilizobaki. Ibara hiyo haikuweka wazi kama kisiwa cha Latham kilikuwa miongoni mwa mamlaka hizo nyenginezo au la;
 
Sababu ya tatu ambayo iliongeza utatanishi ni kuwa mikataba yote haikutoa mamlaka bayana kwa Wajerumani wala Waingereza juu ya kisiwa cha Latham.

Hata hivyo, pamoja na utatanishi huo wa kimikataba, hakukuwahi kutokea ubishani wowote au hoja yoyote juu uhalali wa umiliki wa Zanzibar kwa kisiwa cha Latham kati ya mwaka 1886 hadi 1898.
 
UBISHANI JUU YA UMILIKI WA KISIWA CHA LATHAM

Hoja ya nani mmiliki halali wa kisiwa cha Latham ilizuka mwaka 1898 baada ya kampuni moja iitwayo Messr Dawson & Company ya 9 & 10 Pancras Lane, Queen Victoria Street, London ilipoiandikia Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza kuulizia nani mmiliki halali wa kisiwa cha Latham kati ya Ujerumani na Zanzibar.
 
Baada ya kupata suala hilo, tarehe 19 Agosti 1898, Wizara ya Mambo ya Nje ilimuandikia Waziri Kiongozi wa Sultani (First Minister) kutaka ufafanuzi wa jambo hilo. Balozi Mdogo na Wakala wa Uingereza aliyekuwepo Zanzibar, Sir Arthur H. Hardinge, alijibu barua hiyo tarehe 4 Oktoba 1898. Katika barua yake, alitoa ufafanuzi juu ya kisiwa hicho na msimamo wa kisheria unaotokana na mikataba ya 1886 na ule wa 1890. Hatimaye alihitimisha kwa kusema kuwa kwa vyovyote vile kisiwa hicho hakiwezi kuwa cha Ujerumani. Hata hivyo, alieleza pia utatanishi wa kisheria uliopo juu ya umiliki wa Zanzibar pia.
 
Baada ya kujibu barua hiyo, Sir Arthur Hardinge mnamo tarehe 15 Oktoba 1898 alimuandikia barua Sir Lloyd Mathews ambaye alikuwa Waziri Kiongozi wa Sultani kutoa ufafanuzi zaidi na ushauri wake juu ya kisiwa cha Latham. Katika barua yake alieleza kuwa chini ya mikataba yote miwili kisiwa hicho hakiko chini ya mamlaka ya Ujerumani wala Uingereza. Aidha, mikataba hiyo haikuweka bayana kuwa kiko chini ya mamlaka ya Sultani.

Hivyo, alishauri kuwa kisheria kisiwa hicho si ardhi ya mtu (no man’s land). Kwa sababu hiyo na kwa sababu Zanzibar ndiyo yenye uhusiano wa karibu zaidi na kisiwa hicho, alimshauri Sir Lloyd Mathews aende katika kisiwa hicho haraka iwezekanavyo na akaweke bendera ya Zanzibar ili kukichukua na kukitangaza rasmi kuwa ni kisiwa cha Zanzibar.
 
KISIWA CHA LATHAM KUTANGAZWA RASMI KUWA CHA ZANZIBAR

Mbali ya ushauri huo wa Sir Arthur Hardinge, ambao unaonyesha ulipelekwa pia kwa Sultani, tarehe 17 Oktoba 1898, Sir Lloyd Mathews alipokea maelekezo kutoka kwa Sultani kuwa aende katika kisiwa cha Latham ili akapachike bendera ya Zanzibar na kukitangaza rasmi kisiwa hicho kuwa kiko chini ya mamlaka ya Zanzibar.

Kufuatia maelekezo hayo, Lloyd Mathews aliondoka Zanzibar tarehe 18 Oktoba 1898 kwa kutumia boti ya SS Barawa. Alifuatana na Captain Arthur Agnew, Port Officer wa Zanzibar na Dr. Alfred Andrew Spurrier, Medical Officer, wafanyakazi wa boti hiyo na vibarua wengine kadhaa. Saa 12 asubuhi ya tarehe 19 Oktoba, 1898 bendera ya Zanzibar ilipandishwa ikifuatiwa na saluti ya mizinga 21.
 
Aidha, nyumba ya chuma ilijengwa na bao kubwa la Tangazo lililosomeka “LATHAM ISLAND, FUNGU KIZIMKAZI UNDER ZANZIBAR SOVEREIGNTY” na pembeni ya ubao huo wa tangazo, maneno ya Kiarabu yaliandikwa ambayo yakisomeka kama ifuatavyo “ Seyyid Hamoud byn Mohamed byn Said wa Zanzibar”. Ofisa mmoja aitwaye Captain Baw na wasaidizi wawili waliteuliwa kuwa wasimamizi wa kisiwa hicho. Sir Lloyd Mathews alirejea Zanzibar na akaandika taarifa rasmi kumpelekea Sultani, Waziri Kiongozi na Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza.
 
MADAI YA UJERUMANI JUU YA KISIWA CHA LATHAM

Kwa mara ya mwanzo kabisa, Ujerumani ilizusha madai ya umiliki wa kisiwa cha Latham mnamo mwaka 1910. Madai hayo, hata hivyo, yalianzia mwaka 1909. Mnamo tarehe 23 Juni, 1909 Sir Edward Clarke alimuandikia Gavana wa Ujerumani wa Tanganyika akimueleza kuwa kuna taarifa kuwa wapo raia wa Uingereza wanaoishi kusini mwa Tanganyika ambao wanakwenda kuchukua samadi ya ndege (guano) bila ya ruhusa ya Serikali ya Zanzibar. Alimtaka Gavana asitishe vitendo hivyo mara moja.
 
Tarehe 6 Disemba, 1910, Gavana wa Tanganyika aliandika Waraka kwa Serikali ya Zanzibar akidai kuwa Ujerumani ndiyo yenye mamlaka juu ya kisiwa cha Latham. Katika kujenga hoja hiyo, Waraka huo ulinukuu zaidi vifungu vya mikataba baina ya Wajerumani na Waingereza ambayo ilitambua mamlaka ya Zanzibar. Kwa tafsiri ya mikataba hiyo, alidai kuwa Zanzibar haina mamlaka juu ya kisiwa hicho.

Mnamo tarehe 13 Aprili 1911, Sir Edward Grey alijibu Waraka huo kwa kuandika Waraka wa majibu kumpelekea Herr Von Kuhlmann wa Ofisi ya Gavana wa Tanganyika. Katika majibu yake, Sir Edward Grey alieleza hoja zifuatazo:
 
Kwamba kisiwa cha Latham kiliwekwa rasmi kuwa sehemu ya Zanzibar kuanzia tarehe 19 Oktoba 1898 na akafafanua kwa urefu juu ya kazi ya uwekaji wa bendera ya Zanzibar kulikofanywa na Sir Lloyd Mathews;

b. Alikumbusha kwa urefu mawasiliano yaliyofanywa katika mwaka 1900 baina ya Serikali ya Uingereza na nchi kadhaa ikiwemo Ujerumani juu ya pendekezo la kujenga minara ya kuongozea meli katika eneo la Zanzibar kikiwemo kisiwa cha Latham, Pemba Kaskazini na Chumbe. Alieleza kuwa Ujerumani ilikuwa moja ya nchi zilizotoa maoni kuhusu pendekezo hilo lakini haikuwahi kudai wala kuonyesha dalili ya kuwa Latham ni sehemu ya mamlaka ya Ujerumani wala kupinga mamlaka ya Zanzibar juu ya kisiwa cha Latham;
 
Alifanya uchambuzi wa mikataba hiyo na kuhitimisha kwa kueleza kuwa hakuna mkataba wowote kati ya hiyo ambayo imetoa mamlaka ya wazi kwa Ujerumani au Uingereza juu ya kisiwa cha Latham. Alimalizia kwa kuishauri Ujerumani, kama ina hamu ya kukimiliki kisiwa cha Latham, iwasiliane na Serikali ya Zanzibar ambayo inaweza kuzungumza juu ya suala hilo.

Serikali ya Ujerumani haikuwahi hata mara moja kujibu Waraka huo wa Sir Edward Grey na wala haikuwahi kuwasiliana na Serikali ya Zanzibar juu ya kisiwa hicho. Hatimaye iliwekewa kumbukumbu rasmi kuwa suala la hoja ya Ujerumani juu ya umiliki wa kisiwa cha Latham limefungwa rasmi.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…