HATUA ZA KIUTAWALA NA KISHERIA ZA SERIKALI YA ZANZIBAR JUU YA UMILIKI WA KISIWA CHA LATHAM
Kumbukumbu zinaonyesha kuwa Serikali ya Zanzibar iliendelea kukitumia na kukiendesha kisiwa cha Latham kwa shughuli mbali mbali. Miongoni mwa shughuli hizo ni utafiti wa ndege, kupanda miti, utafiti juu ya kima cha samadi ya ndege (guano) kama inatosheleza kibiashara au la.
Mbali ya shughuli hizo, viongozi kadhaa, akiwemo Sultani na British Resident, walitembelea Kisiwa cha Latham na taarifa za safari zao zimewekewa kumbukumbu. Mfano mzuri ni ziara ya British Resident ya tarehe 9 Machi 1951.
Mnamo mwaka 1959, Serikali ya Zanzibar ilikitangaza kisiwa cha Latham kuwa ni hifadhi ya ndege (bird sanctuary) kupitia Tangazo Namba 56 la 1959. Kwa mujibu wa kumbukumbu tulizoweza kuzitafiti, Tangazo hili bado halijafutwa au kurekebishwa na hivyo, kisheria, kisiwa hicho bado ni hifadhi ya ndege ya Zanzibar.