Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

JUZI imetimia miaka 20 kamili tangu Manchester United ilipofanya maajabu katika Uwanja wa Nou Camp kwa kuichapa Bayern Munich mabao 2-1 katika dakika za mwisho za pambano la fainali Ligi ya Mabingwa wa Ulaya.

Ni mechi inayokumbukwa mpaka leo. Kwa vijana wa kizazi hiki sio mbaya kukumbushwa kilichotokea.
 
Nou Camp yachaguliwa kuandaa

Dimba la Nou Camp linalotumiwa na Klabu ya Barcelona ya Hispania lilichaguliwa kuandaa pambano hilo katika kikao cha Kamati Kuu ya Uefa kilichofanyika jijini Lisbon, Ureno Oktoba 6, 1998. Mchakato wa kuchagua kiwanja cha mechi hii ulifanyika miezi minne kabla, Mei 1998.

Nou Camp ilishindana na Wembley, Uwanja wa Velodrome wa Marseille lakini Nou Camp ilichaguliwa.

Collina aongoza waamuzi
 
Uefa ilimchagua mwamuzi maarufu wa Italia, Pierluigi Collina kuwa mwamuzi wa pambano hilo. Collina alikuwa ameingizwa katika orodha ya waamuzi wa Fifa mwaka 1995 na mechi zake za kwanza za Ulaya zilikuwa msimu wa 1995–96. Kabla ya fainali hii, Colina alikuwa amechezesha mechi nane tu za Ligi ya Mabingwa Ulaya na tatu kati ya hizo alichezesha hatua ya makundi msimu huo ikiwemo mechi kati ya Barcelona na Bayern Munich Nou Camp Novemba 4, 1998.
 
Lakini pia aliwahi kuchezesha fainali za Olimpiki mwaka 1996 katika pambano kati ya Nigeria na Argentina. Aliwahi kuchezesha mechi mbili za makundi Kombe la Dunia mwaka 1998 Ufaransa. Katika pambano hili la United na Bayern Collina alisaidiwa na Waitaliano wenzake, Gennaro Mazzei na Claudio Puglisi huku mwamuzi wa nne akiwa Fiorenzo Treossi.
 
Keane, Scholes nje

Kuelekea pambano hili, Manchester United iliondoka England siku mbili kabla ya mechi ikitumia Uwanja wa Ndege wa Manchester Ringway, kisha wakatua uwanja mkubwa wa Heathrow jijini London ambapo walipanda ndege kubwa aina ya Concord kwenda Barcelona.
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…