TUMESHUHUDIA jinsi wanasoka kibao walioteka ulimwengu wa soka, miaka ya hivi karibuni, wakiamua kutundika daruga. Fernando Torres, Xavi Hernandez, Robin van Persie na Petr Cech wote wamesema basi, kwenye masumbwi tunasema wametupa taulo.
Wanandinga wote waliotajwa hapo juu, ni mastaa na kila mmoja katika nafasi yake. Wakali wa kupiga mabao kama Van Persie, walifunga. Wakali wa kudaka michomo kama Cech walidaka na watawala wa kiungo kama Xavi walitawala, ilimradi kila mtu alifanya yake
Mbali na hao, baada ya kuiongoza Man City kutetea ubingwa wake wa EPL, Kiungo David Silva, aliamua kutundika daruga, pia huenda akaamua kwenda kwengineko. Hawa hapa ni nyota wengine, ambao bado kidogo tu, wanaachana na soka.
‘El Guaje’ ni mmoja wa washambuliaji hatari zaidi, kuwahi kutokea katika ardhi ya Hispania. Ndiye mfungaji bora wa muda wote, kwenye timu ya taifa ya Hispania. Maisha ya soka ya David Villa Sánchez, inafurahisha masikio na kuburudisha moyo pia.
Alishinda kila kitu akiwa na jezi ya timu ya taifa na hata klabu.
Mhispania huyu alitwaa mataji kila alikocheza. Baada ya kutosheka na mafanikio yake katika ligi za Ulaya, alienda Marekani akajiunga na klabu ya New York City FC.
Baada ya kuendeleza moto wake katika ligi kuu ya Marekani (MLS), kila mtu alimtegemea angemalizia soka lake kwenye ardhi ya Donald Trump, lakini haikuwa hivyo, ameamua kuonja ladhaa ya soka la Japan. Lakini, huenda akainua mikono muda wowote.
Pamoja na ukweli tayari kila mtu anafahamu siku atakayotundika daruga, sio vibaya kukumbusha, Muargentina Carlos Tevez, bado ana msimu mmoja wa kuendelea kusakata kabumbu. Anaichezea klabu yake ya utotoni ya Boca Juniors.
Straika huyu, kama ilivyo kwa wachezaji wengi wa Amerika Kusini, amezunguka katika klabu nyingi kubwa za Ulaya na kwengineko. Huko kote hakutoka kapa, kwani ameshinda mataji mengi tu, ambayo tukianza kuhesabu hapa tunaweza kukesha.
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.