Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

KUTOLEWA GEREZANI BABU Baada ya Babu kumaliza kifungo chake, alitolewa gerezani mnamo saa nne za usiku na ilikuwa kwa njia za siri siri. Jambo ambalo si la kawaida. "BABU'S WEEK" Chama cha Hizbu kwa furaha ya kutolewa Katibu wake kifungoni kwa salama, kiliandaa mapokezi yake kwa sherehe kubwa kubwa. Sherehe hizo zilikuwa kwa muda wa wiki mbili, wiki moja zilifanywa Unguja na wiki ya pili zilifanywa Pemba. Kwa kusherehekea siku hio, Makao Makuu ya Chama na Matawi yake yote, Unguja na Pemba, mjini na mashamba, yalipambwa kwa mabendera na mataa ya kila rangi.

Sherehe hizo zilikuwa kwa kusomwa Maulidi, kwa Dhikiri, kwa magoma na hata kwa mashindano ya ngalawa. Babu akibebwa juu ya mabega ya wananchi na huku kukiimbwa "SOTE TWAMPENDA BAABU!". "Babu's Week" (wiki ya shereha za kufunguliwa Babu) ya Unguja ilimalizika kwa Hizbu kufanya karamu kubwa katika uwanja wa Bustani ya Seyyid Khalifa Hall (sasa ati inaitwa Karume House).

Karume House = jengo hilo linaendelea kutumika kama ni studio ya shirika la habari la zanzibar kwa upande wa televisheni
 
BABU NA FISADI YAKE YA MWISHO
Babu alirejea kutoka Pemba siku ya Jumaane kiasi cha saa mbili za usiku. Usiku huo huo, alikutana na kamati ya uchaguzi ya Chama. Kamati hiyo ilimkabidhi Babu orodha ya wagombea uchaguzi wa Hizbu katika Unguja kama walivyo teuliwa na majimbo yao kwa mjini na kwa mashamba. Babu baada ya kupokea orodha huo, naye alitoa orodha wa wagombea uchaguzi wa Hizbu kwa Pemba, naye akiwa ni miongoni mwao. Kamati ilifurahikiwa na matokeo yalivyokwenda vizuri kukhusu uteuwaji wa wagombea uchaguzi, Unguja na Pemba.
 
Siku ya pili yake, Jumaatano, Kamati Kuu ya Hizbu ilikutana. Babu alitoa ripoti yake ya Pemba na kuiarifu Kamati Kuu kuwa yeye ameteuliwa kuwa mgombea wa kiti cha Ziwani Pemba. Kamati Kuu ilifurahikiwa na matokeo yote yaliyotokea Pemba. Baada ya kumaliza hayo, Babu alisema: "Jana usiku nilipofika tu, nilikutana na Kamati yetu ya uchaguzi nao walinikabidhi orodha wa majina ya watetezi 26 (wagombea uchaguzi) "kama walivyo teuliwa na majimbo yao hapa Unguja".
 
Aliendelea kueleza, "Kutokana na namna kinavyoonekana Chama chetu na baadhi ya watu hapa na nje ya nchi kuwa ni Chama cha Kiarabu, nimeonelea bora safari hii tufanye mabadiliko katika kuwasimamisha watetezi wetu kwa uchaguzi huu ujao", alisema Babu. Katika kuendelea na maneno yake Babu alieleza kuwa mabadiliko hayo atakayo kuyaleta, anayaleta kwa ajili ya maslahi ya Chama. Babu alianza kwa kusema kuwa, "Safari hii, tumuondoe Sheikh Ali Muhsin katika jimbo la Malindi na tumpeleke katika jimbo la Tumbatu na aombwe Sheikh Nyakanga (aliyeteuliwa kuwa mtetezi wa jimbo hilo la Tumbatu), yeye safari hii apumzike asisimame.
 
Jimbo la Shangani, safari hii tumuweke Sheikh Juma Aley, pahala pake (yaani jimbo la Nungwi) tumpeleke Sheikh Muhsin Abeid. Sheikh Amirali AbdulRasool, yeye aondoke Shangani aende akasimame katika jimbo la Mlandege, na Sheikh Ibuni Saleh aondoke hapo Mlandege aende akasimame katika jimbo la Kikwajuni. Jimbo la Bumbwini safari hii tulipe Chama cha FPTU., (Fedaration of Progressive Trade Unions) ( chama hichi kilitumika wakati huo kuwa ni kichakachawatoro kwa wakubwa na wengi wa wafuasi wa kilicho dhihiri baada yake kuwa ni Umma Party, yaani makomredi) wao wenyewe watamteuwa anaefaa kusimama huko. Sheikh Haji Muhammadi aombwe safari hii apumzike."
 
Jambo la kustaajabisha juu ya mapendekezo hayo aliyoyaleta Babu ni kuwa yeye yeye Babu baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa mwanzo wa 1957, ndiye alieleta mapendekezo katika Kamati Kuu ya Chama ya kutaka uwezo wa kuwateuwa wagombea wa uchaguzi uwachwe katika mikono ya Matawi na majimbo ya Hizbu wenyewe. Kamati Kuu isiwe na uwezo wa kuwateulia wagombea uchaguzi, ila iwe na uwezo wa kutoa nasaha tu pindi ikihitajika.

Mpango huu ulikubalika na ukawa unatumika tokea wakati huo, hata ukaweza kuzuiya mwana kamati, Bwana Rutti Bulsara kutokuteuliwa na jimbo la Mkunazini na matokeo yake yalimpelekea Bwana Bulsara kukiacha Chama cha Hizbu. Baada ya miaka sita tu Babu huyo huyo na bila hata ya kushauriana na wenziwe na kutaka pafanywe mabadiliko ameleta mapendekezo kinyume kabisa na yale aliyoyaleta mwanzo na yakawa yamekubalika na yakawa yanatumika.
 
KIPI KILICHO MPELEKEA BABU KUCHUKUA KHATUA KAMA HIZO
Kama nilivyotangulia kusema, Babu alikuwa na dhamiri zake ambazo alifikiria ataweza kuzitekeleza kwa kukitumilia Chama. Alipoona kuwa kila alilojaribu kulileta, halikuweza kufuzu, ndipo alipochukua khatua kama hizo na katika wakati kama huo. Babu alikhadaika kwa maneno aliyokuwa akiambiwa na hao wafuasi wake wajiitao "progressives" wakati alipokuwepo kifungoni.

Maneno waliyokuwa wakimpelekea baada ya wao kuwa wakipita wakitangaza propaganda dhidi ya uwongozi wa Hizbu, ni kuwa, "Umma wote wa Hizbu upo nyuma yako na kama utavyoamua baada ya kutoka kifungoni, ndivyo na wao watavyofuata. Ukiamua kutoka katika Chama, basi Umma utakufuata na ukiamua kubakia, nao utabakia na wewe".
 
Kutokana na mapokezi aliyofanyiwa Babu alipotolewa gerezani, aliona yote aliyokuwa akiambiwa na hao watu wake, yalikuwa ni mamneno ya hakika. Vilevile kulikuwepo na mipango ya chini kwa chini baina ya wenye kujiita "progressives" waliyokuwemo katika upande wa Hizbu na waliyokuwa wakijiita "progressives" upande wa AfroShirazi ya kutaka pindi wakiweza kushinda katika viti vyao vya uchaguzi waweze kushirikiana katika kuleta pendekezo litaloweza kupelekea kuanguka kwa Serikali, ili waweze kupata nafasi ya kufanya Serikali nyengine itayo kuwa na mwenendo wautakao wao, ati wa ki"progressive". Na hayo yangelimfurahisha China iliyokuwa ikimpa Babu mshahara uliokuwa kasoro kidogo na wa Mfalme. Babu akipata kutoka China kila mwezi Shs.15,000 safi na Mfalme akipata Shs. 20,000 ghafi.
 
Hayo yalipokuwa hayakuweza kupatikana, ndipo Babu alipojitoa katika Chama kwa kufikiria kuwa umma wa Hizbu utamfuata pamoja naye. Alipoona hayakuwa kama hivyo, ndipo alipoanzisha chama chake cha Umma Party na baadae kujiunga pamoja na wageni kama Okello na Mfaranyaki na wenziwe katika mavamizi ya nchi yake na kuiondoa Serikali ya halali iliyokuwa imechaguliwa na Umma kwa kutumia haki yao ya demokrasi ya "One Man One Vote".
 
UCHAGUZI WA JULAI 1963
Huu ni uchaguzi wa mara ya nne kufanyika Zanzibar katika muda wa miaka sita (1957 1963). Uchaguzi huu ulifanyika baada ya muda mfupi tokea kupatikana Serikali ya Ndani (Internal Self Government) na tokea Babu kutoka katika chama cha Hizbu. Uchaguzi ulikuwa wa viti vyote 31 vya Baraza ya Taifa (National Assembly) na ulifanyika kwa usalama. Matokeo ya uchaguzi huo ilikuwa ni kupata ushindi Muungano wa Hizbu na ZPPP kwa kupata viti 18 na AfroShirazi kupata viti 13.
 
NYERERE ANASEMA WAKOLONI WALIPENDELEA KUIACHA SERIKALI YA ZANZIBAR MIKONONI MWA HIZBU

Kweli, Waswahili wanasema, "Apendae, chongo huita kengeza". Katika uchaguzi huo wa "Mtu Mmoja Kwa Kura Moja" (One Man One Vote), katika viti 31 Muungano wa Hizbu na ZPPP ulipata viti 18 na AfroShirazi walipata viti 13. Sasa Mwalimu nani aliyepata viti vingi kuliko mwenziwe hapo hata astahiki kuendesha serikali? Au ulitaka serikali wapewe AfroShirazi kwa hivyo viti vyao 13, ndio ungeona kuwa imefanywa haki?!

Mwalimu Nyerere anaelewa vizuri kuwa nidhamu za uchaguzi alizokuwa akizitumia Muingereza katika nchi alizokuwa akizitawala ni sawa na nidhamu anazotumia katika chaguzi za nchi yake. Nidhamu za Muingereza juu ya uchaguzi ni zenye kutizama mtetezi aliyepata kura nyingi zaidi kuliko mshindani wake katika lile jimbo lake la uchaguzi. Hazitizami hata chembe juu ya wingi wa kura zilizo patikana katika chama kwa jumla.
 
Kura walizopata Labour Party katika uchaguzi uliopita ni nyingi sana kuliko kura walizopata Chama cha Conservative lakini, Labour hawakuweza kuunda serikali kwa sababu viti walivyopata Conservative ni vingi kuliko walivyopata Labour Party. Sasa mbona Labour hawasemi kuwa Malikia amewapendelea Conservative? Na hivyo, ndivyo ilivyokuwa katika chaguzi zilizofanyika Zanzibar.
 
Wingi wa kura kwa jumla wamepata AfroShirazi ni hakika lakini hawakuweza kupata wingi wa viti. Ina maana kuwa katika baadhi ya majimbo, Hizbu na ZPPP, wameweza kukubalika na Umma kuliko walivyokubalika AfroShirazi. Na katika baadhi ya majimbo, AfroShirazi wameweza kukubalika zaidi kuliko Hizbu na ZPPP na hiyo ndiyo demokrasi ya kweli. Lakini ni majimbo mengi zaidi, (nayo ni 18) yaliyochaguwa ZNP/ZPPP kuliko yaliyochaguwa ASP (nayo ni 13).
 
MKUTANO WA KATIBA YA UHURU.
Muda mfupi baada ya kumalizika kwa uchaguzi wa Julai 1963, Serikali ya Kiingereza ilizialika pande zote mbili yaani Upande wa Serikali ya ZPPP/ZNP na Upande wa Upinzani wa AfroShirazi kuhudhuria kwenye mkutano wa mazungumzo ya Katiba ya Uhuru wa Zanzibar. Kabla ya pande mbili hizo kwenda Uingereza kwa mazungumzo hayo, Balozi wa Kiingereza wa Zanzibar Sir George Mooring, alianzisha mkutano baina ya Serikali na Upinzani hapo hapo Zanzibar kwa kurakhisisha baadhi ya mambo
 
Mkutano huo uliendelea kwa muda na palikuwepo mashirikiano mazuri baina ya pande zote mbili. Wakati ulipowadia, wajumbe wote wa Serikali na wa Upinzani walikwenda Uingereza na huko walizungumza kwa kufahamiana na kukubaliana katika kila kifungu bila ya kutokea pingamizi za namna yoyote. Hii ilikuwa ni ishara njema. Lakini jee hakika ya mambo ndivyo ilivyokuwa?

Kwa kuvamiwa nchi mwezi tu baada ya uhuru huwenda mtu akaunganisha hili na lile akatoka na natija kuwa mipango ya kuivamia Zanzibar ilikuwa tayari kabla ya Uhuru, na ndio maana ikawa rahisi katika mkutano huu kukubaliana 31 bila ya pingamiza. Kinyume na kawaida ya viongozi wa AfroShirazi. (kama ilivyothibitisha Taarikh). Wao siku zote wakisema "zuiya"!
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…