(2) Maalim Harun Ustadh
Wakati tulipofungwa gerezani, Maalim Harun alikuwa akikurubia miaka 70 na siha yake tokea kabla ya kufungwa haikuwa nzuri kutokana na umri wake na maradhi aliyokuwa nayo, presha na ugonjwa wa miguu. Lakini kwa kuwa alikuwa akipata matibabu yaliyokuwa bora na vyakula vyenye kutengeza viwiliwili vya binadamu, na alikuwa na uhuru wake ekenda huku na huku aliweza kuishi kwa uzuri.
Kwa kufungwa na kuyakosa yote hayo, na juu yake kufanyishwa kazi zisizokuwa kadiri yake kutokana na umri wake na maradhi aliyokuwa nayo, kila siku uchao alikuwa akizidi kudhoofika. Mambo yalipomzidia, alianza kukohoa na kutoka damu katika makohoo.
Baadae alianza kuvimba miguu na uso na kupata shida ya kuvuta pumzi. Bwana Mganga wa gereza la Langoni, alitoa pendekezo la kutaka apelekwe Maalim Harun hospitali kuu kwa kukutana na Daktari mkuu, Muhidini Khamis Kwangwati mkuu wa gereza hilo la Langoni na Kinu Moshi kama kawaida yake alipinga na alimuacha Maalim Harun hapo hapo gerezani akiatilika na maradhi
. Alipofika hali ya kuchungulia kaburi kwani alikuwa hata akisema, maneno hayatambulikani sawa sawa na kutoweza hata kujisaidia mwenyewe, ndipo hapo alipoondolewa na kupelekwa katika hicho kihospitali cha Makao Makuu ya Magereza, Kiinua Miguu. Na huko haukuchukua muda ila naye aliiaga dunia kama alivyoiyaga mwenziwe Mzee Mbaba.