Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Twala amesema kwa kusikia hukumu hiyo, ndiyo hapo aliweza kushusha pumzi. Kwani kila alipokuwa Mzee akisema alikuwa akiyaona mauti mbele ya macho yake. Aliendelea kusema kuwa akiona wazi kuwa yale yaliowafika Othaman Shariff na Saleh Saadalla ndio hayo hayo yatakayo mfika yeye. Alisem, akijuwa kuwa ikiwa atapata rehema basi ni kumalizikia gerezani, ambako alikuwa na hakika kuwa huko hakuna mwisho mwema. Alisema, niliondoka hapo siku hiyo sina raha wala furaha.
 
MWISHO WA TWALA
Kuondolewa AbdulAziz Twala katika Wizara ya Fedha, na kupelekwa kwenye Wizara ya Afya, ndio kulikuwa kumalizika kwake. Twala alisema kuwa alipopelekwa Wizara ya Afya, Waziri wake mdogo alikuwa Rashid Abdalla (Mamba). Twala ameniambia kuwa walikuwa na dasturi ya kukutana kila asubuhi kwa ajili ya kuzungumza juu ya kazi zao.

Siku moja, amesema Twala, alimuona Rashid Abdalla amekawia kufika ofisi. Mpaka kiasi cha saa nne ndipo alipoingia na alipoingia alikwenda moja kwa moja mpaka ofisi ya Twala. Alipofika, alimwambia Twala, "Mheshimiwa, tokea sasa hivi, mimi ndiye Waziri wa Afya na wewe funga virago vyako wende nyumbani kwako. Kila kilicho chako chukuwa mwenyewe na kila cha Serikali kiwache. Hata motokari usichukuwe tena. Haya ndiyo niliyoambiwa kutoka State House, unalo suala lolote waulize wenyewe".
 
Twala, ameniambia kuwa hakustaajabu kwa kuambiwa maneno hayo kwani akiuelewa uzuri mwendo wa Serikali yake, lakini juu ya hivyo alitaka kuzidi kuhakikisha juu ya maneno hayo. Kwahivyo alipiga simu State House (Ikulu) na alipouliza jawabu ilikuwa, "Kama alivyokueleza Mheshimiwa Rashid Abdalla ndivyo hivyo hivyo. Pack and go"! Twala amesema kuwa, alifunga funga, na alimuachia ufunguo wa gari Waziri mpya wa Afya, na alishika njia kwenda zake nyumbani akiutwanga wa fisi. Salama wakati huo, alikuwa akikaa Mnazi Mmoja ambapo palikuwa karibu sana na hiyo iliyokuwa ofisi yake.
 
Baada ya siku mbili tatu tokea kutolewa katika uwaziri, alijiwa nyumbani kwake na Mkuu wa Usalama Ibrahim Makungu na alimwambia, "Nimekuja kukutaka unikabidhi bastola pamoja na risasi ulizokuwa umepewa, na pia unikabidhi paspoti yako ya kidiplomasi". Twala amesema, aliingia ndani na akamkabidhi vyote hivyo. Haukupita muda baada ya hapo ila alimuona Mkuu wa Gereza la Mateso ("Kwa Ba Mkwe") Mheshimiwa Mandera amemfikilia nyumbani kwake kiasi cha saa 10 za jioni. Mandera alimwambia Twala, "Wazee wenzako wamenituma nije kukuchukuwa ili mwende mkazungumze kuhusu maombi yako ya paspoti ". Twala baada ya kunyan'ganywa paspoti ya kidiplomasi, alikwenda kuomba paspoti ya kawaida katika Idara ya Uhamiaji.
 
Twala ameniambia kuwa kwa kuja Mandera na kumwambia maneno hayo alihisi kuwa hakuna salama. Aliingia ndani na alimzungumzia mkewe khabari hizo. Wakati huo mama yake mzazi Twala alikuwepo nyumbani, kwani mkewe Twala alikuwa mja mzito na akitarajia kujifungua wakati wowote. Twala baada ya kumzungumzia mkewe, alitoka na kumfuata Mandera. Aliingia katika gari ya Mandera na baada ya muda mdogo, Twala amesema, alijiona amefika kwenye gereza la "Kwa Ba Mkwe". Safari yake ya kukutana na wazee wenzake ilimalizikia hapo.
 
Twala aliniambia kuwa yeye alibahatika hakuteswa kwa namna yoyote zaidi ya kuwekwa humo bila ya kuwa na makosa yoyote. Baada ya kukaa katika gereza hilo kwa muda, Twala alifungwa kifungo cha miaka 10 gerezani kutoka taarikhi 3 Mei, 1969. Kutokana na huko kufungwa kwake, ndio tukawa pamoja na kunihadithia haya niyaelezayo katika kijitabu hiki. 62 Ilikuwa ni kawaida, kila baada ya muda wakiletwa wafungwa waliyokuwa wakiitwa, "wafungwa wa kisiasa" kutoka gereza la "Kwa Ba Mkwe". Wakati mmoja katika jumla ya wafungwa waliyoletwa,
 
alikuwa Idrisa Majura. Idrisa na Twala wakifahamiana sana na kwa hakika walikuwa marafiki tokea walipokuwa wakijifunza uwalimu katika Chuo cha Uwalimu huko BeitelRas, Unguja. Idrisa alijiunga pamoja na sisi na tulikuwa tukikaa pamoja baada ya kumaliza kazi zetu na tulikuwa hata tukila pamoja yaani mimi, Twala na yeye Idrisa. Baada ya muda, Twala alileta shauri katika baraza yetu ya kutaka tufanye mipango ya kutoroka kutoka gerezani.
 
Tuliizungumza kwa urefu sana mipango hiyo, na juu ya yenye kuwezakana kutendeka na yasiyowezekana kutendeka kutokana na hali ilivyokuwa wakati huo. Mimi kwa upande wangu, si kama nilikuwa na woga wa kufanya hayo, bali nilikuwa nikipinga baadhi ya mambo ambayo nikiyaona hayaingii katika mizani ya kuweza kufuzu katika mipango hiyo. Kutokana na hivyo, Twala aliniambia, "Nakuona woga wa kiHizbu umeshakuingia. Lakini nakwambia kuwa sisi hatutokubali kubakia hapa tuwe tunauliwa kidogo kidogo. Tutatoka na lolote na liwe". Tokea siku hiyo, niliwaona kidogo wakiniepuka epuka katika baadhi ya nyakati.
 
Siku moja asubuhi, niliwaona wote wawili wamesimama katika msitari wa wanaotaka kuonana na Bwana Mganga. Kwa hakika haikunipitikia kitu. Niliona ni mambo ya kawaida, kwani wafungwa hufanya mipango kama hiyo angalau wapate mapumziko japo madogo. Miye na wafungwa wenzangu wengine tulipelekwa makondeni kulima kwa siku ile. Tulipokuwa makondeni tukilima kiasi cha saa sita za mchana, tulisikia kipyenga cha kutukusanya pamoja. Mara niliwaona askari waliokuwa wakituchunga wakino'gonezana. Baada ya sote kuhisabiwa na kuonekana tumetimia katika hisabu yao, tuliongozwa na kurejeshwa kambini Langoni.
 
Wakati huo tulikuwa tukifanyakazi sehemu za Kinu Moshi. Tulipofika Langoni, tuliwakuta askari wa polisi na majibwa wao, pia walikuwepo askari wa kijeshi, na Mandera naye pia alikuwepo. Roho zilitusituka na kutupiga paa! Baada ya kuhisabiwa na mchungaji mwenye dhamana ya kotagadi, tulitiwa ndani moja kwa moja, na hapo hapo tulipewa chakula, baada ya kula tulitiwa ndani ya mabanda yetu bila ya hata kwenda chooni. Kila mchungaji alikuwa ameghadhibika kuliko mwenziwe. Wapishi na baadhi ya wachungaji walituno'goneza kuwa Twala na Majura wametoroka.
 
Loo! Niliingiwa na jamba jamba kwa mambo mawili. Kwanza, kwa vile ilivyokuwa kila wakati tukikaa pamoja, tukizungumza pamoja, na hata tukila pamoja; basi nalihisi huenda wakubwa wakafikiri kuwa labda mimi naujuwa huo mpango wao wa kutoroka gerezani. Na ndivyo ilivyofikiriwa. Pili, nilikhofia kuwa ikiwa hawatofuzu katika mipango yao hiyo ikatokea kukamatwa, wasije kwa mateso wakafika kusema kuwa na mimi nilikuwa pamoja nao.
 
Mradi nilikuwa si hadhir khasa kwa namna ya serikali yenyewe ilivyokuwa. Kufika kiasi cha saa moja ya usiku, niliona mlango wa banda nililokuwa nikilala umefunguliwa ghafla, na Sajin Buesha amesimama mlangoni na kusema, "Aman Thani! Toka nje na kirago chako". Roho ilinipiga paa! Niliona kishindo hicho kimeshanifika. Lakini, nilijikaza kiume, nilitoka huku nikionesha kama sina khofu ya lolote.
 
Nilipofika 'kotagadi', niliikuta gari ya magereza. imefunikwa turubali. Gari hii ilikuwa imekuja kutoka Makao Makuu ya Magereza pamoja na wachungaji wa magereza na ofisa wao, kijana wa kiZanzibari mwenye asili ya Kihindi, akiitwa Hassanali. Mpaka wakati huu nishakuwa ninayajuwa magereza yote na wachungaji wote, mote humo ni mwangu; si mgeni tena! Nilipofika tu, nilitiwa katika hiyo gari moja kwa moja mpaka katika vyumba vya kunyongewa (condemned cells). Huko nilimkuta kijana mdogo wa kiMakunduchi aliyekuwa mchungaji sehemu hiyo.

Kijana huyo, alisikitika kwa kuniona nimeletwa katika sehemu hiyo, na neno alilolisema kwangu ni, "Inshaallah, atawajaalia waweze kutoka katika nchi hii kwa salama, na nyote mlodhulumiwa kwa kufungwa bila ya kosa lolote, Mwenyezi Mungu atakutoweni bila ya wao kupenda".
 
Nilistaajabu kumsikia kijana mdogo kama huyo kuweza kusema maneno kama hayo, na khasa kwa vile alivyokuwa ni mfanyakazi katika serikali ya mavamizi katika wakati huo na pahala kama hapo. Langu mimi lilikuwa ni kuitikia, AMIN. Sikuwekwa sana katika sehemu hiyo, ila nilimuona Sajini wa magereza akifuatana na askari wake wawili (wachungaji) wamenitokea na walipofika tu bila ya kunambiya lolote, huyo Sajini alinitia pingu za mikono na niliongozwa kutoka hapo Makao Makuu ya Magereza hadi kwenye gereza la "Kwa Ba Mkwe", "Mlango wa Nyuma". Huko nilimkuta mwenyewe bwana Mandera akinisubiri. Mandera aliniambia kama hivi:
 
"Aman, unajua kwanini ukaletwa hapa?" Nilimjibu, "Sijui". Aliniambia, "Unajua kuwa Twala na Majura wamekimbia kutoka gerezani?" Nilimjibu, "Najua kwa kuwasikia wachungaji wetu wakizungumza hayo baada ya sisi kurejeshwa kambini". Aliniambia, "Basi umeletwa hapa, kwa ajili wewe ni wenzako sana Twala na Majura. Kwahivyo tunatumai utaweza kutwambia, wapi tutawapata. Hapana shaka wewe utaweza kuijuwa uzuri mipango yao". Nilimwambia Mandera, "Unadhani kuwa mimi napenda kuwepo gerezani? Ikiwa nikiijuwa mipango yao ya kutoroka gerezani, basi kwanini na mimi nisiwe pamoja nao? Au wewe unadhani kuwa Twala na Majura wataweza kuniamini mimi kiasi cha kuambizana siri kubwa kama hizo? Vyovyote itavyokuwa, mimi ninazo sababu za kutowaamni wao, na wao vilevile hapana shaka wanazo sababu za kutokuniamini".
 
Nilipokuwa nikimueleza Mandera haya, mara alikuja mmoja katika wachungaji na kunon'gona na Mandera, na hapo hapo Mandera aliondoka na alimpa amri huyo mchungaji anipeleke kwenye chumba cha mahabusi. Nilipotiwa ndani ya chumba hicho, nilimkuta mtu, kwa hakika alikuwa hayupo duniani hayuko akhera! Kwa jinsi alivyoteswa, alikuwa akikoroma tu. Uso wake wote umevimba na umepasuka pasuka na madamu yamemkaukia mwilini mwake
 
Alikuwa hawezi kusema, hawezi hata kutukusika. Baada ya siku tatu, usiku na mchana ndipo nilipoweza kumtambuwa, kwanza kwa kukisia tu, baadae kwa kuwauliza hao wachungaji wa gereza hilo ndipo nilipomjuwa kwa hakika. Bwana huyo tulikuwa tukijuwana kwa miaka mingi sana, kabla ya hata kuingia kwa mambo ya siasa Zanzibar. Siku za siasa, Bwana huyo, alikuwa miongoni mwa makatibu wa matawi ya Hizbu na alikuwa mpenzi wa kweli wa HizbulWattan na nchi yake. Lakini, kwa jinsi alivyoteswa katika gereza hilo, nilishindwa kumtambua mpaka nilipoambiwa. Haukuchukuwa muda mkubwa toka kuwa naye pamoja humo ndani ya chumba ila siku moja katika nyakati za asubuhi, Mwenye Enzi Mungu alichukuwa kiumbe chake, akiwa ni mwnye kudhulumiwa na serikali ya mavamizi.
 
Walipomuona ameshakufa, walimbeba kitikiti, mmoja amekamata mikono na wapili miguu utadhania gunia la muhogo. Binaadamu anafungwa, anateswa, anaachwa afe kisha anabebwa kama mzoga. Haya yamefanywa na wataka maendeleo na wa waondoa dhulma! Mzee huyo akiitwa Mzee Mwinyi, yeye ni mtu wa sehemu ya Shakani au Maungani. Hapo katika miaka ya nyuma akiishi mtaa wa Miembeni, Unguja. Baada ya mimi kutolewa gerezani 1972, nilisikia kuwa mzee huyo baada ya kutolewa maiti kwenye hilo gereza la "Kwa Ba Mkwe", alipelekwa hospitali kuu na waliarifiwa watu wake baada ya kuwepo hapo hospitali kwenda kumchukuwa maiti wao. Walimpeleka hospitali ionekane kwamba kafia huko! Mimi niliwekwa katika chumba hicho cha gereza la "Kwa Ba Mkwe" mpaka walipopenda wenyewe walinitoa na kunirejesha Langoni kuendelea na kifungo changu.
 
Kwa hakika Bwana AbdulAziz Twala alinizungumzia mambo mengi kukhusu mwendo wa Serikali yao ilivyokuwa ikiendeshwa. Mengine naona taabu hata kuyaandika. Yote alionieleza yanathibitisha tulivyokuwa tukiamini tangu awali, kuwa hakukuwa na serikali ila kilichokuwepo ni gengi la wauwaji na wanyan'ganyaji haki za watu, toka majumba, mashamba na mpaka wake, watoto na ndugu za watu.
 
Back
Top Bottom