Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Ikiwa Raisi wa nchi alifika kuweka hashaakum, kuwadi wa kulipwa mshahara kutoka katika fedha za nchi kwa ajili ya kumletea wanawake wa kufanya nao uchafu, basi serikali hiyo, itakuwa na insafu na thamani kutoka wapi?!! Kuthibitisha kuwa wakubwa wote wa serikali hiyo walikuwa ni watu wa aina hiyo hiyo ya mkubwa wao Mzee Karume basi baada ya kufa Karume, kuwadi huyo hakupoteza kazi yake bali alitunukiwa wadhifa mkubwa na kupewa cheo cha udhamini wa Jeshi la Wanamaji katika kisiwa cha Pemba. Hivi ndivyo wanavyo tunzana na kuhifadhiana!!
 
KWANINI MWALIMU NYERERE ALIKATAA KUWAPELEKA ZANZIBAR WATUHUMIWA WA KESI YA UKHAINI?

Alipouliwa Rais wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar, Abeid Amani Karume, Wazanzibari wengi walikamatwa na kutiwa viziwizini vya Magereza ya Zanzibar na ya Tanzania Bara. Wazanzibari waliyotuhumiwa zaidi kwa mauwaji ya Karume, walikuwa ni hao wajiitao, "progressives" au makomredi. Wao, walibakishwa viziwizini kwa muda mkubwa baada ya Wazanzibari wengine kuachiliwa huru. Baada ya muda tokea kuwekwa humo viziwizini, Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar iliwafungulia mashitaka watuhumiwa wote waliyokuwepo Zanzibar na waliyokuwepo Bara. Lakini, inasemekana kuwa Mwalimu Nyerere alikataa kuwapeleka Zanzibar watuhumiwa waliyokuwepo katika magereza ya Tanzania Bara.
 
Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar, walipoona Mwalimu amekataa kuwapeleka Zanzibar watuhumiwa waliyokuwepo Bara kuhudhuria katika mashitaka yao, waliendelea na mashitaka na waliwapeleka Mahakamani watuhumiwa waliyokuwepo katika magereza ya Zanzibar. Mashitaka yalichukuwa muda mkubwa, mwisho Mahakama yalitoa uwamuzi wake juu ya watuhumiwa wote wa Zanzibar na wa Bara (ambao walihukumiwa bila ya wenyewe kuhudhuria Mahakamani). Hukumu iliyotolewa na Mahakama hayo ilikuwa, wengine wapewe adabu ya vifo na wengine wafungwe gerezani kwa vifungo vya muda mbali mbali.
 
Miongoni mwa waliohukumiwa vifo ni huyo mkuu wao "progressives", Abdulrahman Babu. Sisemi kuwa Mahakama hayo na Mahakimu hao waliyoendesha mashitaka hayo walikuwa ni wenye kufaa au wenye ujuzi uliyokhusika na sheria, hashaa! Sote tukijuwa kuwa Mahakimu hao hawakuwa na ujuzi wowote juu ya mambo ya sheria, bali tu walikuwa na ujuzi wa kuuza samaki wakavu na kushona kofia za viuwa. Lakini, kwa vile hao wahukumiwa, wao wenyewe ni washiriki katika kuleta hiyo serikali ya mavamizi, na kwa kiasi fulani walikhusika na nyendo za seikali hiyo ambayo matokeo yake ndiyo kuwepo kwa Mahakama kama hayo na Mahakimu kama hao, kwahivyo, washitakiwa hao kuhukumiwa na Mahakimu kama hao itakuwa wanafaidika kwa matunda waliyoyapanda kwa mikono yao wenyewe
 
Mwalimu aliona ndivyo kuwapeleka Zanzibar Othman Shariff, Abdalla Kassim Hanga, Idrisa Abdalla Majura, Bibi Titi Mohammed, Kamaliza, Chipaka, (hao watatu wa mwisho ni Watanganyika) bila ya kujuulikana makosa yao au kuhukumiwa na yoyote. Nyerere huyo huyo akiwa ni mwalimu wa mipango aliona ni busara kutowapeleka hao wajiitao, "progressives" waliyokuwemo ndani ya mikono yake na waliyokuwa wakitakiwa na Serikali yake ya Mavamizi ya Zanzibar kwa kumuuwa aliiyekuwa Makamo Raisi wake Makamo Raisi wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Jee, haya ni bure bure tu! Haiwezi kuwa! Lazima lipo, lakini ikiwa si leo, kesho na ikiwa si kesho, keshokutwa; bali ikiwa hata si mwaka huu, miaka ijayo. Lakini lazima siku moja ukweli utajichomoza.
 
Vyovyote vile ilivyo lakini, Karume alikuwa ni Rais wa Zanzibar na Makamo wa Kwanza wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Afike kuuliwa, na waliyo tuhumiwa kuwa ndio wauaji wamekamatwa na kuwepo katika mikono ya Serikali, kisha wakahukumiwa na pakatolewa hukumu juu ya washitakiwa hao, na baada ya hukumu wakaachiliwa huru kama kwamba hapana lililotendeka! Oh!, Kweli hayo?!! Ni hakika ingelikuwa kauliwa mwanachama tu wa ASP basi mtuhumiwa huyo angelikiona cha mtema kuni, leo kauliwa Raisi wa Nchi ndio imekuwa si chochote si lolote!
 
Si hayo tu yenye kuwasangaza wananchi wa Zanzibar bali yapo na mengineyo. Lishangazalo zaidi ni kuwa huyo aliyetajwa na ikakubalika kutokana na mashtaka yaliyokuwa yakiendeshwa kuwa ndiye aliyekuwa mwongozi wa hayo machafuko yaliyotendeka nchini (Zanzibar) katika taarikh 7 April, 1972 na kumalizikia kwa kuuawa Rais wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar awe ameruhusiwa bila ya viziwizi vyovyote kuondoka na kurejea katika nchi wakati wowote aupendao. Si hayo tu, bali Serikali hiyo hiyo iliyomuhukumu kifo, ikawa inamualika kushiriki katika mikutano yenye kufanywa katika nchi, akiingia na kutoka maridhawa!!
 
NILITAKIWA NITOKE NCHINI
Mimi, muandishi wa kijitabu hiki, baada ya muda wamiaka 20 toka kutoka nchini naliomba niruhusiwe kuizuru nchi yangu. Nchi nilyozaliwa mimi na wamezaliwa wazee wangu wawili. Kwa shida niliruhusiwa kwa kupewa muda wa miezi mitatu kukaa katika nchi! Kwa kupewa ruhusa hiyo, taarikhi 9 Januari, 1992 nilizuru Zanzibar na 18 Februari, 1992 nilirejea katika masikani yangu, Dubai. Baada ya miezi sita, yaani taarikh 9 Agosti, mwaka huo huo wa 1992, nilikwenda tena Zanzibar na wakati huo nilidhamiria kukaa kwa muda wa miezi mitatu kwa kuendelea na mipango ya miradi yangu ya ukulima na ufugaji niliyo kusudia kuifanya.
 
Niliambiwa nilipofika kiwanja cha ndege siku nilioingia nchini, kuwa ikiwa nitataka kukaa nchini kwa muda zaidi, nenda Idara ya Uhamiaji nikaombe kuongezewa muda. Baada ya mwezi mmoja, nilikwenda huko Idara ya Uhamiaji kutaka niongezwe muda wa kukaa. Nilipofika, walinizuilia paspoti yangu na kisha nikaambiwa nikaonane na "boss". Nilipelekwa mpaka kwa huyo "boss" anaeitwa Ali Daud. "boss" baada ya kunitilia mijiti hii na hii, aliniambia, "Njoo keshokutwa kwani Boss leo hayupo kenda mkutanoni DaresSalaam". Nilimuuliza huyu boss, "Kwani pana jambo gani?" Alinijibu, "boss anataka kukuona". Nilinyamaza na niliondoka.
 
Ilipofika hiyo keshokutwa niliyoambiwa, nilifika Idara ya Uhamiaji na safari hii nilipelekwa kwa "boss" mwengine, Himid Yusuf Himid. Huyu ni kijana mdogo, Mzee wake tulikuwa tukifahamiana sana. Juu yakuwa tulikuwa na tafauti zetu kukhusu msimamo wa fikra za kisiasa, lakini tulikuwa tukihishimiana na tukisikilizana. Nilipofika ofisi ya kijana huyo Himid, aliniambia, "Mambo yako bado hayajamalizika, ikiwa utaweza, kusubiri hapo nje au unaweza kwenda na kurejea kiasi cha saa sita za mchana".
 
Niliporejea mnamo saa sita, aliniuliza, "Ndege ya Arabuni inaondoka hapa siku gani?" Nilimwambia, "Inategemea ndege gani uitakayo, kwani zipo ndege mbili zinazo kwenda Arabuni, na kila moja inayo siku yake na wakati wake". Aliniambia, "Hiyo unayo safiria wewe". Nilimwambia, "Inaondoka hapa kuelekea Dubai kila siku ya Jumaapili asubuhi saa tatu". Baada ya kumjibu hivyo, aliniambia, "Nifuate!" Nilimfuata mpaka ofisi nyengine na huko alimpa kijana aliyekuwa akifanyakazi sehemu hiyo pasipoti yangu na alimwambia, "Mpe muda wa kukaa Zanzibar mpaka Jumaapili tarehe 3 9 92 na muuandikie, 'Final Extension'." Nilimuuliza huyo kijana Himid, "Kwa nini yakawa yote haya kwani nimefanya jambo gani katika nchi hata ikawa nanyimwa kupewa muda zaidi, na kufika hadi kuondolewa katika nchi?" Jawabu aliyonijibu na huku anakwenda zake, "Huo ndio uwamuzi uliyofikiwa".
 
Nilinyamaza na nilingojea pasipoti yangu nilipoipata niliondoka na kwenda kutenegeneza safari. Siku hiyo ilikuwa siku ya Ijumaa taarikhi 1 8 92. Utaona kuwa nimepewa muda wa kasoro kuliko saa 36 niondoke katika nchi yangu niliyokuwa nimezaliwa! Bila ya kuambiwa nimekosa nini. Wakati huo nilikuwa nimefuatana na mwenzangu mmoja. Yeye alihuzunishwa na uwamuzi uliyotolewa dhidi yangu na aliniuliza, "Kwa nini yakatokea yote haya?" Nilimwambia, "Usidhanie kuwa nimefanya lolote kinyume na sheria katika ukaaji wangu hapa. Sikufanya hata chembe, lakini simba ni simba hata akikonga. Akitokeza basi kila aliyepo hawachi kushituka, khasa wale wanaomjuwa tangu hapo zamanai. Kwa hivyo ndugu yangu usiwe na haja ya kutafuta lengine".
 
NAMNA NILIVYOONDOKA KUUKIMBIA WATTANI WANGU
Tokea nilipokuwepo kifungoni, nilikuwa nikipanga njia za kuondoka katika Wattani wangu, Zanzibar, nikijaaliwa kuachiliwa huru kwa salama. Baada ya kutolewa gerezani Januari 12, 1972, nilianza kutafuta pasipoti lakini nilikuwa nikihangaishwa huku na huku, mwisho niliambiwa kwa njia za kiundugu zisizokuwa rasmi kuwa, "Haitokuwa rahisi kwako kupata pasipoti kwa wakati huu". Nilipoambiwa hivyo, nilianza kutupa nyavu kila kipembe. Ilipofika taarikhi 7 Mei, 1972 (mwezi mmoja tokea kuuliwa Rais wa Serikali ya Mavamizi ya Zanzibar) nilimuomba Mwenyezi Mungu nikifuatana na wenzangu wawili, Sheikh Mohammed Ali Abbas na mwanawe Ali Mohammed Ali Abbas.
 
Katika wakati huo, yaani baada ya kuuliwa Karume, usafiri wa namna yoyote ulikuwa na shida kubwa bali hata hivyo tulimuomba Mwenyezi Mungu. Ilipofika saa tatu za usiku wa taarikhi hiyo 7 Mei, tuliondoka. Kulipo pambazuka asubuhi yake, tuliingia katika moja ya bandari za kivuvi ziliopo pwani pwani ya sehemu ya bahari ya Tanganyika. Tulisali alfajiri katika msikiti wa kiambo hicho, kisha tulifungua vinywa kwa chai na maandazi katika kijikahawa kidogo kilichokuwepo hapo. Tulingojea "bas" la kuendea Tanga kwa kupitia Pangani. Kiasi cha saa mbili za asubuhi "bas" lilifika na tuliingia. Jumla yetu tulikuwa watu wane. Sisi watatu na kijana mmoja tuliyepewa na wazee atufikishe Tanga.
 
Tulipoingia katika "bas", tulimkuta kijana wa kiZanzibari kafatana na kijana wa kiTanganyika. Kijana huyu (wa kiTanganyika) alikuwa amevaa nguo za Tanu Youth League. Huyo kijana wa kiZanzibari tulijuana tulipokuwa gerezani, Langoni. Yeye alikuwa amefungwa kwa 'kumnajisi' n'gombe.

Alitulahiki kwa uzuri na tulikaa naye mpaka kufika Pangani. Tulipofika Pangani tulipokuwa tunakula chakula cha mchana, huyo kijana wa kiZanzibari alitujia kwenye meza yetu na alitwambia, "Yule mwenzangu niliyekaa naye, amewekwa sehemu hizi kuchungua watu wanaoingia kwa magendo na wenye kusafirisha karafuu kwa magendo. Alinambia kuwa ana wasiwasi juu yenu na tulipofika hapa, alitaka kukupelekeni kwenye kituo cha polisi cha hapa Pangani, mimi nimemuomba asifanye hivyo. Lakini amesema kuwa anataka kuona vitambulisho vyenu, basi nipeni nimpelekee
 
Tulipofika Tanga, tulipokelewa na ndugu yetu mpenzi ambaye tulijuana tulipokuwa kifungoni, Langoni. Ndugu yetu huyo, yeye alikuwa amefungwa kwa makosa ya kusafirisha karafuu kwa magendo. Yeye ni mzalia wa Tanga na ndiko alikokuwa akiishi. Baada ya kufika kwa mwenyeji wetu, yule ndugu yetu tuliyopewa atufikishe alituaga na alirejea Zanzibar. Sisi tulibakia hapo kwa kufanya mipango ya kuingia Mombasa, Kenya. Mwenyeji wetu huyo, alitupokea kwa uzuri sana na alitupa misaada tuliyokuwa tumeihitajia na hata tuliyokuwa hatukuhitajia.
 
Kwa kutokana na kuuliwa kwa Rais Karume, mipaka ya Tanzania na Kenya ilikuwa na ulinzi mkali sana, hata baadhi ya watu wa Idara ya Usalama kutoka Zanzibar walikuwepo katika ulinzi kwenye mpaka wa Tanzania kuingia Kenya.. Ndugu yetu huyo aliingia katika shughuli za kututafutia mipango ya kuondoka na kila njia aliyokuwa akijaribu, ilikuwa ngumu. Alifika hadi ya kutukatia vipande vya Tanu Youth League na kuwa ni Wadigo tuliyozaliwa Tanga.
 
Siku za mwanzo tu tulipofika Mombasa, tulianza kutafuta mipango ya safari yetu ya kuelekea Dubai. Lakini, kwanza tulijisalimisha kwa Mjumbe wa Umoja wa Mataifa kwa upande wa wakimbizi wa kisiasa, Sheikh Salim Muhasham. Sheikh Salim alitupokea uzuri na la mwanzo alitutengezea warka wa safari wa kutokea nchini (one way travelling document) kutoka Idara ya Uhamiaji ya Kenya, pia alikuwa akitusaidia kwa kila yaliyokuwa yanahitajia. Kwa kupata warka huo, ukaaji wetu wa hapo Kenya ulikuwa wa kihalali. Baada ya muda wa miezi mine tokea kufika hapo Mombasa, Mwenyezi Mungu alinijaalia kutengenekewa na mambo yangu na kuweza kuondoka Kenya mwanzo kuelekea Dubai kabla ya wenzangu wawili. (tulikubaliana kuwa mimi nitangulie). Niliondoka Kenya taarikhi 29 Septemba, 1972 kwa kupata msaada wa safari tokea tikti ya ndege mpaka pesa kidogo za matumizi kutoka katika mfuko wa Umoja wa Mataifa unao shughulikia wakimbizi wa kisiasa (UNHCR).
 
Kiasi cha saa mbili za usiku wa taarikh 30 Septemba, 1972 nilifika Dubai. Pamoja na miye walikuwepo wakimbizi wenzangu wengine, watoto wa Sheikh Kassim Amour Barwani na wa Sheikh Ahmed Issa Barwani. Tulipofika kiwanja cha ndege cha Dubai, tuliukuta umma wa ndugu zetu wa kiZanzibari wakitusubiri kwa hamu kutupokea. Baada ya kumaliza shughuli za Uhamiaji na Forodha hapo, tulitoka nje na huko tulianza kukumbatiana na ndugu zetu, na baada ya kuamkiana, kila mmoja kati yetu alichukuliwa na waliyokuja kumpokea. Mimi kwa usiku huo, nilipangiwa nifikie kwa ndugu yetu (aliyekuwa wakati huo ndiye Rais wa Jumuiya ya Wazanzibari "Zanzibar Asociation"), Seyyid Hashim AbdulMuttalib Hashim. Kulipokucha, yaani siku ya pili yake nilichukuliwa na ndugu yetu mwengine, Sheikh Abdalla Ali kwa majina ya umaarufu hujulikana Abdalla Baba au Abdalla Nura. Huko kwake ndiko nilikoishi kwa muda mrefu. Kila jambo langu lilikuwa hapo.
 
KULETA AHLI ZANGU DUBAI
Tokea siku niliyofika Dubai, fikra zangu, mawazo yangu na ndoto zangu zilikuwa ni kufikiria njia za kuwaleta Dubai mke wangu na wanangu ili tuishi pamoja. Uzito haukuwa juu ya kuwapatia njia ya usafiri bali juu ya kuweza kuwaondoa Zanzibar. Baada ya mimi kutoroka katika nchi yangu, ahli zangu waliwekewa vikwazo vikubwa vya kuwazuwia kuondoka kwa njia yoyote. Wakati ulipofika, Mwenyezi Mungu aliteremsha Rehema Zake. Kama msemo wa nzi, "Ukiujuwa huu, naujuwa huu". Taarikhi 28 Disemba, 1976 ahli zangu wote tokea mke wangu mpaka watoto wangu walifika Dubai kwa kupata msaada wa Umoja wa Mataifa (UNHCR).
 
Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…