Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Uzi maalum wa kupeana Likes: Comment chochote upate "Like"

Rekodi yake ya msimu huu ni mbaya zaidi, akivuna pointi saba tu katika mechi walizocheza nyumbani kwenye Ligi Kuu England na hivyo anaondoka timu ikiwa inashika nafasi ya 17 kwenye msimamo baada ya kuvuna pointi 19 katika mechi 19, ambazo wameshinda tano, sare nne na kuchapwa 10, huku wakiwa na mabao 21 ya kufunga na 32 ya kufungwa.
 
Hata hivyo, Pellegrini si kocha pekee mwenye jina kubwa kwenye soka ambaye amepoteza kazi ndani ya mwaka huu wa 2019, ambao umeshuhudia mengi ikiwamo la Liverpool kubeba mataji matatu makubwa na Jesse Lingard wa Man United kucheza mechi 28 kwenye Ligi Kuu England bila ya kufunga wala kuasisti.
 
Mauricio Pochettino – Tottenham, siku 2002
Muargentina, Mauricio Pochettino aliwashangaza wengi baada ya kufutwa kazi huko Tottenham Hotspur, timu ambayo aliifanya kuwa imara katika kipindi chake cha miaka mitano aliyokuwa na timu hiyo. Kocha huyo, ambaye msimu uliopita aliifikisha Spurs kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya, amefutwa kazi baada ya kuinoa timu hiyo kwa siku 2002, huku uamuzi huo ukifanywa Jumanne ya Novemba 19.
 
Kwa sasa Pochettino hana kazi huku kiti chake kikishikwa na Jose Mourinho huko London. Spurs kwa sasa ipo kwenye nafasi ya saba katika msimamo, ikicheza mechi 16, imeshinda sita, sare tano na vichapo vitano huku ikivuna pointi 23
 
Javi Gracia –
Watford, siku 594
Jumamosi, Septemba 7, Watford ilifanya marekebisho kwenye benchi lake la ufundi wakati ilipomfuta kazi Kocha Javi Gracia. Wababe hao wa Vicarage Road walifikia uamuzi wa kuachana na Kocha Gracia baada ya kukinoa kikosi chao kwa siku 594 na baada ya mwanzo wa hovyo kwa ligi, waliona inatosha na kumfungulia mlango wa kutokea na kuleta kocha mwingine, ambaye pia hakufua dafu na kupigwa kibuti.
 
Mwaka mbaya wa Watford ulionekana tangu mwanzoni tu mwa msimu, ambapo iliwachukua mwezi mmoja tu kwenye msimu mpya wa Ligi Kuu England kumfuta kocha wao, Gracia na baada ya kumleta mwingine, naye pia amefunguliwa mlango wa kutokea mwanzo wa mwezi huu huku timu ikiburuza mkia huko kwenye Ligi Kuu England kwa kuwa na pointi tisa tu katika mechi 16.
 
Carlo Ancelotti –
Napoli, siku 566
Kocha Mtaliano, Carlo Ancelotti kwa sasa anafanya kazi kwenye benchi la ufundi la Everton akiwa kocha mkuu na kuingoza kwenye mechi mbili za Ligi Kuu England ambapo wababe hao wa Goodison Park wameibuka na ushindi. Lakini, kabla ya hapo, kocha huyo maarufu aliyewahi kuzitoa klabu kubwa Ulaya ikiwamo Bayern Munich, Chelsea, Real Madrid, AC Milan, Paris Saint-Germain na nyinginezo, alifutwa kazi huko Napoli, alikodumu kwa siku 566 kwenye timu.
 
Unai Emery –
Arsenal, siku 555
Kichapo kutoka kwa Entracht Frankfurt kwenye Europa League uwanjani Emirates kilitosha kwa mabosi wa Arsenal kushindwa kumvumilia kocha wao, Unai Emery na kuamua kumfuta kazi. Uamuzi wa Mhispaniola huyo kufungashiwa virago vyake ulifikiwa Ijumaa, Novemba 29, ambapo kocha aliachishwa baada ya timu kucheza mechi zaidi ya saba bila ya kupata ushindi. Emery alifutwa kazi baada ya kudumu kwenye kikosi hicho cha Emirates kwa siku 555. Arsenal imemwondoa Emery na timu hiyo kwa sasa ipo chini ya Kocha Mikel Arteta, huku ikishika nafasi ya tisa kwenye msimamo wa ligi, ikicheza mechi 16, ikishinda tano, sare saba na vichapo vinne huku wakiwa wamekusanya pointi 22 tu.
 
Marco Silva –
Everton, siku 553
Alhamisi, Desemba 5, Everton ilitangaza kumfuta kazi kocha wake, Marco Silva baada ya kikosi hicho kukutambana na kipigo cha mabao 5-2 kutoka kwa mahasimu wao Liverpool kwenye mchezo wa Ligi Kuu England uliopigwa uwanjani Anfield. Kipigo hicho kwenye Merseyside derby kiliwafanya mabosi wa Everton kuona inatosha na kuachana na kocha huyo, ambaye alikuwa amedumu katika timu hiyo kwa siku 553. Everton kwa sasa ambayo ipo chini ya staa wa zamani Duncan Ferguson inashika ya 14 kwenye msimamo, ikicheza mechi 16, ikishinda tano, sare mbili na vichapo tisa, huku ikiwa imekusanya pointi 17 tu.
 
Niko Kovac –
Bayer Munich, siku 548
Miamba ya soka ya Ujerumani, Bayern Munich ni moja kati ya timu zilizoingia kwenye rekodi ya kutimua kocha ndani ya mwaka huu. Wababe hao wa Bundesliga, walimfuta kazi Niko Kovac baada ya kuona hana kitu cha maana anachokifanya kwenye timu yao na uamuzi huo ulifikiwa baada ya Bayern kuchapwa 5-1 na Entracht Frankfurt kwenye mchezo wa Bundesliga. Kovac alidumu kwenye kikosi hicho kwa kipindi cha miezi 18, ikiwa ni sawa na siku 548, ambapo kikosi hicho chini ya kocha wa muda kwa sasa kinashika nafasi ya saba kwenye msimamo baada ya kukusanya pointi 24 kwenye mechi 14, ikishinda saba, sare tatu na vichapo vinne.
 
Thierry Henry –
AS Monaco, siku 104
Baada ya kufanya vizuri akiwa kocha msaidizi katika kikosi cha Timu ya Taifa ya Ubelgiji, AS Monaco iliamua kumpa kazi staa wa zamani wa Arsenal, Thierry Henry. Kocha huyo alipewa kazi hiyo Oktoba mwaka jana wakati Monaco ilipomfuta kazi Leonardo Jardim, lakini baada ya siku 104, timu hiyo ikicheza mechi 20, hali ilizidi kuwa mbaya na mabosi wa timu hiyo hawakuwa na namna nyingine zaidi ya kumfungulia tu mlango wa kutokea supastaa huyo wa zamani wa Timu ya Taifa ya Ufaransa na klabu ya Arsenal. Kufikia Januari mwaka huu, Monaco haikuwa na habari tena na kocha huyo na kuamua kuachana naye, hivyo akiingia kwenye rekodi za makocha wenye majina makubwa ambao walipoteza kazi ndani ya mwaka huu.
 
Back
Top Bottom