Pia anashikilia rekodi kibao katika ngazi ya timu ya taifa ikiwa ni pamoja na tuzo ya mchezaji bora wa mwaka wa Canada kwa upande wa timu ya vijana ya U-17 mwaka 2016, tuzo ya mchezaji bora chipukizi wa michuano ya Concacaf Gold Cup 2017, kiatu cha dhahabu cha mfungaji bora wa Concacaf Gold Cup 2017, kujumuishwa kwenye kikosi bora cha michuano ya Concacaf Gold Cup 2017 pamoja na tuzo ya mchezaji bora wa Canada mwaka 2018.
Kwa sasa Alphonso anakunja mshahara wa Dola 24,360 kwa wiki katika kikosi cha Bayern Munich, huku taarifa mpya zikieleza kuwa huenda akaongezewa mkataba mpya kutokana na kiwango chake kuwakuna mabosi wa timu hiyo.
Alphonso ana mkataba wa miaka mitano na wababe hao wa Munich, lakini taarifa mpya zinaeleza kwamba huenda wakampatia mkataba utakaomfanya kukaa klabuni hapo kwa miaka tisa, huku dau atakalolipwa pia likipanda hadi Dola 70, 000 kwa wiki.
Nje ya soka, Alphonso ni shabiki mkubwa wa Ligi ya mpira wa Kikapu Marekani (NBA) akiwa pia ni shabiki wa mastaa kadhaa wa ligi hiyo. Vilevile anapenda michezo ya tenisi na raga, pamoja na kriketi.