“Mama namthamini thamani isiyo kifani.” Hii ni baadhi ya misemo ya Kiswahili kwenye kanga au leso za akina mama. Misemo hii inadokeza kwa namna fulani heshima anayopewa mama. Umama si heshima tu bali ni kazi.
Mama ni mzazi. Mama ni mlezi. Mama ni mwalimu. Mama ni mbeba uhai. Mama ni mbeba mimba. Mama ni mtia moyo. Mama ni mfariji. Mama ni mshauri. Mama ni mzaa chema. Mama ni mzaa mkubwa. Mama ni nguzo. Mama ni mchakalikaji.
Mama ni jiko pindi unapokuwa na njaa. Mama ni hospitali ukiwa mgonjwa. Mama ni ukumbi wa sherehe, pindi unapofurahi. Mama ni saa ya kukuamsha pindi unapolala. Mama ni dua pindi unapokuwa mbali.” Kwa kifupi, mama ana sifa ya huruma.
Upendo ni shamba la mtoto. Lakini si watoto wote wanafaidi matunda kutoka katika shamba hili. “Ni rahisi kujenga watoto shupavu kuliko kukarabati watu wazima waliovunjika,” alisema Frederick Douglass. Malezi ya watoto ni muhimu. Kuna mtoto aliyebandika kijikaratasi kwenye mlango wa chumba cha wazazi wake chenye maneno haya: “Mungu usiwape wazazi mtoto mwingine kwa vile waliye naye hawajui kumlea vizuri.” Katika mazingira kama hayo, kuna mambo ambayo hayako vizuri.
“Kuwa baba mwema na mama mwema, kunahitaji wazazi kuacha mahitaji yao na tamaa zao kwa ajili ya mahitaji ya watoto. Kama matokea ya sadaka ya namna hii, wazazi waangalifu huendeleza ubora wa tabia na hujifunza kuweka katika matendo ukweli usiojitafuta uliofundishwa na Mwokozi mwenyewe,” alisema James E. Faust.
JamiiForums uses cookies to help personalise content, tailor your experience and to keep you logged in if you register.
By continuing to use this site, you are consenting to our use of cookies.