Jifunze ni vitu gani hupaswi kufanya. Watu huwa wanajifunza vitu gani vya kufanya, lakini wanasahau somo muhimu la vitu gani vya kuepuka kufanya. Angalia makosa ambayo wengine wamefanya, halafu wewe usiyarudie makosa hayo.
Tenga muda wa kufanya kazi sana na kisha tenga muda wa mapumziko. Tenga juma moja la kupumzika kila baada ya miezi sita. Na unapotoka kwenye mapumziko, tenga tarehe ya mapumziko yanayofuata. Kadiri unavyofanya kazi sana ndivyo mwili wako unahitaji mapumziko pia, la sivyo utapata uchovu mkubwa utakaokukwamisha.
Msongo utakuua. Epuka sana msongo kwenye maisha yako. Msongo unatokana na hofu ambazo mtu anakuwa amejijengea, ondokana na hofu ulizonazo na hutakuwa na msongo. Jua kila kitu kitakwenda vizuri kama utachukua hatua sahihi.
Unapogundua una msongo mkali, jipe siku ya mapumziko, hata kama huumwi. Mapumziko haya yatapunguza msongo kwa kujiweka mbali na kazi. Lakini pia yatakuepusha kufanya makosa pale unapofanya maamuzi ukiwa na msongo.
Fuata amri kumi za Mungu, kufanya kazi siku sita na ya saba kupumzika. Tengeneza utaratibu mzuri wa kupata siku moja ya kupumzika kila juma, itakuondoa kwenye msongo na kuupa mwili utulivu.
Hakuna kinachoweza kukuzuia wewe kufanikiwa ila wewe mwenyewe. Jiamini kwamba unaweza kuwa chochote unachotaka, weka juhudi na utakuwa. Kama unafikiri unaweza na kama unafikiri huwezi, uko sahihi.
Glasi imejaa mara zote. Ipo njia ya kupima mtazamo wa mtu, kwa kuweka maji nusu glasi kisha kumuuliza mtu aeleze glasi na maji. Wenye mtazamo chanya wanasema glasi imejaa nusu, wenye mtazamo hasi wanasema glasi iko tupu nusu. Wenye mtazamo wa kujiamini wanaona glasi imejaa mara zote. Mara zote chukulia kile unachokutana kwa mtazamo chanya na jiulize unawezaje kunufaika nacho zaidi.
Maisha yenye mlinganyo yanaleta ufanisi mkubwa kwenye biashara. Tumia vizuri muda wako, kuwa na vipaumbele sahihi kwako na usiahirishe yale muhimu. Fanya yale muhimu tu na mengine achana nayo. Una muda wa kufanya kila kitu kama utautumia vizuri.
Epuka sana watu waliokata tamaa, watu ambao hawakazani kufanikiwa, watu wanaolalamika na kulaumu wengine. Watu wa aina hii watanyonya nguvu zako za mafanikio na hutaweza kupiga hatua.
Usijilinganishe na mtu mwingine yeyote, wewe ndiye mtu bora kabisa kuwahi kutokea hapa duniani, hakuna ambaye amewahi kuwepo na wala hatakuja kuwepo. Jua wewe ni wa kipekee na muhimu, hivyo usijilinganishe na yeyote. Jua utofauti wako na utumie huo.
Hakuna mtu mwenye akili kukuzidi wewe. Vitu vyote vikubwa unavyoona vimefanywa, vimefanywa na watu ambao hawajakuzidi sana akili. Hii ina maana na wewe ukiweka juhudi utaweza kufanya makubwa pia.
Uwazi unajenga uaminifu. Kwa kila unachofanya, kuwa na uwazi wa asilimia 100. Usifiche kitu chochote kwenye biashara yako, mweleze mteja ukweli kuhusu kile unachomuuzia. Ukimdanganya kuna siku atakuja kujua na utaharibu kabisa mahusiano yenu ya kibiashara.
Usiwaamini watu ambao siyo waaminifu. Usifanye biashara na watu ambao wanawasaliti wapenzi au wenza wao. Kwa sababu kama wanaweza kuwasaliti watu wa karibu kwao, hawatashindwa kukusaliti wewe kwenye mambo muhimu ya biashara. Pia usiwaamini watu ambao wanawasema wengine vibaya kwako, jua wakienda kwa wengine wanakusema wewe vibaya pia.
Njia nne za kujua kama mtu anadanganya;
Moja; anatoa maelezo marefu kwa swali linalohitaji jibu la ndiyo au hapana.
Mbili; hakuangalii machoni wakati anaongea.
Tatu; anaweka mkono wake mdomoni wakati anaongea.
Nne; anatikisa mguu wake wakati anaongea.
Unaweza kujenga jina lako kwa miaka 30, halafu ukalivunja kwa sekunde 30 tu. Kuwa makini na kila unachofanya, hasa kwenye mitandao ya kijamii, unaweza kufanya kitu kidogo na kikawa na madhara makubwa sana kwako.
UNASHINDA VITA KABLA HATA HUJAINGIA KWENYE MAPAMBANO.
Weka maandalizi makubwa kwenye chochote unachofanya. Kama mshindani wako anatumia masaa 5 kujiandaa kwa kitu, wewe tumia masaa 50. Mara zote weka maandalizi makubwa kwenye chochote unachofanya kuliko wengine wanavyoweka na hilo litakupa nafasi kubwa ya mafanikio.
Zoezi rahisi la kupata wafanyakazi bora au wewe mwenyewe kuwa mfanyakazi bora. Zoezi hili lina maswali manne, ambapo kama majibu ni ndiyo kwenye maswali yote basi mtu huyo ni bora. Kama kuna jibu la hapana, mtu huyo siyo bora. Maswali hayo ni kama ifuatavyo;
Moja; je anafurahia kufanya kazi kwenye kampuni hiyo?
Mbili; je mtu anatumia muda mwingi kusikiliza kuliko kuongea?
Tatu; je wanauliza wengine maswali zaidi na kuwasikiliza wakijieleza?
Nne; je ni watu wanaoaminika?